Jumatano. 04 Desemba. 2024
feature-top
Papa Francisko asikitishwa sana na vitendo vya kigaidi dhidi ya Wakristo huko Jimbo Katoliki la Jolo nchini Ufilippini.

Baba Mtakatifu amesikitishwa sana na vitendo vya kigaidi vilivyofanywa huko mjini Jolo, nchini Ufilippini, kwa kulipua mabomu mawili Kanisani, ambamo waamini walikuwa wanaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, Jumapili, tarehe 28 Januari 2019. Watu 20 wamepoteza maisha na wengine 110 wamejeruhiwa vibaya.

Jumuiya ya Kimataifa kila mwaka ifikapo tarehe 27 Januari, inawakumbuka wahanga wa utawala wa kinazi waliopoteza maisha yao wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Mauaji ya kimbari yaani “Shoa” yaliyofanywa na utawala wa kinazi ni changamoto ya kulinda na kuthamini utu wa kila mtu! Baba Mtakatifu Francisko mara baada ya Sala ya Malaika wa Bwana kwenye Kituo cha Msamaria Mwema cha Juan Diaz kwa ajili ya Wagonjwa wa Ukimwi, ameitaka Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inaendelea kuiweka hai historia iliyopita na majanga yaliyomwandama mwanadamu, ili kuwasaidia watu kujifunza kurasa chungu katika historia ya mwanadamu, ili kamwe wasithubutu tena kurejea na kutumbukia katika makosa ya zamani!

Baba Mtakatifu anaitaka Jumuiya ya Kimataifa kuendelea kujibidisha katika ujenzi wa misingi ya haki, ili kudumisha amani na maelewano pamoja na kujikita katika maendeleo fungamani kama chombo cha amani sanjari na ujenzi wa ulimwengu ulio bora zaidi. Baba Mtakatifu amewakumbuka na kuwaombea waathirika wa maafa yaliyotokea Ijumaa, tarehe 25 Januari 2019 huko nchini Brazil, baada ya Bwawa kubomoka na kusababisha mafuriko makubwa. Inasemekana kwamba, zaidi ya watu 58 wamepoteza maisha na wengine 305 hawajulikani mahali waliko. Baba Mtakatifu anawaombea wale wote walioguswa na kutikiswa na msiba huu mzito. Anapenda kuwahakikishia uwepo wake wa karibu kwa sala na sadaka yake!

Baba Mtakatifu ameikumbuka pia familia ya Mungu nchini Venezuela inayopitia katika kipindi kigumu cha maisha na historia yake. Kwa sasa kuna marais wawili wanaoongoza; watu wanaendelea kuuwawa kila kukicha. Baba Mtakatifu anaiombea Venezuela ili iweze kufikia suluhu ya amani na maridhiano kati ya watu; kwa kuheshimu na kudumisha haki msingi za binadamu; daima ustawi, mafao na maendeleo ya wengi vikipewa kipaumbele cha kwanza. Baba Mtakatifu amesikitishwa sana na vitendo vya kigaidi vilivyofanywa huko mjini Jolo, nchini Ufilippini, kwa kulipua mabomu mawili Kanisani, ambamo waamini walikuwa wanaadhimisha Ibada ya Misa Takatifu, Jumapili, tarehe 27 Januari 2019. Watu 20 wamepoteza maisha na wengine 110 wamejeruhiwa vibaya. Baba Mtakatifu anasikitika kusema, mauaji haya yanaendelea kusababisha majonzi makubwa katika Jumuiya za Wakristo.

Baba Mtakatifu amechukua fursa hii, kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea raha ya milele wale waliofariki dunia na majeruhi waweze kupona haraka na kurejea katika shughuli zao za kila siku. Baba Mtakatifu anamwomba Kristo Yesu, Mfalme wa amani aweze kuwaongoa magaidi hawa, ili hatimaye wananchi waweze kupata amani ya kweli na utulivu! Mwishoni, Papa Francisko ameonesha masikitiko makubwa, kutokana na vitendo vya kigaidi vilivyotokea hivi karibuni, kwenye Chuo cha Polisi Kitaifa huko, Bogota, nchini Colombia na kusababisha watu 21 kupoteza maisha yao na wengine 50 kujeruhiwa vibaya. Tukio hili la kigaidi limezua hofu na mashaka ya kuzuka tena kwa vitendo vya kigaidi vilivyositishwa kunako mwaka 2016. Baba Mtakatifu amewataja Askari wote hawa kwa majina yao! Ameombea amani iweze kudumishwa nchini Colombia.


Maoni


Ingia utoe maoni