Jumanne. 26 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

Jumanne ya 1 ya Mwaka (Jumanne, Januari 15, 2019)  

Somo la 1

Ebr 2:5-12

Mungu hakuuweka chini ya malaika ulimwengu ule ujao tunaounena, ila mtu mmoja ameshuhudia hivi mahali fulani, akisema, Mwanadamu ni nini hata umkumbuke, Ama mwana wa binadamu, hata umwangalie? Umemfanya mdogo punde kuliko malaika, Umemvika taji ya utukufu na heshima, Umemtawaza juu ya kazi za mikono yako; Umeweka vitu vyote chini ya nyayo zake. Kwa maana katika kuweka vitu vyote chini yake hakusaza kitu kisichowekwa chini yake. Lakini sasa bado hatujaona vitu vyote kutiwa chini yake. ila twamwona yeye aliyefanywa mdogo punde kuliko malaika, yaani, Yesu, kwa sababu ya maumivu ya mauti, amevikwa taji ya utukufu na heshima, ili kwa neema ya Mungu aionje mauti kwa ajili ya kila mtu. Kwa kuwa ilimpasa yeye, ambaye kwa ajili yake na kwa njia yake vitu vyote vimekuwapo, akileta wana wengi waufikilie utukufu, kumkamilisha kiongozi mkuu wa wokovu wao kwa njia ya mateso. Maana yeye atakasaye na hao wanaotakaswa wote pia watoka kwa mmoja. Kwa ajili hii haoni haya kuwaita ndugu zake; akisema, Nitalihubiri jina lako kwa ndugu zangu; Katikati ya kanisa nitakuimbia sifa.

Wimbo wa Katikati

Zab 8:2, 5-9

Vinywani mwa watoto wachanga na wanyonyao Umeiweka misingi ya nguvu;
Kwa sababu yao wanaoshindana nawe;
Uwakomeshe adui na mijilipiza kisasi.
Umemfanya mdogo punde kuliko Mungu;
Umemvika taji ya utukufu na heshima;
(K) Umemtawaza mwanao juu ya kazi ya mikono yako.

Umemtawaza juu ya kazi za mikono yako;
Umevitia vitu vyote chini ya miguu yake.
Kondoo, na ng'ombe wote pia;
Naam, na wanyama wa kondeni;
(K) Umemtawaza mwanao juu ya kazi ya mikono yako.

Ndege wa angani, na samaki wa baharini;
Na kila kipitacho njia za baharini.
Wewe, MUNGU, Bwana wetu, Jinsi lilivyo tukufu jina lako duniani mwote!
(K) Umemtawaza mwanao juu ya kazi ya mikono yako.

Shangilio

Ebr. 4:12

Aleluya, aleluya,
Neno la Mungu li hai tena li na nguvu, li jepesi kuyatambua mawazo na makusudi ya moyo.
Aleluya.

Injili

Mk 1:21-28

Yesu na wanafunzi wake walishika njia mpaka Kapernaumu, na mara siku ya sabato akaingia katika sinagogi, akafundisha. Wakashangaa mno kwa mafundisho yake; kwa maana alikuwa akiwafundisha kama mtu mwenye amri, wala si kama waandishi. Na mara palikuwapo ndani ya sinagogi lao mtu mwenye pepo mchafu; akapaza sauti, akisema, Tuna nini nawe, Yesu wa Nazareti? Je! Umekuja kutuangamiza? Nakutambua u nani, Mtakatifu wa Mungu. Yesu akamkemea, akisema, Fumba kinywa, umtoke. Yule pepo mchafu akamtia kifafa, akalia kwa sauti kuu, akamtoka. Wakashangaa wote, hata wakaulizana, wakisema, Nini hii? Ni elimu mpya! Maana kwa uweza awaamuru hata pepo wachafu, nao wamtii! Habari zake zikaenea mara kotekote katika nchi zote kandokando ya Galilaya.

Maoni


Ingia utoe maoni