Jumanne. 26 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumatano ya 6 ya Mwaka (Jumatano, Februari 20, 2019)  

Somo la 1

Mwa. 8:6 – 13, 20 – 22

Ikawa baada ya siku arobaini, Nuhu akalifungua dirisha la safina, alilolifanya; akatoa kunguru, naye akatoka akaenda huko na huko, hata maji yakakauka juu ya nchi. Kisha akatoa njiwa, aone kwamba maji yamepunguka usoni pa nchi; bali yule njiwa hakuona mahali pa kutua kwa wayo wa mguu wake, akamrudia Nuhu safinani, maana maji yalikuwa juu ya uso wa nchi yote; naye akanyosha mkono, akamtwaa, akamwingiza mle safinani. Akangoja na siku saba tena, akamtoa yule njiwa katika safina mara ya pili, njiwa akamjia jioni, na tazama, alikuwa na jani bichi la mzeituni kinywani mwake, ambalo amelitunda, basi Nuhu akajua ya kwamba maji yamepunguka juu ya nchi. Akangoja na siku saba tena, akamtoa yule njiwa; naye asimrudie tena kamwe. Ikawa mwaka wa mia sita na moja, mwezi wa kwanza, siku ya kwanza ya mwezi, maji yalikauka juu ya nchi. Nuhu akaondoa kifuniko cha safina, naye akaona, na tazama, uso wa nchi umekauka. Nuhu akamjengea Bwana madhabahu; akamtwaa katiak kila mnyama aliye safi, na katika kila ndege aliye safi, akavitoa sadaka za kuteketezwa juu ya madhabahu. Bwana akasikia harufu ya kumridhisha; Bwana akasema moyoni, Sitailaani nchi tena baada ya hayo kwa sababu ya wanadamu, maana mawazo ya moyo wa mwanadamu ni mabaya tangu ujana wake; wala sitapiga tena baada ya hayo kila kilicho hai kama nilivyofanya. Muda nchi idumupo, majira ya kupanda, na mavuno, wakati wa baridi na wakati wa hari, wakati wa kaskazini na wakati wa kusi, mchana na usiku, havitakoma.

Wimbo wa Katikati

Zab. 116:12 – 15, 18 – 19

Nimrudishie Bwana nini
Kwa ukarimu wake wote alionitendea?
Nitakipokea kikombe cha wokovu,
Na kulitangaza jina la Bwana.
(K) Nitakutolea dhabihu ya kushukuru, ee Bwana.

Nitaziondoa nadhiri zangu kwa Bwana,
Naam, mbele ya watu wake wote.
Ina thamani machoni pa Bwana
Mauti ya wacha Mungu wake.
(K) Nitakutolea dhabihu ya kushukuru, ee Bwana.

Nitaziondoa nadhiri zangu kwa Bwana,
Naam, mbele ya watu wake wote,
Katika nyua za nyumba ya Bwana,
Ndani yako, ee Yerusalemu.
(K) Nitakutolea dhabihu ya kushukuru, ee Bwana.

Shangilio

Efe. 1:19 – 27

Aleluya, aleluya,
Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo ayatie nuru macho ya mioyo yetu, tujue tumaini la mwito wetu jinsi lilivyo.
Aleluya.

Injili

Mk. 8:22 – 26

Siku ile, Yesu na wanafunzi wake, wakafika Bethsaida, wakamletea kipofu, wakamsihi amguse. Akamshika mkono yule kipofu, akamchukua nje ya kijiji, akamtemea mate ya macho, akamwekea mikono yake, akamwuliza, Waona kitu? Akatazama juu, akisema, Naona watu kama miti, inakwenda. Ndipo akaweka tena mikono yake juu ya macho yake, naye akatazama sana; akawa mzima, akaona vyote waziwazi. Akampeleka nyumbani kwake akisema, Hata kijijini usiingie.

Maoni


Ingia utoe maoni