Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani ni tukio la furaha na matumaini kwa Kanisa na jamii katika ujumla wake, ni fursa ya ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Uwepo wa Khalifa wa Mtakatifu Petro katika matukio kama haya unapania pamoja na mambo mengine, kuadhimisha na kupyaisha imani na matumaini, tayari kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia Injili ya Kristo. Hili ni tukio la kupyaisha ujana wa Kanisa kwa kumsikiliza Roho Mtakatifu, kama ilivyokuwa wakati wa Pentekoste ile ya kwanza! Hii ni huduma inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha.
Kwa maneno haya, Baba Mtakatifu Alhamisi, tarehe 24 Januari 2019 amezindua rasmi maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani huko kwenye Uwanda wa Cinta Costera, Panama. Amewashukuru vijana wote waliojisadaka tangu mwanzo wa maadhimisho haya kutoka sehemu mbali mbali za Amerika ya Kusini. Hija inayowawezeaha vijana kutembea kwa pamoja ni kielelezo cha ufuasi na utume wa Kristo; watu wanaothubutu. Hawa ni vijana wanaotoka katika mila, desturi, tamaduni na lugha mbali mbali, lakini wote wanaunganishwa na imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake.
Vijana wanapongezwa kwa kuchakarika bila ya kujibakiza katika mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana, kwa kutambua na kuthamini tofauti zao msingi; kwa kuheshimiana na kuthaminiana. Vijana wawe na ujasiri wa kukataa kishawishi cha watu wanaotaka kuwagawa na kuwatenganisha kwa sababu yoyote ile! Upendo wa dhati ni nyenzo muhimu sana inayowaunganisha watu kama alivyokaza kusema Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI aliyekuwa anafuatilia tukio hili akiwa mjini Vatican. Vijana wamemtumia salam na matashi mema.
Vijana wasikubali kushawishiwa na Shetani, anayependa kuona watu wakitwangana ngumi, wakigawanyika na kusambaratika; watu wanaomezwa kwa hofu na mashaka na badala yake, wawe ni watu wanaojifunza kushirikiana, kushikamana na kufanya kazi kwa pamoja, tayari kubomoa kuta za utengano zinazojengwa na wanasiasa duniani. Vijana wawe ni wajenzi na vyombo vya amani na utamaduni wa watu kukutana na kusaidiana kwa hali na mali, kwani utamaduni wa kukutana ni wito mtakatifu. Tofauti zao msingi ni amana na utajiri unaopaswa kulindwa na kudumishwa!
Vijana wawe ni mashuhuda wa Injili ya matumaini inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Wawe ni mashuhuda wa Injili ya upendo kwa Mungu na jirani. Ikumbukwe kwamba, Ukristo si mkusanyiko wa kweli ambazo watu wanapaswa kuzisadiki; Sheria, kanuni na taratibu za kufuatwa. Ukristo ni dini ya Kristo Yesu aliyewapenda watu wake upeo, kiasi hata cha kujisadaka Msalabani kwa ajili ya kuwakomboa watu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Vijana watambue kwamba, upendo wa Kristo unawawajibisha; unawaunganisha; unawainua juu kama mlingoti wa bendera. Huu ni upendo unaowaweka wote huru, unaowaganga na kuwaponya. Ni upendo unaowapatanisha na Mungu pamoja na jirani zao; ni upendo unaowachangamotisha kujisadaka katika huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Huu ndio upendo unaolipa katika maisha na utume wa vijana, unaojisadaka katika huduma.
Baba Mtakatifu anasema, Bikira Maria ni kielelezo cha upendo wa dhati kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Alikubali kutekeleza mpango wa Mungu katika maisha yake, akakubali kuwa ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili. Vijana wanahamasishwa na Mama Kanisa kuhakikisha kwamba, wanakuwa na ujasiri wa kukubali na kutekeleza mpango wa Mungu katika maisha yao. Siku ya Vijana Duniani iwe ni chemchemi ya matumaini, sala na ushuhuda unaomwilishwa na vijana wenyewe katika utakatifu wa maisha, ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Baba Mtakatifu anawataka vijana kumwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kuwafunda, kuwakumbusha yale wanayojifunza na hatimaye, kuyatekeleza katika matendo.
Vijana wamwombe Roho Mtakatifu fadhila ya upendo, ili waweze kupenda kwa moyo wote, wawe raia wema na waamini watakatifu! Mwishoni, Baba Mtakatifu amewashukuru vijana kwa kukubali na kuitikia wito wa kushiriki katika maadhimisho haya. Amelishukuru Baraza la Maaskofu Katoliki Panama kwa kufanikisha maandalizi na hatuimaye, maadhimisho haya, kiasi kwamba, Panama imekuwa ni daraja linaloendelea kumwilisha ndoto ya Mungu kwa binadamu.
Maoni
Ingia utoe maoni