Alhamisi. 21 Novemba. 2024
feature-top
Rais Paul Kagame wa Rwanda amechaguliwa kushika nafasi ya uenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki

Jumuiya ya Afrika Mashariki imemchagua Rais Paul Kagame kushika nafasi ya Uenyekiti kwa mwaka mmoja.Jumuiya hiyo inaundwa na nchi ya Uganda,Kenya,Rwanda,Burundi,Tanzania na Sudan Kusini

Rais wa nchi ya Rwanda Bwana Paul Kagame amekubali kuwa Mwenyekiti mpya wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Ijumaa tarehe 1 Januari 2019. Ameshika nafasi hiyo aliyoachiwa na Rais Museven wa Uganda wakiwa katika Mkutano wa wakuu wa jumuiya hizo mjini Arusha Tanzania. Na wakatu wa kukabidhiwa nafasi hiyo amewashukuru marais wenzake kwa kumpatia dhamana hiyo ambapo ameahidi kutumikia nafasi hiyo ipasavyo. Rais Kagame amesema: “ninayo heshima kutumikia nafasi hii kwa kipindi cha mwaka mmoja. Natarajia kufanya kazi kwa ushirikiano wa pamoja na viongozi wenzangu kuwatumikia watu wa Afrika Mashariki". Aidha akiendelea na hotuba yake ya kupokea uongozi huo, Mwenyekiti mpya amemshukuru Rais Yoweri Museveni wa Uganda, aliyemaliza muda wake baada ya kuwa mwenyekiti wa Jumuiya ya nchi za Afrika Mashariki kwa kipindi cha miaka miwili. Rais Kagame amependa kumthibitishia pia ukaribu na Rais Kenyatta na watu wa Kenya katika kupambana na ugaidi Afrika Mashariki. "Hii ni fursa ya kuweza kukabiliana na changamoto zilizo kuwepo moja kwa moja ambazo zinaikabili jumuiya na kwa ukweli, ili sote kwa pamoja tuweze kusonga mbele”, amesema Rais Kagame.

Mafanikio ya jumuiya ya Afrika Mashariki

Mwenyekiti mpya Rais Kagame amesema kwamba jumuiya itaweza kupima mafanikio yake kwa namna ambayo watu, bidhaa na mitaji yao itakavyoweza kuingia katika nchi hizi na jinsi watakavyo weza kupata mafanikio kutokana na ushirikiano huo. kwa kusisitiza anasema: “Hili ni jukumu letu. Najua sote tuko sawa katika hili, iwapo tutaelekeza nguvu zetu zote ili kulifanisha hili.” Aidha Rais Kagame amekazia kusema kwamba, jumuiya isikubali kurudishwa nyuma katika hatua ya ushirikiano ambayo nchi zimekubaliana kwa maslahi ya pamoja, ikiwemo biashara, miundombinu, viwanda na usalama. “Hatuwezi kuruhusu kurudi nyuma hasa wakati EAC imeanza kupiga hatua nzuri, ni juu yetu kuhakikisha Jumuiya inafanya kazi ipasavyo”.

Hatua za maendeleo ya Afrika Mashariki

Rais Kagame kama mwenyekiti mpya wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki amesema kwamba, Afrika inapiga hatua kwa kuungana zaidi, kama ilivyo kwa Jumuiya za Kiuchumi za maeneo mengine, ambayo ni muhimu kwa kujenga umoja unaounganisha bara la Afrika:“Mkutano huu wa marais umekuja wakati mwafaka sana ambapo tunatarajia kuadhimisha miaka 20 tangu kufufuliwa upya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kuna mengi ya kusheherekea, lakini pia ni wakati wa kutafakari juu ya thamani na umuhimu wa Jumuiya hii ambayo ni muhimu kwetu sote”.

Historia ya Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC)

Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) ni muundo wa kisiasa unaounganisha nchi sita za kanda ya Maziwa Makuu ya Afrika Mashariki: Burundi, Kenya, Rwanda, Sudan Kusini, Tanzania na Uganda. Jumuiya yenye jina hilo imepatikana mara mbili katika historia, kwanza ilikuwa ni ya jumuia ya nchi tatu kubwa zaidi kati ya hizo iliyo anzishwa mwaka 1967, lakini ikasambaratika mwaka 1977. Jumuiya ya Afrika ya Mashariki iliweza kufufuliwa kunako tarehe 7 Julai 2000. Nchi tano za Afrika ya Mashariki zilizokuwa chini ya utawala wa Uingereza na Ubelgiji zilianza uhuru wao kwa kuendeleza ushirikiano wa karibu uliorithiwa kutokana na utawala wa pamoja wakati wa ukoloni. Baada ya kupata uhuru mwaka 1961 nchi tatu ziliunda Mamlaka ya Huduma za Pamoja za Afrika ya Mashariki (EACSO). Ushirikiano ulihusu fedha (East African Shilling), forodha (Customs Union), huduma za reli (East African Railway), ndege (East African Airways), mabandari, posta na simu na elimu ya juu (Chuo Kikuu cha Afrika ya Mashariki chenye kampasi Makerere, Dar es Salaam na Nairobi). Mkataba ulilenga pia mahakama kuu ya pamoja na sera ya kiuchumi ya soko la pamoja. Haya yote yalitakiwa kuwa chini ya Bunge la Afrika ya Mashariki.

Tangu 1965 umoja huo ulianza kurudi nyuma wakati nchi zilipoanzisha pesa yake.

Mwaka 1967 nchi tatu zilijaribu upya kuimarisha umoja wao kwa Mkataba wa Ushirikiano wa Afrika ya Mashariki wakiita umoja wao “Jumuiya ya Afrika ya Mashariki” ikiwa na makao makuu Arusha, Tanzania. Lakini mielekeo ya nchi zote tatu zilitofautiana sana kama vile nchini Kenya iliendelea kwa njia ya upebari lakini Tanzania ilijaribu kujenga Ujamaa, kuanzia mwaka 1967. Na nchini Uganda ikaingia katika kipindi cha udikteta mkali wa Idi Amini aliyeharibu uhusiano na majirani alipoanza kudai sehemu za maeneo yao. Sababu nyingine ni madai ya Kenya ya kuwa na viti zaidi kuliko Uganda na Tanzania katika kamati za maamuzi, huku kukiwa na kutokuelewana kulikosababishwa na udikteta wa Idi Amin nchini Uganda, ujamaa huko Tanzania, na soko huria nchini Kenya, hivyo wanachama hawa watatu wakapoteza ushirikiano wa miaka zaidi ya sitini na manufaa ya ukubwa wa jumuiya hii kiuchumi. Kila mmoja wa wanachama hawa ilimbidi kuanza kutoa huduma na kujenga viwanda ambavyo hapo awali vilikuwa chini ya Jumuiya ya Afrika Mashariki. Kunako mwaka 1977 Jumuiya ya Afrika Mashariki ilikoma kufanya kazi yoyote na 1983 ilifutwa rasmi. Mali iliyobaki iligawanywa kati ya nchi zote tatu.

Kenya, Tanzania na Uganda zina historia ya ushirikiano tangu mwanzoni mwa karne ya 20, wakati wa ukoloni, ikiwa ni pamoja na Umoja wa Forodha baina ya Kenya na Uganda mwaka 1917, Tanganyika ilijiunga mnamo mwaka 1927, katika Ubalozi wa Afrika Mashariki (1948-1961), 'East African Common Services Organisation' (1961-1967) na Jumuiya ya Afrika Mashariki (1967-1977). Jumuia ambayo ilianzishwa baada ya uhuru ilidumu miaka 10 tu, lakini ilifufuliwa kwa mkataba wa tarehe 30 Novemba 1999, ulioanza kufanya kazi tarehe 7 Julai 2000, miaka 23 baada ya kifo cha ile ya kwanza. Burundi na Rwanda, ambazo ziliwahi kuwa koloni moja na Tanzania bara kabla ya Vita vikuu vya kwanza, zilijiunga na Mtangamano tarehe 6 Julai 2009. Mara baada ya kupata uhuru mwaka 2011, Sudan Kusini iliomba kujiunga na Jumuia, lakini haikukubalika hadi Machi 2016 kutokana na hali ya vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

Hatua za kuanzisha Shirikisho la Afrika Mashariki

Hatua kubwa ya awali katika kuanzisha Shirikisho la Afrika Mashariki ni muungano wa forodha katika mataifa husika uliotiwa saini mnamo Machi 2004 na ulioanza kutumika tarehe 1 Januari mwaka 2005. Chini ya masharti ya mkataba, Kenya, ambayo ndiyo nchi inayopata mauzo bora zaidi nje ya nchi katika kanda ya Afrika Mashariki, iliendelea kulipa ushuru kwa bidhaa zake zinazoingia nchi nyingine wanachama hadi mwaka 2010, kwa kiwango kilichopungua na wakati. Mfumo sawa wa ushuru utatumika kwa bidhaa kutoka nchi ambazo si wanachama.

Mambo muhimu ya kutambua katika umoja huu

Mahakama ya Afrika Mashariki: Mahakama ya Afrika Mashariki ndiyo mahakama inayosimamia kesi zote katika eneo hilo. Kwa sasa imo mjini Arusha, Tanzania. Bunge la Afrika Mashariki: Bunge la Afrika Mashariki ndicho kitengo cha kutengeneza sheria katika eneo la Afrika Mashariki. Ina wajumbe 27 ambao wote wamechaguliwa na mabunge ya nchi wanachama. Linahusika na masuala yote ambayo yanahusu Jumuiya hii kama vile kujadili bajeti ya Jumuiya ya Afrika Mashariki na masuala yote ya Jumuiya na kutoa mapendekezo kwa Baraza juu ya mambo wanayoyadhani muhimu kwa utekelezaji wa mkataba, kushirikiana pamoja na Bunge husika na kuanzisha kamati kwa makusudi kama vile wanavyodhani ni muhimu. Tangu uzinduzi wake mwaka 2001, bodi hii imekuwa na vikao kadhaa mjini Arusha, Kampala na Nairobi.

Pasipoti ya Afrika Mashariki:Pasipoti ya Afrika Mashariki ilizinduliwa rasmi tarehe 1 Aprili 1999 ili kurahisisha usafiri na kuvuka mipaka ya nchi husika. Ni halali kwa kusafiri ndani ya eneo la Afrika Mashariki (Kenya,Uganda na Tanzania) na kutoa haki ya kuingia na kukaa kwa miezi sita katika nchi yoyote na kisha unaweza ukaitumia tena. Pasipoti hii inapatikana katika Makao Makuu ya Idara ya Uhamiaji katika miji ya Nairobi, Kampala na Dar es Salaam. Ni raia tu wa Afrika Mashariki wanaoweza kuomba pasipoti hii. Ingawa pasipoti hii ni halali tu ndani ya Afrika Mashariki, majadiliano yalifanywa ili kuwa na hati sawa za kusafiri kwa watu wote wa Afrika Mashariki.

Hali ya mazingira

Sudan Kusini, Uganda, Rwanda na Burundi hazina pwani baharini, lakini zina mvua za kutosha. Huku inapatikana minne kati ya milima mirefu zaidi barani Afrika: Mlima Kilimanjaro (Tanzania), Mlima Kenya (Kenya), milima ya Rwenzori (Uganda/DRC) na Mlima Meru (Tanzania). Ziwa Turkana, Kenya, ndiyo ziwa la jangwani kubwa na lenye maji ya chumvi nyingi kuliko yote duniani. Ziwa Victoria linaunganisha nchi za Kenya, Uganda na Tanzania na ni la pili duniani kwa eneo. Ziwa Tanganyika mashariki kwa Tanzania ni la pili duniani kwa kina. Kenya pekee ina jangwa, jangwa la Chalbi katika Kaunti ya Marsabit.

Lugha katika Jumuiya ya Afrika Mashariki

Lugha kubwa zaidi katika Mtangamano ni Kiswahili, ambacho kutoka pwani ya Kenya na Tanzania kimeenea kwa namna moja au nyingine katika nchi zote sita na nje yake pia. Lugha rasmi ni Kiingereza pia. Lugha nyingine muhimu ni kama vile Kirundi na Kinyarwanda, ingawa Kifaransa kimeenea pia. Jumla ya wakazi wote ilikuwa 173,583,000 mnamo Julai 2016. Katika Mtangamano, hasa nchini Tanzania, zinapatikana jamii zote za makabila ya Afrika kusini kwa Sahara: Khoisan, Wakushi (Lugha za Kikushi ni kati ya lugha za Kiafrika-Kiasia. Zinatumika hasa katika Pembe la Afrika na nchi za jirani, kuanzia Misri hadi Tanzania.), Wabantu,(Wanailoti. Asilimia ya wakazi wanaoishi mijini ni 20 tu, lakini wanaongekeza kwa 4.71% kila mwaka.

Dini katika Jumuiya ya Afrika Mashariki

Upande wa dini, (Dini inamaanisha jumla ya imani ya binadamu kadhaa pamoja na mafundisho wanayotoa kuhusu yale ambayo wanayazingatia ama kuyasadiki, yaani mambo ya roho, kama vile kuhusiana na Mungu, maisha na uumbaji) unaongoza Ukristo kwa asilimia 76.04%, ikifuatwa na Uislamu kwa asilimia 14.06% na dini asilia za Kiafrika kwa asilimia 3.9%(Dini asilia za Kiafrika ni kati ya dini za jadi ambazo zinadumu hata leo, ingawa wafuasi wake wanapungua mwaka hadi mwaka kulingana na dini zilizotokea Mashariki ya Kati, hasa Ukristo na Uislamu, ambazo zinazidi kuenea barani Afrika), Kati ya Wakristo, Wakatoliki wanaongoza nchini Burundi na Sudan Kusini, wakati huo Waprotestanti wanaongoza nchini Kenya, huku aina hizo mbili zikilingana Tanzania, Uganda na Rwanda ( Uprotestanti ni aina ya Ukristo iliyotokana na Kanisa Katoliki huko Ulaya Kaskazini katika karne XVI kufuatana na mvutano wa kidini na kisiasa ambao ni maarufu kwa jina la upyaisho wa Kiprotestanti na waanzilishi wake ni Martin Luther na Yohane Kalvini).


Maoni


Ingia utoe maoni