Jumapili. 24 Novemba. 2024
feature-top
Papa Francisko awataka wakleri, watawa na waamini walei kupyaisha maisha na utume wao kwa Kristo Yesu

Kuna wakati maisha yanakuwa ni mzigo mzito usioweza kubebeka. Matokeo yake, watu wanatumbukia katika msongo wa mawazo na katika hali ya kukata tamaa! Kumbe, kuna haja ya kutafuta kisima cha maji ya wokovu ili kuzima kiu na mchoko wa hija ya maisha! Papa anasema, huu ni mchoko wa matumaini kutokana na wingi wa kazi na utume kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake.

Kazi ya ukarabati wa Kanisa kuu la “Santa Maria la Antigua” Jimbo kuu la Panama, imechukua takribani miaka saba. Baba Mtakatifu Francisko wakati wa maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani kwa mwaka 2019 huko Panama, Jumamosi tarehe 26 Januari 2019, ametabaruku Altare ya Kanisa kuu, tayari sasa kuanza kutumika kwa ajili ya maadhimisho ya mafumbo ya Kanisa. Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashukuru wale wote waliojisadaka ili kufanikisha ukarabati huu na kwamba, sasa familia ya Mungu Jimbo kuu la Panama ina nyumba ya kuadhimishia Ibada ya Misa Takatifu.

Ibada hii ya Misa ilikuwa ni maalum kwa ajili ya wakleri, watawa na waamini walei kutoka Jimbo kuu la Panama. Kumbe, hata mahubiri ya Baba Mtakatifu yaliwalenga watu hawa zaidi kwa kufanya rejea katika Injili ya Yohane inayomwonesha Kristo Yesu akikutana na Mwanamke Msamaria kwenye Kisima cha Yakobo na kumwomba maji ili kuzima kiu yake, baada ya kutembea mwendo mrefu. Yesu aliomba maji ya kunywa ili kupata tena nguvu ya kusonga mbele na utume wake wa kuwatangazia watu Habari Njema ya Wokovu!

Yesu alikuwa anawahubiria maskini Habari Njema, wafungwa kufunguliwa kwao, kuwaacha huru waliosetwa na hatimaye, kutangaza mwaka wa Bwana uliokubaliwa. Matukio yote haya anasema Baba Mtakatifu yanafyonza sana nguvu. Ni matukio ambayo yalishuhudiwa na Mitume wake, kiasi kwamba, ubinadamu ukaweza kukutana na Neno la uzima. Yesu alikuwa amechoka na safari na katika dhana hii ya “mchoko”, watu wa Mungu katika ujumla wao, wanaweza kupata pia utambulisho wao. Hivi ndivyo ilivyo hata kwa wakleri, watawa na waamini walei katika vyama na mashirika yao ya kitume.

Hawa ni watu ambao wanatumia muda mrefu kwa ajili ya kazi, kiasi hata cha kukosa muda wa chakula, mapumziko, kukaa pamoja na familia au hata kukosa kabisa muda wa kusali. Katika mwelekeo huu, maisha yanakuwa ni mzigo mzito usioweza kubebeka. Matokeo yake, watu wengi wanatumbukia katika msongo wa mawazo na katika hali ya kukata tamaa! Katika hali na mazingira kama haya, kuna haja ya kutafuta kisima cha maji ili kuzima kiu na mchoko wa hija ya maisha! Baba Mtakatifu anasema, huu ni mchoko wa matumaini kutokana na wingi wa kazi na utume kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Mwisho wa siku, watu wawe na ujasiri wa kutabasamu na kusonga mbele kwa imani na matumaini!

Mchoko wa kukatisha tamaa ni kikwazo kinachomzuia mwamini kuona mbele kutokana na changamoto za ulimwengu mamboleo, majadiliano, ukweli wa maisha pamoja na changamoto changamani zinazowakumba wakleri na watawa katika maisha na utume wa Kanisa. Dunia inabadilika kwa kasi kubwa, kiasi hata cha kukosa muda wa kufanya tafakari ya kina. Lakini, mchoko wa matumaini ni changamoto inayoibuliwa na Mama Kanisa kama sehemu ya mbinu mkakati wa kupambana na madonda ya dhambi za watoto wake, kwa kutambua kwamba, kama Mama alishindwa kusikiliza kilio cha Kristo Yesu, alipokuwa akilia na kusema, “Mungu wangu, mbona umeniacha?”

Baba Mtakatifu Francisko anasema, huu ndio mwelekeo wa mchoko sahihi unaowataka watu wa Mungu kujiaminisha mbele ya Mungu, wakati wanakabiliana na hali tete na zenye mashaka kwa maisha na utume wao kwa siku za mbeleni! Pale ambapo Jumuiya za Wakleri zinakosa imani na matumaini kiasi cha kuona kwamba, hata Kristo Yesu hana tena jipya la kuwaambia wala kuwapatia! Katika mazingira kama haya watu wanashindwa kuwa ni nuru ya ulimwengu na chumvi ya dunia, matokeo yake ni kutoa mwelekeo tenge wa maisha!

Baba Mtakatifu anawataka watu wa Mungu kuzima kiu ya maisha na utume wao kutoka kwa Kristo Yesu, chemchemi ya maji yanayobubujikia uzima wa milele, ili hatimaye, waweze kumwabudu Mwenyezi Mungu katika roho na kweli. Huu ndio upya wa maisha. Katika mazingira na hali ya kukata tamaa, watu wa Mungu wathubutu kurejea tena katika kisima che upendo ule wa kwanza, Yesu alipowaona, akawaita na kuwatuma kwenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu.

Watu waguswe na upendo wa Kristo katika ngazi ya mtu binafsi, lakini zaidi kama jumuiya. Wajitahidi kurejea tena na kuanza kujikita katika uaminifu wa karama unaofumbatwa katika kipaji cha ubunifu; kwa kuwaheshimu, kuwapenda na kuwajali jirani, ambao kimsingi ni watakatifu walioko pembeni mwao. Ni katika mwelekeo huu, Kanisa limebahatika kuwa na mifano ya wakleri, watawa na waamini walei waliojisadaka kujenga na kuimarisha misingi ya jumuiya zao kwa kujikita katika matumaini na utu!

Kuzima kiu maana yake ni kuanza mchakato wa kujitakasa, kukumbatia amana na utajiri wa karama za mashirika ya kitawa na kazi za kitume, tayari kusoma alama za nyakati ili kuzimwilisha katika maisha na utume wa Kanisa. Watu wa Mungu watambue kwamba, wao ni wahitaji na kwamba, wanapaswa kukutana na Mwenyezi Mungu anayewawezesha kuishi kikamilifu bila wasi wasi wala makunyanzi, daima kwa kujitahidi kusoma alama za nyakati. Baba Mtakatifu anakaza kusema, mchoko wa matumaini unaweza kutakaswa na kuwa ni kikolezo cha kurejea tena katika upendo ule wa asili, ili kuambata mambo msingi katika maisha. Kristo Yesu anaendelea kuwatafuta, kuwaangalia, kuwapenda na kuwatuma kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kutabarukiwa kwa Kanisa iwe ni chachu ya kupyaisha matumaini, kugundua uzuri uliopita, ili kuweza kuudumisha kwa siku za usoni.


Maoni


Ingia utoe maoni