Alhamisi. 21 Novemba. 2024
feature-top
Umuhimu wa Majiundo ya Kiliturujia kwa Watu wa Mungu: Ili Mwenyezi Mungu atukuzwe na mwanadamu atakatifuzwe

Mama Kanisa anatamani sana waamini wote waongozwe kwenye kuyashiriki maadhimisho ya Liturujia kwa utimilifu, kwa ufahamu na utendaji! Hii ndiyo tabia ya Liturujia na kwa sababu ya Sakramenti ya Ubatizo, ni haki na wajibu wa waamini ambao kimsingi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki wa Mungu. Liturujia ni chemchemi ya roho ya kweli ya kikristo.

Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican walifanya mabadiliko makubwa katika maisha na utume wa Kanisa katika Liturujia kwa kutambua nafasi ya Liturujia katika Fumbo la Kanisa, kwani Liturujia ni chemchemi na kilele cha maisha na utume wa Kanisa. Kanisa, kimsingi lina asili mbili ile ya Kimungu kwa sababu limeanzishwa na Kristo Yesu na kibinadamu kwa sababu linawaambata binadamu. Hivyo Liturujia ya kila siku inawajenga wale waliomo katika Kanisa wawe Hekalu la Roho Mtakatifu, Makao ya Mungu katika Roho, mpaka kuufikia utimilifu wa Kristo.

Liturujia inaimarisha nguvu za waamini kumtangaza na kumshuhudia Kristo. Lengo ni umoja na mshikamano wa watoto wa Kanisa. Liturujia ni muhimu kwa ajili ya kumtukuza Mwenyezi Mungu na mwanadamu kutakatifuzwa kwa njia ya Kristo Yesu. Liturujia ni utekelezaji wa kazi ya Kikuhani ya Kristo Yesu. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanasema, katika Liturujia, Ibada halisi za hadhara huadhimishwa na Mwili wa Fumbo wa Kristo Yesu, yaani Kanisa. Hili ni tendo takatifu katika maisha na utume wa Kanisa.

Mama Kanisa anaendelea kuwachangamotisha viongozi wa Kanisa kuhakikisha kwamba, wanajikita katika malezi makini ya Kiliturujia pamoja na ushiriki hai wa waamini. Ni Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican waliotambua na kuthamini umuhimu wa kutafsiri vitabu vya Liturujia ili Ibada mbali mbali ziweze kufahamika na wengi: kwa kukazia ukamilifu na ufahamu wa Ibada inayoadhimishwa. Liturujia irekebishwe kulingana na hali za watu na Mapokeo yao, kwa maneno mengine, huu ulikuwa ni mwanzo wa jitihada za utamadunisho wa Liturujia katika uhalisia wa maisha ya waamini sehemu mbali mbali za dunia.

Mama Kanisa anatamani sana waamini wote waongozwe kwenye kuyashiriki maadhimisho ya Liturujia kwa utimilifu, kwa ufahamu na utendaji! Hii ndiyo tabia ya Liturujia na kwa sababu ya Sakramenti ya Ubatizo, ni haki na wajibu wa waamini ambao kimsingi ni mzao mteule, ukuhani wa kifalme, taifa takatifu, watu wa milki wa Mungu. Liturujia ni chemchemi ya kwanza ambayo mwamini anaweza kuchota roho ya kweli ya kikristo. Ni kutokana na changamoto hizi, Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa, kuanzia tarehe 12-15 Februari 2019 linafanya mkutano wake wa mwaka, unaoongozwa na kauli mbiu “Majiundo ya Kiliturujia kwa Watu wa Mungu”.

Huu ni mkutano unaohudhuriwa na Makardinali 22, Maaskofu wakuu 8 na Maaskofu 11 kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Kati ya mada zinazojadiliwa ni pamoja na: Taalimungu ya Liturujia; Liturujia inaliunda Kanisa Mahalia pamoja na “Majiundo ya kiakili na maisha ya kiroho kwa majandokasisi pamoja na wakleri”. Wajumbe watapata nafasi ya majadililiano katika vikundi kuhusu mada zinazowasilishwa. Tarehe 14 Februari 2019, baada ya maadhimisho ya Misa Takatifu itakayoongozwa na Kardinali Robert Sarah, Mwenyekiti Baraza la Kipapa la Ibada na Nidhamu ya Sakramenti za Kanisa, wajumbe watapata nafasi ya kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko na hatimaye, jioni, watahitimisha na mapendekezo yatakayokuwa yametolewa kwenye majadiliano ya vikundi, kwa kuyapigia kura, tayari kuwasilishwa kwa Baba Mtakatifu kwa ajili ya tathmini na utekelezaji wake.


Maoni


Ingia utoe maoni