Fumbo la Umwilisho ni ushuhuda wa uwepo endelevu wa Mungu kati pamoja na watu wake! Baba Mtakatifu Francisko akiwa nchini Panama, Jumapili tarehe 27 Januari 2019 ametembelea Kituo cha Msamaria Mwema cha Juan Diaz kwa ajili ya Wagonjwa wa Ukimwi, kama kielelezo cha mchungaji mwema anayeguswa na mahangaiko ya watu wake! Kituo hiki kilianzishwa na Kanisa Katoliki nchini Panama kunako mwaka 2005 kwa ajili ya kuwahudumia waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi; kiuchumi, kisaikolojia na katika maisha ya kiroho. Takwimu zinaonesha kwamba, Panama ina waathirika wa Virusi vya Ukimwi wapatao 7, 000. Inakadiriwa kwamba, kati ya watu 25, 000 hadi 30, 000 wameambukizwa virusi vya ugonjwa wa Ukimwi.
Baba Mtakatifu ametumia fursa hii kuwashukuru wale wote wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kuwajengea tena matumaini ya maisha mapya, waathirika wa ugonjwa wa Ukimwi. Kituo hiki kimekuwa ni chemchemi ya imani na matumaini ya Kanisa yanayoendelea kupyaishwa kila kukicha kwa njia Injili ya upendo. Baba Mtakatifu anawaalika wadau katika kituo hiki kumwomba Roho Mtakatifu ili waweze kuwaona wagonjwa hawa kama jirani zao; watu wanaokutana nao kila siku, kiasi hata cha kugusa maisha yao. Hii ni changamoto ya kuwa ni Wasamaria wema, kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu, kwa kuguswa na mateso pamoja na mahangaiko ya jirani zao na kamwe wasiwageuzie kisogo!
Huduma kwa wagonjwa wa Ukimwi ni ushuhuda wa Mama Kanisa anayetekeleza utume wake wa kinabii kwa kuanzisha makazi na jumuiya ambamo huruma na upendo wa Mungu vinaweza kumwilishwa na kuwa ni sehemu ya Habari Njema ya Wokovu. Waamini wanahamasishwa kujenga na kudumisha mshikamano wa upendo na huduma kwa wagonjwa. Waendelee kujifunza kuvumilia na kusamehe, ili watu waendelee kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao.
Baada ya tafakari hii, Baba Mtakatifu amewaongoza wale wote waliokuwepo kwenye Kituo cha Msamaria Mwema cha Juan Diaz kwa ajili ya Wagonjwa wa Ukimwi kwa Sala ya Malaika wa Bwana, kwa kuwaweka chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, ili watu wote waweze kuonja umoja na upendo wa kidugu; utume ambao unawaunganisha wote. Wasi wasi, matamanio yao halali, uchungu na fadhaa pamoja na madonda wanayobeba ndani mwao, yote wayapeleke kwa Bikira Maria, ili aweze kuwasaidia na kuwambea kwa wema na upendo wake wake wa Kimama.
Maoni
Ingia utoe maoni