Jumatano. 04 Desemba. 2024
feature-top
Vijana wafurahia uwepo wa Baba Mtakatifu Francisko kati yao, wasahau hata utamu wa chakula walichoandaliwa.

Vijana waliopata chakula cha mchana pamoja na Baba Mtakatifu Francisko wanasema, chakula halikuwa ni jambo la muhimu kwao, bali ile nafasi ya kukutana, kukaa na kuzungumza na Papa, imewaachia faraja katika maisha na utume wao! Sasa wako tayari kuwa ni mashuhuda wa Injili ya huruma, upendo na mshikamano; wajenzi wa madaraja ya kuwakutanisha watu!

Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, tarehe 26 Januari 2019 amepata chakula cha mchana pamoja na vijana 10 kutoka mataifa mbali mbali kwenye Seminari kuu ya San Josè Jimbo kuu la Panama kama sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2019. Askofu mkuu José Domingo Ulloa Mendieta wa Jimbo kuu la Panama ameshikiri pia katika mlo huu. Baada ya chakula cha mchana, Baba Mtakatifu alijitenga na vijana hawa na kwenda kusali kwa faragha kwenye Kikanisa Seminarini hapo.

Baba Mtakatifu pia amepata nafasi ya kusalimiana na majandokasisi wanaoendelea na malezi pamoja na majiundo yao ya kikasisi seminarini hapo. Amewatia moyo kusonga mbele kwa imani na matumaini, daima wakitamani kumhudumia Kristo Yesu na Kanisa lake! Vijana waliopata chakula cha mchana pamoja na Baba Mtakatifu Francisko wanasema, chakula halikuwa ni jambo la muhimu kwao, bali ile nafasi ya kukutana, kukaa na kuzungumza na Baba Mtakatifu, imewaachia faraja kubwa katika maisha na utume wao! Kwa sasa wako tayari kuwa ni mashuhuda wa Injili ya huruma, upendo na mshikamano; wajenzi wa madaraja ya kuwakutanisha watu katika medani mbali mbali za maisha.

Vijana hawa wanasema, kwa hakika Baba Mtakatifu Francisko ni kiongozi wa watu na mnyenyekevu sana, anayeendelea kuwakumbusha watu wa Mungu kwamba, Mungu ni upendo na watu wanapaswa kupendana, kuheshimiana na kuthaminiana. Papa Francisko ni kiongozi anayeguswa na mahangaiko ya watu wa Mungu na anaonesha upendeleo wa pekee katika maisha na utume wa vijana ambao kwake wana thamani kubwa sana. Vijana hawa wanakabiliwa na changamoto na matatizo mbali mbali, lakini pia wanazo fursa ambazo wanaweza kuzitumia ili kukuza na kudumisha utu na heshima ya binadamu.

Baba Mtakatifu anaguswa na matatatizo ya wengi na wala si tu vijana, kwani amekuwa ni mtetezi mkuu wa wakimbizi na wahamiaji; maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Ameendelea kusimama kidete kupinga rushwa na ufisadi wa mali ya umma unaowatumbukiza watu wengi katika majanga ya maisha! Ni kiongozi anayetaka kutangaza na kushuhudia Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo pamoja na sera za ukoloni wa kiitikadi.

Papa Francisko ni kiongozi anayeitaka Jumuiya ya Kimataifa kulinda na kudumisha haki msingi, utu na heshima ya binadamu. Ni kiongozi ambaye amekuwa mstari wa mbele katika harakati za utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote pamoja na amani duniani. Huyu ndiye Papa Francisko anavyoeleweka na vijana waliobahatika kupata chakula pamoja naye kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani. Ni kiongozi ambaye anaendelea kulihamasisha Kanisa kujenga na kudumisha sanaa na utamaduni wa kuwasikiliza vijana, tayari kuwasindikiza na kuwaongoza katika safari ya maisha yao. Baba Mtakatifu amepata nafasi ya kuzungumza na vijana hawa kila mmoja wao na kuonesha nia ya kutaka kutembelea nchi kama India, Visiwa vya Oceania, baadhi ya nchi za Asia kama vile Indonesia na Afrika.

Baba Mtakatifu anakiri kwamba, wakati mwingine, amepata taabu sana kujibu maswali ya vijana hawa ambao walikuwa na udadisi mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Anakumbusha kwamba, kusikiliza ni kipaji kinachopaswa kumwilishwa katika maisha na utume wa viongozi wa Kanisa, wazazi na walezi. Baba Mtakatifu anatambua na kuthamini mchango mkubwa unaotolewa na vijana wa kizazi kipya katika maisha na utume wa Kanisa.


Maoni


Ingia utoe maoni