Jumapili. 24 Novemba. 2024
feature-top
Papa Francisko asema, Njia ya Msalaba inaendelea kushuhudiwa katika mateso na mahangaiko ya watu wengi duniani!

Njia ya Msalaba, kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu; ni safari ya mateso na upweke inayoendelea ktika maisha ya mwanadamu katika ulimwengu mamboleo, kwa kuwabeza maskini na wanyonge, kiasi cha kutoguswa na mateso pamoja na mahangaiko yao. Hata wakati mwingine kwa waamini, imekuwa ni vigumu kwao kuwatambua ndugu zao wanaoteseka.

Baba Mtakatifu Francisko baada ya kuongoza Ibada ya Kitubio kwenye Gereza la Watoto Watukutu huko Garzas de Pacora, Ijumaa jioni, tarehe 25 Januari 2019, aliongoza Ibada ya Njia ya Msalaba kwenye eneo la Cinta Costera, na kuhudhuriwa na bahari ya vijana kutoka ndani na nje ya Panama. Kufuata nyayo za Yesu katika Njia ya Msalaba ni tukio la neema linalowawezesha waamini kupyaisha na hatimaye kuimwilisha na kuizamisha katika undani wa maisha yao, kwa kutambua nguvu ya Neno la Mungu.

Baba Mtakatifu anasema, ni hatari sana kufuata Njia ya Msalaba kwa sababu maneno na matendo ya Kristo Yesu yanasigana na kupingana na malimwengu. Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia, tabia na utamaduni wa kutoguswa na mahangaiko ya wengine na ukosefu wa upendo na mshikamano wa dhati vinatawala. Njia ya Msalaba ni chemchemi ya matumaini na mapendo. Hii ni njia ambayo Kristo Yesu na Bikira Maria waliipitia na Mama Kanisa anaiendeleza kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji.

Baba Mtakatifu katika tafakari yake baada ya Njia ya Msalaba, anaendelea kufafanua kwa kusema, Njia ya Msalaba ni kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa binadamu; ni safari ya mateso na upweke inayoendelea katika maisha ya mwanadamu katika ulimwengu mamboleo, kwa kuwabeza maskini na wanyonge, kiasi cha kutoguswa na mateso pamoja na mahangaiko yao. Hata wakati mwingine kwa waamini, imekuwa ni vigumu kwao kuwatambua ndugu zao wanaoteseka, kiasi cha kuwageuzia kisogo na kutaka kumezwa na makelele na hatimaye, kufumba mdomo, ili kutokupiga kelele.

Kishawishi kikubwa ni kujenga na kudumisha urafiki katika ushindi, mafanikio na utukufu.Ni rahisi sana kukaa karibu na watu maarufu na mashuhuri; wale wanaodhaniwa kuwa ni washindi wa ulimwengu huu. Lakini bado kuna kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo, uonevu pamoja na vitisho. Lakini, Kristo Yesu pale Msalabani alijifananisha na wale wote wanaoteseka, watu wanaojisikia kusahauliwa, kubezwa na kusukumizwa pembezoni mwa jamii, kiasi cha kuwakumbatia wote, kwa kuwapatia faraja na baraka.

Kwa Njia ya Msalaba, Kristo Yesu anajiunga na kila kijana na kila hali ya maisha, ili kuleta upya na ufufuko wa maisha. Leo hii Njia ya Msalaba inaendelezwa katika utamaduni wa kifo unaokumbatiwa na sera za utoaji mimba; kwa watoto kukosa familia, elimu na mahali pa kuchezea. Kuna wanawake na wasichana wanao ambulia vipigo, nyanyaso na dhuluma; watu wanaotumbukizwa katika mifumo ya utumwa mamboleo, uhalifu wa magenge kitaifa na kimataifa mambo yanayo dhalilisha utu na heshima ya bindamu.

Njia ya Msalaba inaendelezwa kwa vijana wasiokuwa na fursa ya kazi, wanaolazimika “kula pensheni” kabla ya wakati; vijana wanaotumbukizwa katika biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya! Badala ya upendo na mshikamano wa dhati, wakimbizi na wahamiaji wanatelekezwa, wanakataliwa, wanaachwa wateseke kwa njaa, magonjwa na utupu, kwa kisingizio kwamba, wao ni chanzo cha majanga yanayowakabili wananchi katika nchi wahisani. Ni Njia ya Msalaba inayoendelezwa kwa wazee na wagonjwa; wazawa wanaong’olewa kutoka katika ardhi yao, kiasi cha kukosa matumaini ya leo na kesho iliyo bora zaidi.

Mateso ya Kristo yanaendelea kujionesha katika uchafuzi wa mazingira nyumba ya wote. Baba Mtakatifu anasema, katika changamoto zote hizi za: Umaskini, magonjwa, wakimbizi na wahamiaji, waamini na watu wote wenye mapenzi mema wanapaswa kuonesha ujasiri na ukarimu kama ule wa Simoni wa Kirene kwa kuwa: vyombo vya amani, wajenzi wa madaraja ya mshikamano wa upendo na udugu! Baba Mtakatifu amewauliza vijana, ikiwa kama wanao ujasiri wa kusimama chini ya Msalaba kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria! Mama ambaye alithubutu kumsindikiza Mwanaye wa pekee katika Njia ya Msalaba, akamwangalia kwa jicho la upendo na wala hakupigishwa magoti na makali ya uchungu yaliyopenyeza moyoni mwake.

Leo hii, kuna Misalaba ya Wakristo wengi kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Kwa mfano wa Bikira Maria, wazazi na walezi wawe na ujasiri wa kuwasindikiza watoto wao wanapopita katika mateso na mahangaiko makubwa! Wazazi wajifunze kutengeneza mazingira mazuri yanayopambwa kwa tunu msingi za maisha ya kifamilia sanjari na kuunga mkono wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kuwalinda na kuwatetea watoto dhidi ya nyanyaso. Kwa mfano wa Bikira Maria, Kanisa lijifunze kujenga na kudumisha utamaduni wa kupokea, kulinda, kuendeleza na kushirikisha, kwa kuwaheshimu na kuwathamini wakimbizi na wahamiaji.

Kwa njia ya Bikira Maria, Kanisa liendelee kujikita katika Ibada, kwa kuwaheshimu na kuwapenda watu wote. Kanisa liwe ni kumbu kumbu endelevu inayoheshimu na kuthamini wazee, kwa kuwapatia nafasi katika maisha na utume wa Kanisa. Kwa mfano wa Bikira Maria, Kanisa lijifunze kuwa chini ya Misalaba, kwa kuwafungulia vijana macho na nyoyo zao; kwa kuwaondolea woga na hali ya kukata tamaa. Vijana wajifunze kukaa pamoja na Kristo Yesu, Bikira Maria na watakatifu wote! Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kuwapatia vijana baraka ya Msalaba, amewataka vijana kurejea kwenye makazi yao kwa hali ya ukimya na amani ya ndani na furaha ya kutaka kuendelea kumfuasa Kristo Yesu katika Njia ya Msalaba! Yesu mwenyewe awaongoze katika maisha yao na Bikira Maria walinde na kuwatunza!


Maoni


Ingia utoe maoni