Masomo ya Misa
Ijumaa ya Oktava ya Pasaka (Ijumaa, Aprili 26, 2019)
Mdo 4:1-12
Petro na Yohane walipokuwa wakisema na watu wale, makuhani na akida wa hekalu na Masadukayo wakawatokea, wakifadhaika sana kwa sababu wanawafundisha watu na kuhubiri katika Yesu ufufuo wa wafu. Wakawakamata, wakawaweka gerezani hata asubuhi; kwa kuwa imekwisha kuwa jioni. Lakini wengi katika hao waliosikia lile neno waliamini; na hesabu ya watu waume ikawa kama elfu tano. Hata asubuhi wakubwa na wazee na waandishi wakakusanyika Yerusalemu, na Anasi Kuhani Mkuu, na Kayafa pia, na Yohane na Iskanda, na wote wale waliokuwa jamaa zake Kuhani Mkuu. Walipowaweka katikati wakawauliza, Kwa nguvu gani na kwa jina la nani ninyi mmefanya haya? Ndipo Petro, akijaa Roho Mtakatifu, akawaambia, Enyi wakubwa wa watu na wazee wa Israeli, kama tukiulizwa leo habari ya jambo jema alilofanyiwa yule mtu dhaifu, jinsi alivyoponywa, jueni ninyi nyote na watu wote wa Israeli ya kuwa kwa jina la Yesu Kristo wa Nazareti, ambaye ninyi mlimsulibisha, na Mungu akamfufua katika wafu, kwa jina hilo mtu huyu anasimama ali mzima mbele yenu. Yeye ndiye jiwe lile lililodharauliwa na ninyi waashi, nalo limewekwa kuwa jiwe kuu la pembeni. Wala hakuna wokovu katika mwingine awaye yote, kwa maana hapana jina jingine chini ya mbingu walilopewa wanadamu litupasalo sisi kuokolewa kwalo.
Zab 118:1-2, 4, 22-27
Haleluya. Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema,
Kwa maana fadhili zake ni za milele.
Israeli na aseme sasa,
Ya kwamba fadhili zake ni za milele.
Wamchao Bwana na waseme sasa,
Ya kwamba fadhili zake ni za milele.
(K)Jiwe walilolikataa waashi, Limekuwa jiwe kuu la pembeni.
Jiwe walilolikataa waashi
Limekuwa jiwe kuu la pembeni.
Neno hili limetoka kwa Bwana,
Nalo ni ajabu machoni petu.
Siku hii ndiyo aliyoifanya Bwana,
Tutashangilia na kuifurahia.
(K)Jiwe walilolikataa waashi, Limekuwa jiwe kuu la pembeni.
Ee Bwana, utuokoe, twakusihi;
Ee Bwana, utufanikishe, twakusihi.
Na abarikiwe yeye ajaye kwa jina la Bwana;
Tumewabarikia toka nyumbani mwa Bwana.
Bwana ndiye aliye Mungu, Naye ndiye aliyetupa nuru.
(K)Jiwe walilolikataa waashi, Limekuwa jiwe kuu la pembeni.
Yn 21:1-14
Baada ya hayo Yesu alijidhihirisha tena kwa wanafunzi wake, penye bahari ya Tiberia, naye alijidhihirisha hivi. Simoni Petro, na Tomaso aitwaye Pacha, na Nathanaeli wa Kana ya Galilaya, na wana wa Zebedayo, na wengine wawili wa wanafunzi wake, walikuwapo pamoja. Simoni Petro aliwaambia, Naenda kuvua samaki. Nao wakamwambia, Sisi nasi tutakwenda nawe. Basi wakaondoka, wakapanda chomboni; ila usiku ule hawakupata kitu. Hata asubuhi kulipokucha, Yesu alisimama ufuoni; walakini wanafunzi hawakujua ya kuwa ni Yesu. Basi Yesu akawaambia, Wanangu, mna kitoweo? Wakamjibu, La. Akawaambia, Litupeni jarife upande wa kuume wa chombo, nanyi mtapata. Basi wakatupa; wala sasa hawakuweza kulivuta tena kwa sababu ya wingi wa samaki. Basi yule mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda akamwambia Petro, Ndiye Bwana. Naye Simoni Petro, aliposikia ya kwamba ni Bwana, akajifunga vazi lake, (maana alikuwa uchi), akajitupa baharini. Na hao wanafunzi wengine wakaja katika mashua; maana hawakuwa mbali na nchi kavu; ila yapata dhiraa mia mbili; huku wakilikokota lile jarife lenye samaki. Basi waliposhuka pwani, wakaona huko moto wa makaa, na juu yake pametiwa samaki, na mkate. Yesu akawaambia, Leteni hapa baadhi ya samaki mliowavua sasa hivi. Basi Simoni Petro akapanda chomboni, akalivuta jarife pwani, limejaa samaki wakubwa, mia hamsini na watatu; na ijapokuwa ni wengi namna hiyo, jarife halikupasuka. Yesu akawaambia, Njoni mfungue kinywa. Wala hakuna mtu katika wale wanafunzi aliyethubutu kumwuliza, U nani wewe? Wakijua ya kuwa ni Bwana. Yesu akaenda akautwaa mkate, akawapa, na samaki vivyo hivyo. Hiyo ndiyo mara ya tatu ya Yesu kuonekana na wanafunzi wake baada ya kufufuka katika wafu.
Maoni
Ingia utoe maoni