Jumatano. 04 Desemba. 2024
feature-top
Papa Francisko "achonga" na waandishi wa habari wakati akirejea kutoka Panama!

Papa Francisko amegusia mambo yafuatayo: mateso na mahangaiko ya watu baada ya kutoa mimba; yale yaliyomgusa katika maadhimisho ya Siku ya Vijana; tendo la ndoa kwa wanandoa ni jambo takatifu; sababu za vijana wengi kutoshiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa; uwezekano wa Mapadre Wakatoliki kuruhusiwa kuoa; huruma ya Mungu ni kwa ajili ya wote! Venezia?

Baba Mtakatifu Francisko, wakati akirejea kutoka kwenye maadhimisho ya Siku ya XXXIV Vijana Duniani kwa Mwaka 2019, nchini Panama, Jumapili tarehe 27 Januari 2019 amepata nafasi ya “kuchonga” na wanahabari waliokuwa kwenye msafara wake kwa muda wa dakika 50. Itakumbukwa kwamba, kulikuwa na waandishi wa habari 2, 500 kutoka sehemu mbali mbali za dunia waliohakikisha kwamba, ujumbe wa Baba Mtakatifu unawafikia vijana wengi zaidi.

Katika mahojiano magumu na yenye mitego ya kimaadili, Baba Mtakatifu Francisko aliweza kugusia mambo makuu yafuatayo: mateso na mahangaiko ya watu baada ya kutoa mimba; yale yaliyomgusa katika maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani huko Panama; tendo la ndoa kwa wanandoa ni jambo takatifu; sababu za vijana wengi kutoshiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa; uwezekano wa Mapadre Wakatoliki kuruhusiwa kuoa; huruma ya Mungu ni kwa ajili ya watu wote; shida na mahangaiko ya familia ya Mungu nchini Venezuela; nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo pamoja na changamoto ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani!

Mateso ya wanawake waliotoa mimba na jitihada za kutaka kujipatanisha tena na watoto ambao wamewatupa kwenye shimo la taka ni makubwa miongoni mwa wanawake wanaotaka tena kujipatanisha na Mwenyezi Mungu, ili waendelee kuwa imara katika imani, matumaini na mapendo! Baba Mtakatifu anasema, huu ni uzoefu ambao ameupata kutoka kwenye Mahakama ya huruma ya Mungu, yaani “Kiti cha Maungano” wakati anapotoa Sakramenti ya Upatanisho. Utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro ni kuwamarisha ndugu zake katika imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.

Wanawake waliotoa mimba wanapaswa kusaidiwa katika kiti cha maungamo, ili kutambua hali yao, tayari kujipatanisha na Mungu. Ni kutokana na huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake, wanaotambua dhambi zao na wako tayari kukimbilia tena huruma ya Mungu, Baba Mtakatifu Francisko wakati wa kufunga Mwaka Mtakatifu wa huruma ya Mungu, akatoa ruhusa kwa Mapadre wenye haki ya kuungamisha kuwaondolea dhambi hata wale wanawake waliotoa mimba. Wanawake waliotoa mimba wasaidiwe kujipatanisha na Mungu pamoja na watoto wao.

Kuna watoto ambao wanateseka kwa sababu wazazi wao wamefariki dunia wakiwa njiani kuwatafutia usalama, hifadhi na maisha bora zaidi. Huu ni utume unaogusa akili, moyo na mikono ya watu, ili kuweza kufikiri, kuamua na kutenda kikamilifu. Baba Mtakatifu anasema, katika maisha na utume wake, yote haya anayafanyia kazi na wakati mwingine, anapitiwa na usingizi na kujikuta akiwa amesinzia mbele ya Altare! Mateso na mahangaiko ya watu yanagusa akili, nyoyo na jinsi ya kutenda kadiri ya mapenzi ya Mungu.

Kuhusu Elimu ya Jinsia, Baba Mtakatifu anasema, vijana wanapaswa kufundishwa kuhusu tendo la ndoa kama zawadi kubwa inayodhihirisha upendo wa dhati na kwamba, hii ni kwa ajili ya kushiriki na kuendeleza mpango wa Mungu katika kazi ya uumbaji na wala si kwa ajili ya kujifurahisha na kutafuta fedha! Tendo la ndoa ni takatifu linapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa na kamwe lisitumiwe na baadhi ya nchi na Mashirika ya Kimataifa kutaka “kuwakoroga watu” kwa ukoloni wa kiitikadi kama inavyojionesha kwa sasa.

Elimu na malezi kuhusu tendo la ndoa, yawasaidie watu kukua, kukomaa na kuwajibika barabara. Wazazi na walezi wanapaswa kuwa wadau wa kwanza katika kuwaelimisha watoto wao maana na umuhimu wa tendo la ndoa. Lakini kwa bahati mbaya, wazazi wengi wameacha dhamana hii kwa shule kufanya zinavyotaka na matokeo yake ni kumong’onyoka kwa maadili na utu wema, kiasi cha kuwafanya vijana wengi kujisikia watupu kimaadili!

Vijana wa kizazi kipya kushindwa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa, Baba Mtakatifu anasema, kuna sababu nyingi lakini zaidi ni vijana kushindwa kuona na kupata ushuhuda wenye mvuto na mashiko kutoka kwa wachungaji wao. Viongozi wa Kanisa wanapaswa kuwa kati pamoja na vijana, ili kuwaonesha dira na mwongozo wa maisha, ili kamwe wasijisikie kuwa ni watoto yatima! Ushuhuda unaofumbatwa katika maneno na matendo; katika haki na ukweli unapaswa pia kutolewa na waamini wote na wala si wakleri peke yao.

Kwa sababu takwimu zinaonesha kwamba, Wakristo hao hao wanaokwenda Kanisani kila jumapili, ndio wa kwanza hata kushiriki katika matendo yanayodhalilisha utu na heshima ya binadamu; yanayosigina haki msingi na uhuru wa watu wengine! Matendo yote haya yanawafanya vijana wengi kushindwa kushiriki kikamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Kumbe, changamoto kwa Wakristo ni kuhakikisha kwamba, wanakuwa kweli ni mfano bora wa kuigwa kwa maneno na matendo yao na kamwe wasikubali kumezwa na malimwengu. Pale waamini wanapoanguka na kutumbukia dhambini, wawe na ujasiri wa kusimama tena kwa neema na huruma ya Mungu, tayari kusonga mbele! Kanisa linawahitaji waamini ambao ni mashuhuda wa ukweli, haki na upendo na wala si watu wanafiki!

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 huko Panama, ni tukio ambalo limewakutanisha vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Hii ni sehemu ya mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji kwa ajili ya vijana. Ni ukweli usiofumbaiwa macho kwamba, mavuno ni mengi lakini watenda kazi katika shamba la Bwana ni wachache! Baba Mtakatifu anasema hata katika mazingira na changamoto kama hii, Kanisa Katoliki litaendelea kuenzi Sheria ya Kanisa kuhusu Useja kama zawadi na sadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Anasema, kabla ya kubadili sheria hii na kuifanya kuwa ni uamuzi wa mtu binafsi, ni afadhali atangulie mbele ya haki.

Ikumbukwe kwamba, maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi yanajenga na kuliimarisha Kanisa. Sakramenti ya Daraja Takatifu inampatia Padre dhamana ya: kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu “Munera: munus regendi, munus docendi & munus sanctificandi. Haya ni mambo ambayo wale wote wanaodai kwamba, Mapadre waruhusiwe kuoa wanapaswa kuyatafakari kwa kina. Katika historia ya Kanisa, wakati wa utawala wa Kikomunisti, kuna baadhi ya wakulima, walifundishwa kidogo na hatimaye, wakapewa Daraja Takatifu ya Upadre, lakini, wakulima hawa walikuwa wanateseka sana! Uhuru wa kidini uliporeshwa tena, Kanisa likaendelea na Mapokeo yake.

Haya ni mambo ambayo watu wanapaswa kuyatafakari na hatimaye, kusali ili kumwomba Bwana wa mavuno aweze kupeleka watenda kazi wema, watakatifu na wachapa kazi katika shamba lake. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, alitoa ruhusa kwa Waanglikani waliokuwa wameoa kujiunga na Kanisa Katoliki na kuendelea kuishi na familia zao: Haya yanapatikana katika Waraka wake wa kitume “Anglicanorum coetibus”. Ni Mapadre kama wale wa Makanisa ya Mashariki ambao wanaruhusiwa kuoa kabla ya kupewa Daraja ya Ushemasi. Mapadre waseja bado ni hazina kubwa kwa Kanisa, licha ya mapungufu yao ya kibinadamu!

Baba Mtakatifu Francisko anasema, anafuatilia kwa umakini mkubwa, hali tete ambayo watu wa Mungu nchini Venezuela wanaipitia wakati huu katika historia ya nchi yao. Ushauri wa kichungaji ni kuwataka wadau wote wanaohusika kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kadiri ya uwezo wao kutafuta suluhu ya amani. Ni changamoto ya kuondokana na matumizi ya nguvu, kiasi cha kumwaga damu ya watu wasiokuwa na hatia. Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa wanaoweza kutatua mgogoro huu, wajibidishe haraka iwezekanavyo. Kuna haja ya misingi ya haki, amani na maridhiano kuanza kuzamisha mizizi yake huko Amerika ya Kusini, baada ya mateso makali huko Colombia pamoja na vitendo vya kigaidi vilivyoibuka hivi karibuni!

Mkutano wa Viongozi wa Kanisa utakaofanyika mwezi Februari kuhusu dhamana ya kuwalinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia kwa kuwaundia mazingira bora zaidi ya malezi na makuzi yao, anasema Baba Mtakatifu ni changamoto iliyotolewa Baraza la Makardinali Washauri. Lengo ni kutoa katekesi kwa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia, ili Maaskofu waweze kutambua madhara ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo. Watu walionyanyaswa kijinsia wanakabiliana na hali ngumu sana katika maisha yao: kiroho na kiutu.

Jambo la pili, ni kuwasaidia Maaskofu kuchukua hatua makini mintarafu Sheria, Kanuni na Taratibu za Kanisa. Mkutano maalum wa viongozi wa Kanisa kwa ajili ya kuwalinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia utafanyika mjini Vatican kuanzia tarehe 21-24 Februari 2019. Kitakuwa ni kipindi cha sala, tafakari pamoja na kusikiliza ushuhuda, ili kutambua uzito wa kashfa hii katika maisha na utume wa Kanisa. Itakuwa ni nafasi ya kufanya toba, wongofu wa kichungaji na kuomba msamaha, tayari kuanza upya, ili kujikita katika mchakato wa utakatifu wa maisha. Baba Mtakatifu anakaza kusema, watu wasiwe na matarajio makubwa kwani kashfa kama hizi ni sehemu ya udhaifu wa binadamu unaoendelea kufanyika kwenye familia na jamii katika ujumla wake! Jambo la msingi kwa Mama Kanisa ni kuwa na protokali ya utekelezaji wa ulinzi kwa watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia!

Wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji ni changamoto changamani anasema Baba Mtakatifu Francisko inayopaswa kushughulikiwa kwa ari na moyo mkuu, kwa kutambua kwamba, mataifa mengi yanaundwa na wakimbizi pamoja na wahamiaji. Jambo la msingi ni watu kuwa na kumbu kumbu endelevu ya historia ya nchi zao, ili viongozi wa Serikali waweze kufanya maamuzi kwa hekima na busara zaidi. Hii inatokana na ukweli kwamba, suluhu ya wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji inafumbatwa kwa namna ya pekee katika fadhila ya upendo na ukarimu kama unavyoshuhudiwa na nchi kama: Italia, Uturuki na Ugiriki.

Jambo la pili ni kuziwezesha kiuchumi zile nchi ambazo zinazalisha wakimbizi na wahamiaji wengi, ili ziweze kujenga mazingira bora zaidi kwa watu wake. Mataifa na makampuni makubwa ya kimataifa yanaendelea kukwapua utajiri wa Bara la Afrika ambao ungeweza kutumika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu Barani Afrika. Lebanon imeonesha mfano bora zaidi wa kuigwa katika kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji huko Mashariki ya Kati. Hili ni tatizo changamani linalopaswa kuzungumzwa katika ukweli na uwazi bila ya kuwa na maamuzi mbele.

Baba Mtakatifu amehitimisha kipindi cha maswali na majibu kwa kukiri kwamba, kwa kweli anajisikia kupyaishwa zaidi baada ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani. Nchini Panama, amekutana na watu wa kawaida, wanaojivunia utajiri wa watoto wao ambao kimsingi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu; matumaini yao kwa siku za usoni! Idadi ya watoto wanaozaliwa Barani Ulaya inaendelea kupungua mwaka hadi mwaka. Kumbe, jambo la kujiuliza kwa wananchi wa Ulaya, wanaona fahari kwa kitu gani? Utalii? Mapumziko? Jumba la fahari? Mbwa? Au Mtoto aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu.

Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba zake kufunga maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani huko Panama,  amewataka vijana kuhakikisha kwamba, wanatekeleza kwa dhati leo ya Mungu katika uhalisia wa maisha yao. Utamaduni na sanaaa ya watu kukutana pamoja na kuwasikiliza vijana ni amana na urithi mkubwa wa Kanisa kutoka kwa Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana iliyohitimishwa hivi karibuni. Baba Mtakatifu Francisko anasema, mapungufu ya kibinadamu miongoni mwa vijana waliokuwa wanajitolea huko Panama, hayakuwa ni kikwazo kikubwa cha kushindwa kutoa huduma, bali wameonesha ujasiri wa hali ya juu, changamoto kwa sasa ni kuhakikisha kwamba, wanajitahidi kurekebisha vilema na mapungufu yao kwa mwanga wa upendo na huruma ya Mungu, tayari kushiriki katika maisha na utume wa Kanisa. Huduma kwa waathirika wa UKIMWI ni ushuhuda wa Injili ya upendo!


Maoni


Ingia utoe maoni