Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 huko Panama, Ijumaa, tarehe 25 Januari 2019 alipata nafasi ya kuadhimisha Ibada ya Kitubio kwenye Gereza la Watoto Watukutu huko Garzas de Pacora. Gereza hili lilizinduliwa kunako mwaka 2012 na lina uwezo wa kutoa hifadhi kwa wafungwa na mahabusu 200. Watoto wafungwa wanapokuwa gerezani humo wanapata nafasi ya kusoma na kujifunza stadi za maisha sanjari na maendeleo fungamani ya binadamu!
Baba Mtakatifu amewaungamisha vijana 12 na katika mahubiri yake amekazia kwa namna ya pekee mambo makuu mawili: umuhimu wa kuondokana na manung’uniko kama walivyoonesha Mafarisayo na waandishi kwa kumshutumu Kristo Yesu kwamba, alikuwa anakawaribisha na kula na wenye dhambi. Pili ni kujikita katika toba na wongofu wa ndani, tayari kuanza kutembea katika mwanga wa furaha ya Injili kama ilivyokuwa kwa Mwana mpotevu! Mafarasayo na waandishi walikwazwa na kukereka sana kutokana na tabia ya Yesu kushirikiana na wadhambi.
Baba Mtakatifu anasema, watu wote ni wadhambi na wametindikiwa neema, hivyo wanapaswa kumkaribisha Kristo Yesu katika maisha yao, kwa toba na wongofu wa ndani kama walivyofanya watoza ushuru pamoja na kuzungumza naye. Vinginevyo, baadhi ya watu wanaweza kujiona kuwa na haki na watakatifu zaidi kiasi hata cha kumfungia Kristo Yesu malango ya maisha yao. Kwa waamini wanaothubutu kumfungulia Yesu malango ya nyoyo zao na kumkaribisha anawakirimia uwezo wa kuangalia mbali mbali zaidi na kuonja upendo wake usiokuwa na mipaka.
Hata leo hii, bado kuna watu wanaonung’unika na “kupika majungu” na kusahau kwamba, jicho la huruma na upendo wa Mungu linawaelekea zaidi wadhambi, wanaohitaji kuonjeshwa: wema, ukarimu na upendo. Kwa bahati mbaya, kuna watu ambao ni mafundi sana wa kuwagawa jirani zao katika makundi ya wema na wabaya; wadhambi na watakatifu, tabia ambayo haimpendezi Kristo Yesu hata kidogo. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kuwa makini ili kamwe wasitumbukie katika tabia ya kutaka kuwabeza wengine kutokana na mapungufu yao ya kibinadamu.
Tabia kama hii inawachafulia watu: majina, utu na heshima yao na hatimaye, kujenga ukuta wa watu wanaonung’unika kwa kudhani kwamba, huu ndio mtindo wa maisha. Hawa ni watu wasiomkubali Kristo Yesu katika maisha yao na daima ndio wale wanaokwenda kinyume cha mafundisho yake, kwa kudhani kwamba, wao eti ni wenye haki, wateule wa Mungu. Ni kutokana na mwelekeo huu potofu, jamii inaweza kujikuta ikitumbukia katika tabia ya kuwatenga maskini na kuwasukumizia pembezoni mwa jamii, kiasi hata cha kushindwa kuwajibika. Hivi ndivyo ilivyokuwa katika unabii wa Kayafa, Kuhani mkuu wa wakati ule kwamba, “Yafaa mtu mmoja afe kwa ajili ya wengi”, ili watu waweze kuondokana na kile kilichodaiwa kuwa ni “kero kutoka kwa Kristo Yesu”.
Jambo la kusikitisha ni kuona kwamba, waathirika wakuu katika mitazamo hii tenge ya kijamii ni maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Wanaendelea kugandamizwa, kiasi hata cha kushindwa kusimama tena na kuendelea na safari ya maisha. Baba Mtakatifu anawaalika waamini kutubu na kumwongokea Mungu anayewaangalia kwa jicho la huruma na mapendo, daima yulo tayari kuwapokea na kuwakumbatia wale wote wanaomwendea kwa moyo wa toba na majuto kamili, ili kuwashirikisha furaha ya maisha mapya kama ilivyokuwa kwa Mwana mpotevu. Waamini watambue kwamba, wanaye Baba mwenye huruma, anayewapenda na kuwathamini watoto wake. Anayetaka kuwajengea mazingira yatakayowasaidia kupambana na hali zao, tayari kutembea katika mwanga wa maisha mapya, kwa kukua na kukomaa katika kufanya maamuzi ya maisha.
Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, upendo wa Yesu unampatia mwamini fursa mpya ya maisha, tayari kumwingiza katika maisha ya jumuiya ya waamini baada ya kujitenga kutokana na dhambi. Ni upendo fungamani unaowawezesha waamini kukita maisha yao katika mchakato wa mageuzi kama ilivyokuwa kwa Mathayo mtoza ushuru, aliyeacha yote na kuamua kumfuasa Kristo kwa toba na wongofu wa ndani, kiasi hata cha kuwafanyia rafiki zake sherehe kubwa.
Kwa kuandamana na Kristo Yesu, waamini wanajengewa uwezo wa ndani wa kufanya mageuzi makubwa katika maisha yao! Jambo la msingi ni kujitambua kwamba, wao ni wadhambi. Hata Mitume wa Yesu walikuwa ni wadhambi wakubwa, mmoja wao akamsaliti kwa vipande thelathini vya fedha, Petro akamkana mara tatu na wengine, wakakimbia na kumwacha akiteseka, akahukumiwa na hatimaye, akafa Msalabani. Ikumbukwe kwamba, Mitume wa Yesu ni watu walioteuliwa mmoja mmoja!
Mitume wa Yesu, baada ya kutubu na kuongoka, wakawa ni chachu ya mageuzi ulimwenguni. Hawa wamejifunza kutoka kwa Yesu mwenyewe, anayewaita tena na tena ili kuwaimarisha, leo hii wamekuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa. Furaha na matumaini ya Kikristo yanajikita katika moyo wa mwamini ambaye ameonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yake, kama ilivyokuwa kwa Mwana mpotevu! Hapa hakuna sababu ya kukata wala kujikatia tamaa, daima Mwenyezi Mungu anapenda kuwaokoa waja wake, ili kuwashirikisha furaha ya maisha ya uzima wa milele.
Baba Mtakatifu anapenda kuwatia shime, vijana watukutu wanaotumikia adhabu yao magerezani, kukumbuka kwamba, wao ni sehemu ya familia! Wanayo mengi ya kuweza kuwashirikisha hata vijana wenzao katika mchakato wa toba na wongofu wa ndani, ili kuweza kufurahia matokeo ya mabadiliko katika maisha. Jamii itakuwa na kasoro kubwa, ikiwa kama itashindwa kufanya sherehe kutokana na wongofu wa watoto wake. Jamii ina shida kubwa ikiwa kama daima itaendelea kuogelea katika manung’uniko, kwa kuwalaani watu na hata wakati mwingine, kwa kutoguswa na mahangaiko yao.
Jumuiya inapaswa kujifunza kutoa nafasi ya toba na wongofu wa ndani; kwa kupambana kufa na kupona ili kujenga mazingira yatakayowawezesha vijana kuwa na matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi, kwa kupata fursa ya elimu na kazi. Watu wote wanapaswa kuwajibika ili kuhakikisha kwamba, Jumuiya inaunda mazingira bora kwa watu wake, kuweza kurejea na kushiriki katika maisha. Hii ni changamoto ya ujasiri kwa watu wote.
Baba Mtakatifu mwishoni mwa mahubiri yake, amewakumbusha vijana hawa kwamba, mwanadamu ana tabia ya kuangalia mambo ya nje, lakini Mwenyezi Mungu anachunguza yale yaliyofichika kwenye sakafu ya moyo wa mwanadamu. Anawakirimia waja wake nguvu ya kuweza kufanya mageuzi katika maisha yao, tayari kusherehekea zawadi ya wokovu kwa kuwa na mwelekeo mpana zaidi katika maisha, kama ilivyokuwa kwa Mwana mpotevu katika Injili ya Luka.
Maoni
Ingia utoe maoni