Jumamosi. 23 Novemba. 2024
feature-top
Changamoto za Umoja wa Mataifa katika ulimwengu mamboleo!

Baba Mtakatifu Francisko anakazia umuhimu wa Kanisa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa familia ya Mungu nchini India. Anawaalika Maaskofu kukutana upya na Kristo Yesu katika hija ya maisha yao na kumpatia nafasi, ili aweze kupyaisha maisha na vipaumbele vyao, ili waendelee kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili.

Khalifa wa Mtakatifu Petro na kwa wakati huu ni Baba Mtakatifu Francisko anatumwa kutekeleza dhamana yake kama sehemu ya utii wa Kristo Yesu aliyemtaka Mtakatifu Petro kuwalisha kondoo wake! Ndiyo maana Vatican na Kanisa katika ujumla wake, linaguswa sana na uchungu, fadhaa na mahitaji ya familia ya binadamu: kiroho na kimwili, kwa kuendelea kuwa sikivu kwa mahangaiko yanayomsibu mwanadamu katika ulimwengu mamboleo! Ili kujenga na kudumisha umoja na mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa kuna haja ya kuondokana na utaifa usiokuwa na mashiko kwa ustawi, maendeleo na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa.

Umoja wa Mataifa unapaswa kuendeleza dhamana na wajibu wake, lakini kwanza unapaswa kufanyiwa mageuzi makubwa na kwamba, mshikamano wa dhati ni muhimu ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa inataka kucharuka katika maendeleo hasa kwa nchi maskini zaidi ulimwenguni. Kumbe, kuna haja ya kutenga rasilimali watu, fedha na vitu! Hii ni changamoto inayotolewa na Askofu mkuu Bernardito Auza Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa anayefanya rejea kwenye hotuba ya Baba Mtakatifu Francisko kwa Mabalozi na wawakilishi wa Mashirika ya Kimataifa mjini Vatican kwa mwaka 2019.

Anaendelea kufafanua kwamba, Umoja wa Mataifa umeshindwa kutekeleza dhamana na wajibu wake katika medani mbali mbali za kimataifa kutokana na utaifa usiokuwa na mvuto wala mashiko kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Matokeo yake ni kukwama kwa utekelezaji wa “Global Compact 2018” yaani “Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji 2018” unaopania pamoja na mambo mengine kukomesha ubaguzi na maamuzi mbele; kuongeza fursa za ushirikishwaji wa wahamiaji katika maisha ya nchi wahisani; kupunguza gharama za kuwahudumia wakimbizi na wahamiaji sehemu mbali mbali za dunia.

Kwa sasa kuna baadhi ya nchi kama Brazil zimeanza kujitoa na nyingine, nyingi zilikataa kuridhia mkataba huu kutokana na mivutano ya sera na siasa za kitaifa. Hayo ndiyo yanayojitokeza hata katika utekelezaji wa maazimio ya Mkutano 24 wa Mkataba wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi, COP24 Katowice, Poland, unaokazia umuhimu wa utekelezaji wa Makubaliano ya Paris kama kielelezo cha mshikamano wa Jumuiya ya Kimataifa katika kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote! Hizi zote ni changamoto zinazoukabili Umoja wa Mataifa. Askofu mkuu Bernardito Auza anakaza kusema, haya ndiyo yanayojitokeza hata kwenye Baraza kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa. Kuna baadhi ya nchi zinatumia kura la veto ili kulinda masilahi yao kitaifa kama ilivyo katika vita inayoendelea huko Mashariki ya Kati.

Mshikamano na mafungamano ya Jumuiya ya Kimataifa katika mchakato wa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi unaathiriwa kwa kiasi kikubwa na ukoloni wa kiitikadi kama unavyofafanuliwa na Baba Mtakatifu Francisko kama njia ya nchi changa zaidi duniani kupatiwa msaada. Matokeo yake ni kuendelea kusua sua kwa Malengo ya Maendeleo Endelevu Kimataifa ifikapo mwaka 2030. Baba Mtakatifu Francisko anautaka Umoja wa Mataifa kuwa ni jukwaa la kuwakutanisha wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa ili kupanga na kutekeleza sera na mikakati mbali mbali ya maendeleo inayozingatia utu, heshima, haki msingi za binadamu; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Umoja wa Mataifa hauna budi kuwa ni sauti ya maskini zaidi duniani, kati yao ni wakimbizi na wahamiaji; wazee na wagonjwa. Umoja wa Mataifa unapaswa kufanyiwa marekebisho makubwa kwa kusoma alama za nyakati ili kukidhi mahitaji ya Jumuiya ya Kimataifa kwa wakati huu, kuliko hata ilivyokuwa miaka 70 iliyopita. Lengo ni kupata ufumbuzi wa vita ambavyo vimesahaulika duniani, kudhibiti biashara na matumizi ya silaha za maangamizi duniani pamoja na kuwekeza katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Baba Mtakatifu Francisko amekuwa ni sauti ya wakimbizi na wahamiaji pamoja na familia ya Mungu huko Mashariki ya Kati ambako vita, dhuluma na nyanyaso zinaendelea! Kuna Mataifa makubwa yaliyowekeza huko na makampuni makubwa yanaendelea kutengeneza silaha na kuwauzia hao “wanaotwangana huko Mashariki ya Kati. Askofu mkuu Bernardito Auza anahitimisha mahojiano maalum na Vatican News kwa kusema kwamba, Vatican imeendelea kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi katika Jumuiya ya Kimataifa.

Maoni


Ingia utoe maoni