Baba Mtakatifu Francisko amepokea kwa masikitiko makubwa taarifa za msiba wa Kardinali Fernando Sebastian Aguilar, C.M.F. Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Pamplona na Tudela lililoko nchini Hispania, aliyefariki duniani tarehe 24 Januari 2019 akiwa na umri wa miaka 89 baada ya kushambuliwa hivi karibuni na ugonjwa wa Kiharusi. Baba Mtakatifu ameyasema hayo katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican kwenda kwa Askofu mkuu Francisco Pèrez Gonzàlez wa Jimbo kuu la Pamplona na Tudela. Baba Mtakatifu anaungana na wale wote walioguswa na msiba huu mzito, hasa: waamini, ndugu jamaa, wanashirika pamoja na wakleri aliofanya nao kazi kwa karibu sana enzi ya uhai wake katika majimbo mbali mbali nchini Hispania.
Baba Mtakatifu anamkumbuka kwa ustadi wake wa kufundisha na kama kiongozi wa Chuo Kikuu cha Kipapa cha Salamanca. Ni kiongozi wa Kanisa aliyejisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa Kanisa na Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania. Baba Mtakatifu anaiombea roho ya Marehemu Kardinali Fernando Sebastian Aguilar, C.M.F. raha ya milele na mwanga wa milele, ili aweze kupumzika kwa amani, miongoni mwa watakatifu wa Mungu. Itakumbukwa kwamba, Kardinali Fernando Sebastian Aguilar alizaliwa tarehe 14 Desemba 1929, Jimboni Tarazona. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi, tarehe 28 Juni 1953 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Mtakatifu Yohane Paulo II akamteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki Lèon hapo tarehe 22 Agosti 1979 na akawekwa wakfu hapo tarehe 29 Septemba 1979.
Tarehe 8 Aprili 1988 akateuliwa kuwa Askofu mkuu mwandamizi mwenye haki ya kurithi Jimbo kuu Granada na tarehe 26 Machi 1988 akasimikwa rasmi kuwa Askofu wa Jimbo kuu la Pamplona na Tudela. Ilikuwa ni tarehe 31 Julai 2007 alipong’atuka kutoka madarakani. Baba Mtakatifu Francisko kunako tarehe 22 Februari 2014 akamteuwa kuwa Kardinali. Marehemu Kardinali Fernando Sebastian Aguilar, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Pamplona na Tudela na amezikwa, Jumamosi, tarehe 26 Januari 2019.
Maoni
Ingia utoe maoni