Mara baada ya maadhimisho ya Misa Takatifu ya kufunga rasmi maadhimisho ya Siku ya XXXIV Vijana Duniani kwa Mwaka 2019 huko Panama, Askofu mkuu José Domingo Ulloa Mendieta wa Jimbo kuu la Panama amemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kuwawezesha vijana kuonja amana na utajiri wa imani ambayo wamejitahidi kuiishi kwa furaha na matumaini makubwa, kiasi hata cha kuendelea kuwa na matumaini kwamba, iko siku ndoto za vijana hawa zitaweza kumwilishwa katika uhalisia wa maisha yao!
Vijana wamepata nafasi ya kugundua tena na tena Ibada kwa Bikira Maria na dhamana ya kuendelea kujisadaka kwa ajili ya ndugu na jirani zao na kwamba, kwa sasa wanahamasishwa kuitikia wito kutoka kwa Mwenyezi Mungu kama alivyofanya Bikira Maria. Maadhimisho haya yamejikita katika: Maisha ya sala, malezi na majiundo; upyaisho wa maisha kwa njia ya Sakramenti za Kanisa pamoja na wongofu wa shughuli za kichungaji. Kanisa nchini Panama limeimarishwa na kuhamasishwa kusonga mbele kwa ari na moyo mkuu katika umisionari na utume wake ili kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili! Huu ni mwanzo wa mpango mkakati wa uinjilishaji mpya Amerika ya Kusini, kwa kujikita katika matumaini na mapendo yaliyoshuhudiwa na vijana.
Kwa upande wake, Kardinali Kevin Joseph Farrell, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha anasema, maadhimisho haya ni sehemu ya mchakato wa Kanisa kutembea kwa pamoja kama ilivyokuwa wakati wa utangulizi na hatimaye, maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana. Imekuwa ni fursa kwa vijana kuishi kwa umoja, upendo na mshikamano wa imani kama mbinu ya kupambana na changamoto mamboleo sanjari na kujikita katika utekelezaji wa dhamana ya maisha na utume wao ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake.
Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani ni tukio ambalo limepyaisha maisha na utume wa Kanisa kwa kuona tena ufunuo wa Uso wa huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Kardinali Kevin Joseph Farrell ametangaza kwamba, maadhimisho ya Siku ya XXXV ya Vijana Duniani kwa Mwaka 2022 yatafanyika Jimbo kuu la Lisbon, nchini Ureno.
Maoni
Ingia utoe maoni