Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani ni tukio muhimu sana, linalopaswa kuacha chapa ya kudumu katika maisha ya vijana duniani. Hili ni jukwaa lenye utajiri mkubwa wa tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kijamii. Hiki ni kipindi cha neema, baraka na changamoto kwa vijana kuendelea kuwa ni vyombo na mashuhuda wa furaha ya Injili ya Kristo Yesu miongoni mwa vijana wenzao, kwa kujikita katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Ni kipindi cha katekesi makini na endelevu miongoni mwa vijana!
Ujumbe wa Tanzania wenye idadi ya watu 21, katika maadhimisho haya unaongozwa na Askofu Desiderius Rwoma na Padre Liberatus Kadio, Mkurugenzi wa utume wa vijana kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania. Askofu Msaidizi Eusebius Nzigilwa wa Jimbo kuu la Dar es Salaam ambaye pia yuko nchini Panama wakati huu anasema, maadhimisho haya ni tukio la kiimani na kihija, linalowashirikisha viongozi wa Kanisa na waamini walei, kama sehemu ya mchakato wa kuwajengea vijana uwezo kutangaza, kushuhudia na kuinjilisha.
Vijana katika maisha yao wana malengo, mipango na mikakati yao, lakini wanapaswa kuwa tayari kujibu na kutekeleza wito wa Mungu kama ilivyokuwa kwa Bikira Maria katika ujana wake. Bikira Maria aliweza kujibu wito wa Mungu kwa moyo, imani na matumaini thabiti. Hata leo hii, Askofu Msaidizi Nzigilwa anasema vijana wanapaswa kuwa ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu, kwa kukaza masikio ya mioyo yao ili kusikiliza sauti ya Mungu na hatimaye, kuijibu kikamilifu!
Katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia kuna kelele nyingi zinazowachanganya na kuwavuruga vijana kiasi cha kupoteza dira na mwelekeo wa maisha na matokeo yake ni vijana wengi kujikuta wametumbukia katika giza la udanganyifu na mmong’onyoko wa maadili na utu wema. Vijana wanapaswa kukumbuka kwamba, wao ni leo na kesho ya maisha na utume wa Kanisa na Jamii katika ujumla wake. Vijana ni nguvu, jeuri na matumaini ya Kanisa na kwamba, wao ni chachu ya mageuzi yanayojikita katika mwanga wa Injili na Mafundisho Jamii ya Kanisa!
Askofu Msaidizi Nzigilwa anakaza kusema, katika hija hii, vijana wanasindikizwa kwa mfano na maombezi ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa aliyediriki kusema, “Tazama, mimi ni mjakazi wa Bwana; iwe kwangu kama ulivyosema”. Lk. 1:38. Huu ni ushuhuda wa ujasiri na ukarimu kwa mwamini aliyetambua siri ya wito wake, tayari kujitosa kimasomaso bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani. Bikira Maria, katika ujana wake, alibahatika kushirikishwa na Mwenyezi Mungu mpango wa Ukombozi, kwa kuwa ni Tabernakulo ya kwanza ya Neno wa Mungu aliyefanyika mwili.
Hata baada ya kumzaa mwanaye wa pekee, akaendelea kupeta katika “ujana wake” kwa kuwa ni mwanafunzi mahiri wa Mwanaye Kristo Yesu, akaandamana naye kwenye Njia ya Msalaba, hadi akadiriki kusimama chini ya Msalaba, akimwona Mwanaye akiinamisha kichwa na kukata roho! Hata baada ya Kupalizwa mbinguni mwili na roho, Bikira Maria ameendelea kuwa kijana kutokana na utakatifu wa maisha ulioko ndani mwake!
Maadhimisho ya Siku ya XXXIV ya Vijana Duniani kwa mwaka 2019 yameiwezesha Panama kuwa ni daraja linalowakutanisha vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia kusikiliza kile ambacho Kanisa linataka kuwapatia kama dira na mwongozo wa maisha baada ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya vijana iliyofanyika mwaka 2018. Ni fursa kwa vijana pia kujenga utamaduni wa majadiliano ya kiekumene katika sala na maisha ya kiroho; katika huduma na ushuhuda wenye mvuto na mashiko, ikizingatiwa kwamba, maadhimisho haya yanakwenda sanjari na Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo, linaongozwa na kauli mbiu “Yaliyo ya haki kabisa ndiyo utakayoyafuata”. Kumb. 16:18-20.
Sehemu hii ya Maandiko Matakatifu inakazia: haki kati ya watu wa Mungu; inakataza rushwa na ufisadi; kwani rushwa hupofusha macho ya wenye akili, na kugeuza daawa ya wenye haki. Wakristo wanahamasishwa kutafuta haki na kuiambata ili waweze kuirithi nchi ya ahadi wapewayo na Mwenyezi Mungu. Tafakari ya Juma la Kuombea Umoja wa Wakristo kwa mwaka huu, imeandaliwa na Wakristo kutoka nchini Indonesia na Juma linafungwa tarehe 25 Januari, katika Sherehe ya Kuongoka kwa Mtakatifu Paulo, Mtume na Mwalimu wa Mataifa! Wakristo wanahamasishwa kudumisha umoja katika utofauti uliopatanishwa kwa njia ya Damu Azizi ya Kristo! Licha ya tofauti mbali mbali zilizopo miongoni mwa Wakristo, lakini kuna mambo msingi yanayowaunganisha kwa pamoja: Imani yao kwa Kristo Yesu, Sakramenti ya Ubatizo na Maandiko Matakatifu.
Maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani, ni fursa kwa Mama Kanisa kukuza na kudumisha utume wake miongoni mwa vijana wa kizazi kipya: kwa kuwasikiliza, kuwasindikiza na kuwasaidia kufanya maamuzi magumu katika maisha yao kadiri ya mwanga wa Injili ya Kristo na Mafundisho Jamii ya Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko anawakumbusha vijana kwamba, mapinduzi ya huduma ndiyo nguvu na jeuri ya vijana wa kizazi kipya! Vijana kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaendelea kushangazwa na ukarimu unaooneshwa na familia ya Mungu nchini Panama!
Vijana wanaendelea kushangazwa na neema, huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Kwa hakika vijana wanahamasishwa kuwa ni chumvi ya dunia na mwanga wa mataifa, kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko, ili kweli dunia iweze kuwa ni mahali pa furaha, amani, upendo na mshikamano! Vijana wanaendelea pia na shuhuda pamoja na katekesi katika Parokia mbali mbali mjini Panama kama sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Vijana Duniani.
Maoni
Ingia utoe maoni