Tarehe 31 Januari 2019 wamepokelewa katika uwanja wa ndege wa Fiumicino, Roma kikundi cha wakimbizi waliofikia kwa njia ya Protokali zilizokubaliwa na Serikali ya Italia na kusainiwa na Baraza la Maaskofu katoliki Italia, katika kitengo cha Caritas na Mfuko wa Wahamiaji (Migrantes) na Jumuiya ya Mtakatifu Egidio ili kusaidia wakimbizi na wahamiaji kuingia salama, halali kisheria katika nchi. Hawa ni watu 85 na walio wengi ni kutoka Pembe ya Afrika ambao wamepokelewa katika baadhi ya majimbo 15 katoliki ya Italia. Kati ya wakimbizi waliofika, wapo hata familia nzima na watoto kama kumi, na aliye mdogo zaidi hajafikisha hata mwaka mmoja. Kwa mujibu wa Protokali na msaada wa Baraza la Maaskofu Italia hadi sasa wamewezesha kuhamisha wakimbizi 500 kutoka nchini Ethiopia kwa mika 2 tu. Yote hiyo ni shukrani kwa ukarimu wa majimbo, familia na mashirika ya watawa. Vile vile hata matumizi ya majengo binafsi, kwa kusaidiwa na wataalam wa masuala ya familia katika kusindikiza mchakato mzima wa ushirikishwaji kijamii na kazi ya kila mmoja katika eneo ili kuhakikisha huduma,mafunzo ya lugha ya kiitaliano na matibabu yanayostahili.
Wakimbizi na wahamiaji bado ni tatizo kubwa
Bado kuna wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani kote ambapo ni pamoja na kuibuka kwa misimamo mikali ya kisiasa ambayo haiwezi kamwe kuleta maendeleo ya nchi yoyote zaidi ya machafuko na umasikini katika nchi mahalia. Pamoja na hayo bado kuna ubaguzi na chuki dhidi ya wageni ambao kwa sasa ni kati ya changamoto zinazoendelea kutishia mpango wa mkakati wa Kanisa katika huduma kwa wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum. Vile vile suala la kutisha ni lile la kuwa na baadhi ya viongozi wa kisiasa wanaotaka umaarufu wa kisiasa kwa kutoa sauti zenye ukali dhidi ya wakimbizi na wahamiaji, lakini yote hiyo ni woga na ukosefu wa utambuzi wa nini maana maisha ya mwanadamu ambaye daima yuko katika safari.
Kwa kutazama ujumbe wa Baba Mtakatifu Francisko wa hivi karibuni wa amani amesema siasa safi ni chombo cha huduma ya haki, amani, ustawi na maendeleo fungamani ya binadamu. Akiwa na maana ya kwamba watu wote wanahamasishwa kushiriki kikamilifu katika mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu ambao kwa dhati unajikita katika kiini cha haki, amani na upendo vitu ambavyo vinahitaji uongofu wa kweli wa ndani ambao unatambua sura ya Mungu kama mfano wa kila mtu tunayekutana naye. Baba Mtakatifu anakazia kuwa na ufunguzi wa mioyo ili kuweza kujenga madaraja yanayowakutanisha watu: kitamaduni, kidini na kiutu, kwa kutambua kwamba, wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu na wala tofauti zao msingi zisiwe ni kisingizio cha vita, kinzani na mipasuko ya kijamii na kifamilia. Ni kwa njia ya kujenga umoja na mshikamano ambao unaweza kusitisha ubaguzi wa ndugu hawa wakimbizi na wahamiaji.
Maoni
Ingia utoe maoni