Jumanne. 26 Novemba. 2024

Masomo ya Misa

KUMBUKUMBU YA MT. JOSAFATI (Jumatatu, Novemba 12, 2018)  

Somo la 1

Tit. 1:1 – 9

Paulo, mtumwa wa Mungu, na mtume wa Yesu Kristo; kwa ajili ya Imani ya wateule wa Mungu, na ujuzi wa kweli ile iletayo utauwa; katika tumaini la uzima wa milele, ambao Mungu asiyeweza kusema uongo aliuahidi tangu milele; akalifunua neno lake kwa majira yake katika ule ujumbe niliowekewa amana mimi kwa amri ya Mwokozi wetu Mungu; kwa Tito, mwanangu hasa katika Imani tuishirikiyo. Neema na iwe kwako na amani zitokazo kwa Mungu Baba na kwa Kristo Yesu Mwokozi wetu. Kwa sababu hii nalikuacha Krete, ili uyatengeneze yaliyopunguka, na kuweka wazee katika kila mji kama vile nilivyokuamuru; kiwa mtu hakushitakiwa neno, naye ni mume wa mke mmoja, ana watoto waaminio, wasioshitakiwa kuwa ni wafisadi wala wasiotii. Maana imempasa askofu awe mtu asiyeshitakiwa neno, kwa kuwa ni wakili wa Mungu; asiwe mtu wa kujipendekeza nafsi yake, asiwe mwepesi wa hasira, asiwe mlevi wala mgomvi, asiwe mpenda mapato ya aibu; bali awe mkaribishaji, mpenda wema, mwenye kiasi, mwenye haki, mtakatifu, mwenye kudhibiti nafsi yake; akilishika lile neno la Imani vile vile kama alivyofundishwa, apate kuweza kuwaonya watu kwa mafundisho yenye uzima, na kuwashinda wenye kupinga.

Wimbo wa Katikati

Zab. 24: 1 – 6

Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana,
Dunia na wote wakaao ndani yake.
Maana ameiweka misingi yake juu ya bahari,
Na juu ya mito ya maji aliithibitisha.
(K) Hiki ndicho kizazi cha wakutafutao, Ee Bwana.

Ni nani atakayepanda katika mlima wa Bwana?
Ni nani atakayesimama katika patakatifu pake?
Mtu aliye na mikono safi na moyo mweupe,
Asiyeiinua nafsi yake kwa ubatili.
(K) Hiki ndicho kizazi cha wakutafutao, Ee Bwana.

Atapokea Baraka kwa Bwana,
Na haki kwa Mungu wa wokovu wake.
Hiki ndicho kizazi cha wamtafutao,
Wakutafutao uso wako, Ee Mungu wa Yakobo.
(K) Hiki ndicho kizazi cha wakutafutao, Ee Bwana.

Shangilio

1Sam. 3:9, Yn. 6:68

Aleluya, aleluya,
Nena, Bwana, kwa kuwa mtumishi wako anasikia: wewe unayo maneno ya uzima wa milele.
Aleluya.

Injili

Lk. 17:1 – 6

Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Makwazo hayana budi kuja, lakini ole wake mtu yule ambaye yaja kwa sababu yake! Ingemfaa zaidi mtu huyo jiwe la kusaga lifungwe shingoni mwake, akatupwe baharini, kulikko kumkosesha mmojawapo wa wadogo hawa. Jilindeni. Kama ndugu yako akikosa, mwonye; akitubu msamehe. Na kama akikukosa mara saba katika siku moja, na kurudi kwako mara saba, akisema, Nimetubu, msamehe. Mitume wakamwambia Bwana, Tuongezee Imani. Bwana akasema, Kama mngekuwa na Imani kiasi cha chembe ya haradali, mngeuambia mkuyu huu, Ng’oka ukapandwe baharini, nao ungewatii.

Maoni


Ingia utoe maoni