Baba Mtakatifu Francisko anasema Askofu ni alama ya utimilifu wa Daraja Takatifu na zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu kwa ajili ya Kanisa lake. Askofu anapewa dhamana na mamlaka ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Ni dhamana inayofumbatwa katika unyenyekevu na upendo na kamwe Maaskofu wasijisikie kuwa ni wafalme bali watu walioteuliwa kwa ajili ya uongozi wa Kanisa. Maaskofu wanapaswa kuwa ni watu wema na wenye kiasi, wapenda haki na watakatifu; watu wenye mifano bora ya kuigwa. Maaskofu wanapaswa kuratibu maisha na utume wa Kanisa, daima wakimwachia nafasi Roho Mtakatifu ili aweze kuwaongoza na kuwasimamia katika kutekeleza dhamana na utume wao ndani ya Kanisa.
Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Jumamosi, tarehe 19 Januari 2018 amemweka wakfu Askofu mkuu Christophe Zakhia El Kassis aliyeteuliwa hivi karibuni kuwa Balozi wa Vatican nchini Pakistan. Katika mahubiri yake, Kardinali Parolin amekazia dhamana ya Roho Mtakatifu anayetakatifuza, anayeongoza, anayefariji na kuwaimaarisha waja wake kama ilivyokuwa wakati wa Sherehe ya Pentekoste, Roho Mtakatifu alipowashukia Mitume. Ni Roho Mtakatifu anayemwimarisha Askofu mkuu ili aweze kutekeleza dhamana na utume wake kwa ari na moyo mkuu kama sehemu ya utekelezaji wa kazi ya uokombozi iliyoanzishwa na Kristo Yesu.
Ni Roho Mtakatifu anayemwezesha Askofu mkuu kumwilisha tunu msingi za Kiinjili, ili kukata kiu ya matarajio, matumaini na udadisi wa watu wa Mungu, tayari kuwajenga na kuwaimarisha kama Kanisa la Kristo, kila mara wanapomwita! Licha ya ukosefu, udhaifu na mapungufu ya mwanadamu, lakini bado Mwenyezi Mungu kwa njia ya Roho Mtakatifu anakuja kuwasaidia waja wake wanaomkimbilia kwa: imani, matumaini na unyenyekevu mkuu! Roho Mtakatifu analitakatifuza Kanisa, analijalia neema inayobubujika kutoka katika Sakramenti na Mafumbo ya Kanisa, ili Kanisa liweze kuongozwa na upendo pamoja na wema, ili kuganga migawanyiko na kinzani zinazoweza kujitokeza katika maisha na utume wa Kanisa.
Askofu mkuu Christophe Zakhia El Kassis amewekwa wakfu ili kumwakilisha Khalifa wa Mtakatifu Petro kwenye Makanisa mahalia, daima akijitahidi kukuza na kudumisha umoja na Khalifa wa Mtakatifu Petro, akiwasilisha mawazo ya Papa kwa uaminifu mkubwa, ili waamini kwenye Makanisa mahalia waweze kuhisi uwepo wake wa kibaba. Askofu mkuu El Kassis anapaswa kuwa ni shuhuda wa imani, matumaini, haki na mapendo, licha ya mipasuko na misigano inayoendelea sehemu mbali mbali za dunia. Askofu mpya anapaswa kuonesha upendo wa dhati kwa Kristo na Kanisa lake, maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwa kutambua kwamba, daima Fumbo la Msalaba litakuwa mbele yake, chemchemi ya furaha na nguvu ya kusonga mbele katika utume na hatimaye kuzaa matunda kwa wakati wake!
Kardinali Parolin anakaza kusema, upendo ni fadhila kubwa kuliko zote kwani upendo: uuvumilia, hufadhili, hauhusudu, hautakabari, haujivuni, hautafuti mambo yake, hauoni uchungu, hauhesabu mabaya haufurahii udhalimu bali hufurahi pamoja na kweli. Upendo wa Kristo unawawezesha Maaskofu kuwa wema, wanyenyekevu na wachapa kazi katika shamba la Bwana. Askofu mkuu Christophe Zakhia El Kassis anatoka Lebanon nchi utajiri wa historia ya Maandiko Matakatifu.
Motto yake ya Kiaskofu ni “Scis Domine, quia, amo te! Yaani “Wewe Bwana wanajua jinsi ninavyokupenda! Mwenyezi Mungu anafahamu karama na udhaifu wake ndiyo maana anapaswa kujikabidhi mbele ya Mwenyezi Mungu ili aweze kumwongoza na kumlinda kwa tunza yake, ili kweli aweze kuwa ni shuhuda wa imani, matumaini na mapendo. Askofu mkuu Christophe El Kassis, sehemu kubwa ya utume wake, ameitekelezea katika nchi za Kiislam na sasa anatumwa kwensa Pakistan, changamoto ya kuonesha uwepo wa karibu wa Baba Mtakatifu kwa ndugu zake katika imani, kwa kuwatia shime, ili kukuza na kudumisha umoja na mshikamano wa Kanisa; pamoja na matumaini kwa kuheshimu dhamiri zao nyofu.
Askofu mkuu El Kassis anapaswa kuwa tayari kuwafafanulia watu kweli za Kiinjili, kwa kujikita katika diplomasia, sera na mikakati ya shughuli za kichungaji inayofumbatwa katika majadiliano ya kidini, ili wote waweze kukua na kukomaa katika imani, kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu, ili kwamba, tofauti zao msingi ziwe ni amana na utajiri wao. Awasaidie watu kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya kiroho, ili kujenga utamaduni wa ushirikiano na mshikamano; amani na utulivu; tayari kupambana na misimamo mikali ya kidini na kiimani; kumong’onyoka kwa tunu msingi za maisha kiakili, kimaadili na kiutu!
Askofu mkuu Christophe Zakhia El Kassis alizaliwa tarehe 24 Agosti 1968 huko Beirut, nchini Lebanon. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikuhani, tarehe 21 Mei 1994 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre na kuwa ni sehemu ya Kanisa la Wamoriniti wa Beirut. Alijiendeleza na hatimaye, kufaulu kutunukiwa shahada ya uzamivu katika Sheria na Taratibu za uendeshaji wa kesi mahakamani!
Wakati wa maadhimisho ya Jubilei kuu ya Miaka 2000 ya Ukristo, tarehe 19 Juni, akaanza utume wake katika masuala ya diplomasia ya Kanisa. Tangu wakati huo, akabahatika kutekeleza dhamana na utume wake kwenye Balozi za Vatican nchini Indonesia, Sudan, Uturuki na baadaye katika kitengo cha mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa mjini Vatican. Ni bingwa aliyebobea katika lugha ya: Kiarabu, Kifaransa, Kiitalia, Kiindonesia, Kihispania na Kijerumani, matendo makuu ya Mungu, zawadi ya Roho Mtakatifu kwa waja wake!
Maoni
Ingia utoe maoni