Jumatano. 04 Desemba. 2024
feature-top
Papa Francisko aanza hija ya kitume nchi ya Umoja wa Falme za Kiarabu kwa kubeba moyoni mwake, mateso na mahangaiko ya watoto nchini Yemen.

Baba Mtakatifu Francisko, amewaombea watoto ambao wanateseka na kufa kwa baa la njaa na kiu ya kutisha; watoto wanaofariki mikononi mwa mama zao pasi na huduma bora ya afya; hawa ni watoto wanaonyemelewa na kifo wakati wowote ule! Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuwakumbuka watoto hawa katika sala zao!

Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana, kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican, Jumapili tarehe 3 Februari 2019, ameyaelekeza mawazo yake nchini Yeme ambako watu wanateseka kutokana na vita, njaa, magonjwa na umaskini wa hali na kipato. Kilio cha watoto na wazazi wao, kinamfikia Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kutoa mwaliko kwa viongozi wanaohusika pamoja na Jumuiya ya Kimataifa katika ujumla wake, kusimama kidete, ili kutekeleza mikataba ya kimataifa iliyotiwa sahihi pamoja na kuhakikisha kwamba, wananchi wanagawiwa chakula pamoja na kuendelea kujikita katika kutafuta na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Baba Mtakatifu katika sala iliyoungwa mkono na waamini waliokuwa kwenye Uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro, wamewaombea watoto ambao wanateseka na kufa kwa baa la njaa na kiu ya kutisha; watoto wanaofariki mikononi mwa mama zao pasi na huduma bora ya afya; hawa ni watoto wanaonyemelewa na kifo wakati wowote ule! Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuwakumbuka katika sala watoto hawa!

Baba Mtakatifu ameungana pia na Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI kuadhimisha Siku ya 41 ya Maisha Kitaifa. Amewatakia heri na baraka wananchi wanaotoka Mashariki ya Mbali, ambao hapo tarehe 5 Februari, wataadhimisha Mwaka Mpya. Amewataka kumwilisha tunu msingi, ili kudumisha amani inayopaswa kutafutwa, kulindwa na kudumishwa na wote.

Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwajulisha waamini kwamba, Jumapili tarehe 3-5 Februari 2019 anafanya hija ya kitume kwenye nchi ya Umoja wa Falme za Kiarabu. Amewaomba waamini na watu wote wenye mapenzi mema kumsindikiza kwa sala katika hija hii fupi, lakini muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa. Baba Mtakatifu, Jumamosi, tarehe 2 Februari 2019 alikwenda kusali kwenye Kanisa kuu la Bikira Maria mkuu, ili kujikabidhi chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Afya ya Warumi wakati huu wa hija yake ya kitume.


Maoni


Ingia utoe maoni