Jumatatu. 13 Mei. 2024
feature-top
Papa Fransisko amepokelea na mrithi wa kiti cha mfalme wa Abu Dhabi

Papa Francis amewasili katika Umoja wa falme za kiarabu kwa ziara ya kwanza kuwahi kufanyika na kiongozi mkuu katika kanisa katoliki Roma, katika rasi ya Arabuni.

Alitua mjini Abu Dhabi ambako alikaribishwa na mwanamfalme Sheikh Mohammed bin Zayed al-Nahyan.

Papa anatarajiwa kuhudhuria mkutano wa dini mbali mbali na Jumanne aandae misa ambapo takriban watu 120,000 wanatarajiwa kuhudhuria.

Kabla ya kuondoka alielezea wasiwasi wake kuhusu vita nchini Yemen ambapo Umoja wa Falme za kiarabu umehusika.

"Raia nchini Yemen wamechoshwa na mzozo wa muda mrefu na watoto wengi wanateseka kwa njaa, lakini hawawezi kufikia maghala ya chakula ," Papa amesema

"Kilio cha watoto na wazazi wao kinapaa mbinguni kwa Mngu," aliongeza.

Haijulikani wazi iwapo anapanga kulizusha suala hilo mbele ya umma au katika faragha wakati wa ziara yake. Umoja wa Falme za kiarabu unahusika katika mzozo nchini Yemen kama sehemu ya muungano unaoongozwa na Saudia.

Kwanini ziara ya Papa ni muhimu Arabuni?

Kuna takriban watoliki milioni moja katika Umoja huo wa Falme za kiarabu, wengi wao kutoka Ufilipino na nchini India.

Baadhi tayari wamekuwa wakisimama kusubiri misa hiyo ya hapo kesho Jumanne. Mmoja ameliambia shirika la habari la AFP kwamba ziara ya Papa "inafungua milango kwa mazungumzo kuhusu kuvumiliana, ujumbe ambao dunia nzima unahitaji kuusikia".

Katika ujumbe kwenye video alioutoa siku ya Alhamisi, Papa alisema : "Imani kwa Mungu inaunganisha watu na haiwatenganishi, inatufanya kuwa karibu licha ya tofuati zetu, inatutenga na uhasama na maovu."

Alitoa heshima zake kwa Umoja huo wa flame za kaiarabu kuwa "nchi ambayo inajaribu kuwa mfano wa watu kuishi pamoja, mfano wa udugu, na eneo lililo na raia wa tabaka na tamaduni mbali mbali ".

Akiwa Abu Dhabi, Papa anatarajiwa pia kufanya mkutano na Sheikh Ahmed al-Tayeb, Imamu mkuu wa mskiti wa al-Azhar Cairo, ambao ni wadhifa mkuu wa mafunzo ya kidini kwa madhehebu ya Sunni kwa waislamu.

Mwandishi wa BBC aliyepo Abu Dhabi, anasema Vatican inatarajia kuwa ziara ya Papa itasaidia kulainisha vikwazo dhidi ya ujenzi wa makanisa katika enoe hilo, hususan katika eneo jirani Saudi Arabia ambako hakuna maeneo yanayoruhusiwa ya kuabudu kwa wasio waislamu.

Maafisa wa Vatican wanasema wanahitaji kuwa na uwepo mzito katika Umoja huo wa Falme za kiarabu, kusimamia jamii ya wakatoliki huko.

"Tumelemewa sana. Tunahitaji makanisa zaidi. Tunahitaji makasisi zaidi," afisa mmoja amenukuliwa na shirika la habari la Reuters.


Maoni


Ingia utoe maoni