Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya kuzungumza na viongozi wa Serikali, wanadiplomasia pamoja na viongozi wa kiraia nchini Panama, Alhamisi, tarehe 24 Januari 2019 alipata nafasi ya kuzungumza na Sekretarieti ya Mabaraza ya Maaskofu Katoliki, Amerika ya Kati, SEDAC. Baba Mtakatifu katika hotuba yake amekazia mambo yafuatayo: Kanisa kutambua na kushuruku; Umuhimu wa kukuza chachu ya upendo wa watu wa Mungu; kuliishi Fumbo la Umwilisho, yaani “Kenosis” ya Kristo Yesu: kwa moyo na roho miongoni mwa vijana. Unyenyekevu wa Maaskofu ushuhudiwe katika Daraja Takatifu na kati ya maskini.
Baba Mtakatifu anasema, uwepo wake kati yao ni kutaka kuwakumbatia watu wote wa Mungu huko Amerika ya Kati; katika imani na matumaini yao; matatizo na changamoto wanazokabiliana nazo, ili hatimaye, Kanisa liweze kuwajengea tena matumaini na upendo kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu kamwe hawezi kusinzia, anaona na hatimaye, atawasaidia kwa wakati muafaka. SEDAC ni chombo cha mawasiliano Amerika ya Kati. Ni jukwaa la kushirikishana: mang’amuzi, vipaumbele na utekelezaji wake kama sehemu ya mchakato wa kupyaisha na kuyatajirisha Makanisa mahalia. Huu ndio mwelekeo mpya wa maisha na utume wa Kanisa unaofumbatwa kwa kufikiri na kuwa na mwelekeo mpana zaidi; kwa kusikiliza, kuelewa na kushiriki kikamilifu, ili kutoa nafasi kwa Roho Mtakatifu ili aweze kuliongoza Kanisa lake
SEDAC katika kipindi cha miaka 75 ya uwepo wake, imekuwa ni mahali pa kushirikishana furaha na machungu; ndoto na mahangaiko ya watu wa Amerika ya Kati. Kuna wakleri, watawa na waamini walei ambao wamejisadaka bila ya kujibakiza ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Ni watu ambao wamekuwa ni sauti ya kinabii, wakasimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu dhidi ya ukosefu wa haki, umaskini na matumizi mabaya ya madaraka.
Ni kwa njia ya ushuhuda wa utakatifu wa maisha yao, wamekuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa matendo ya huruma. Kati yao ni Mtakatifu Oscar Arnulfo Romero Galdamez, aliyefikiri na kutenda pamoja na Kanisa, kiasi kwamba, maisha yake yalisheheni uaminifu hata katika kile kipindi tete cha dhuluma na nyanyaso dhidi ya Kanisa. Huu ni mwaliko kwa viongozi wa Kanisa kuendelea kujisadaka kila siku kwa ajili ya huduma kwa vijana wa kizazi kipya katika utakatifu na ushuhuda wa kinabii, sehemu muhimu sana ya vinasaba vya Makanisa mahalia, Amerika ya Kati.
Umuhimu wa Kanisa: Kufikiri, kutambua, kushukuru na kulipenda Kanisa kama chemchemi ya imani, chachu ya toba na wongofu wa ndani, unaomwezesha mwamini kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kushuhudia imani kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Kifodini anasema Baba Mtakatifu kinamwezesha mwamini kumwilisha ndani mwake moyo wa shukrani kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Oscar Arnulfo Romero Galdamez. Baba Mtakatifu anakazia umuhimu wa kukuza chachu ya upendo wa watu wa Mungu, ili kuwajenga na kuwaimarisha, tayari kumkiri katika imani na kumhudumia katika utakatifu wa maisha kama njia ya kupata wokovu. Maaskofu wanapaswa kumsikiliza Roho Mtakatifu pamoja na watu wa Mungu; kutafakari Neno la Mungu na kulimwilisha katika sera na vipaumbele vya shughuli za kichungaji, tayari kugundua utashi wa Mungu na kuutekeleza.
Kristo Yesu anaendelea kuishi ndani ya Kanisa lake, kumbe, Kanisa linapaswa kujikita katika fadhila ya unyenyekevu. Liwe tayari kukumbatia ufukara, ili kuondokana na kishawishi cha Kanisa kutaka kujitenga na watu pamoja na kujitosheleza lenyewe! Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu kuliishi Fumbo la Umwilisho, yaani “Kenosis” ya Kristo Yesu ambaye ni njia, ukweli na uzima. Hiki ni kielelezo cha Mwenyezi Mungu anayeokoa na anayetaka kukutana pia na watu wake. Maaskofu wathubutu kugusa madonda na mahangaiko ya watu wao, ili kuibua mbinu na mpango mkakati utakaojibu kilio cha chao.
Ni mwaliko wa kubainisha vipaumbele katika maisha na utume wa Kanisa. Maaskofu watenge rasilimali fedha na watu, ili kutekeleza mpango huo, ili kuwapatia watu maana na matumaini ya maisha yanayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu ambaye anapaswa kuwa ni msingi wa mahusiano na mafungamano yao! Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, “Kenosis” ya Kristo Yesu iwawezeshe Maaskofu kukutana na kuwa karibu zaidi na vijana, ili kusoma alama za nyakati, tayari kupyaisha ulimwengu kwa tunu msingi za Kiinjili. Vijana ni dira na mwongozo wa maisha ya Kanisa, mwaliko na changamoto ya kuwasikiliza kwa makini.
Kanisa ni Mama na Mwalimu, anapaswa kuwasaidia vijana kukuza na kudumisha uhuru kwa njia ya elimu makini, ili kuwajengea uwezo wa kupambana na hali pamoja na mazingira yao. Vijana wawe ni ngazi ya kumwendea Kristo Yesu kwa njia ya huduma makini! Kwa bahati mbaya, vijana wanakibiliwa na matatizo pamoja na changamoto mbali mbali za maisha. Ni watu wasiokuwa na fursa za ajira, wasichana wanakabiliwa na vipigo vya majumbani; biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya, mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo pamoja na nyanyaso dhidi ya watoto wadogo. Hali mbaya ya uchumi pamoja na sera zisizotoa kipaumbele cha kwanza kwa utu na mahitaji msingi ya binadamu. Kuna vijana ambao wamekuwa yatima na wala hawana makazi ya kuishi. Kanisa halina budi kusimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu.
Kanisa liendelee kupambana na kumong’onyoka kwa tunu msingi za maisha na tamaduni pamoja na kuenea kwa majangwa ya maisha ya kiroho yanayoendelea kusababisha umaskini na kudhohofisha nguvu ya kupambana na mambo yanayokwenda kinyume cha utu na heshima ya binadamu! Wongofu wa ndani, mshikamano, elimu makini pamoja na kuguswa na mahangaiko ya watu ni kati ya changamoto zinazopaswa kuvaliwa njuga na Mama Kanisa kwa wakati huu. Baba Mtakatifu anakaza kusema, Kenosis” ya Kristo Yesu imwilishwe katika fadhila ya unyenyekevu unaofumbatwa katika Daraja Takatifu, kwa Maaskofu kuendelea kujifunza kuwa watu, mapadre na wachungaji wa roho za watu. Maaskofu wasadake maisha na muda wao kwa ajili ya huduma kwa watu wa Mungu. Wawe ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu na kwamba, maisha katika huduma ya Daraja takatifu si lele mama wala maji kwa glasi!
Maaskofu wakuze sanaa na utamaduni wa kusikiliza kwa makini; kutangaza na kushuhudia Injili kwa harufu ya utakatifu wa maisha. Maaskofu wawe ni viongozi bora, tayari kukabiliana na changamoto za maisha kwa ujasiri na moyo mkuu. Maaskofu watoe kipaumbele cha kwanza kwa Mapadre ambao ni wasaidizi wao wa kwanza katika kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Furaha ya Maaskofu iwe ni katika kuona watoto wao wanakua na kuzaa matunda bora!
Baba Mtakatifu anahitimisha hotuba yake kwa Maaskofu wa SEDAC kwa kusema, “Kenosis” ya Kristo Yesu imwilishwe katika huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kwa kutambua kwamba, ufukara wa Kanisa ni nguzo ya kulilinda Kanisa lenyewe dhidi ya ubinafsi na hatimaye, kumezwa na malimwengu. Nguvu ya Kanisa ishuhudiwe katika huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.
Maoni
Ingia utoe maoni