Masomo ya Misa
Ijumaa ya 7 ya Mwaka (Ijumaa, Mei 20, 2016)
Yak 5:9-12
Ndugu, msinung'unikiane, msije mkahukumiwa. Angalieni, mwamuzi amesimama mbele ya milango. Ndugu, watwaeni manabii walionena kwa jina la Bwana, wawe mfano wa kustahimili mabaya, na wa uvumilivu. Angalieni, twawaita heri wao waliosubiri. Mmesikia habari ya subira yake Ayubu, mmeuona mwisho wa Bwana ya kwamba Bwana ni mwingi wa rehema, mwenye huruma. Lakini zaidi ya yote, ndugu zangu, msiape, wala kwa mbingu wala kwa nchi; wala kwa kiapo kinginecho chote; bali ndiyo yenu na iwe ndiyo, na siyo yenu iwe siyo, msije mkaangukia hukumu.
Zab 103:1-4, 8-9, 11-12
Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana. Naam, vyote vilivyo ndani yangu Vilihimidi jina lake takatifu.
Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana, Wala usizisahau fadhili zake zote.
(K)Bwana amejaa huruma na neema.
Akusamehe maovu yako yote, Akuponya magonjwa yako yote,
Aukomboa uhai wako na kaburi, Akutia taji ya fadhili na rehema,
(K)Bwana amejaa huruma na neema.
Bwana amejaa huruma na neema, Haoni hasira upesi, ni mwingi wa fadhili.
Yeye hatateta sikuzote, Wala hatashika hasira yake milele.
(K)Bwana amejaa huruma na neema.
Maana mbingu zilivyoinuka juu ya nchi, Kadiri ile ile rehema zake ni kuu kwa wamchao.
Kama mashariki ilivyo mbali na magharibi, Ndivyo alivyoweka dhambi zetu mbali nasi.
(K)Bwana amejaa huruma na neema.
Yn 17: 17b, 17a
Aleluya, Aleluya
Neno lako ndiyo kweli,
Uwatakase kwa ile kweli;
Aleluya
Mk 10:1-12
Yesu alifika mipakani mwa Uyahudi, na ng'ambo ya Yordani; makutano mengi wakakutanika tena wakamwendea; akawafundisha tena kama alivyozoea. Basi Mafarisayo wakamwendea, wakamwuliza, Je! Ni halali mtu kumwacha mkewe? Huku wakimjaribu. Naye akajibu, akawaambia, Musa aliwaamuru nini? Wakasema, Musa alitoa ruhusa kuandika hati ya talaka na kumwacha. Yesu akawaambia, Kwa sababu ya ugumu wa mioyo yenu aliwaandikia amri hii. Lakini tangu mwanzo wa kuumbwa ulimwengu, aliwafanya mume na mke. Kwa sababu hiyo mtu atamwacha babaye na mamaye, ataambatana na mkewe; na hao wawili watakuwa mwili mmoja; hata wamekuwa si wawili tena, bali mwili mmoja. Basi alichokiunganisha Mungu, mwanadamu asikitenganishe. Hata nyumbani tena wanafunzi wakamwuliza habari ya neno hilo. Akawaambia, Kila mtu atakayemwacha mkewe na kuoa mwingine azini juu yake; na mke, akimwacha mumewe na kuolewa na mtu mwingine, azini.
Maoni
Ingia utoe maoni