Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na rais wa Ufaransa Emmanuel Macron wanatarajiwa kutia saini mkataba mpya wa urafiki baina ya nchi zao, katika mji wa magharibi nchini Ujerumani wa Aachen Jumanne(22.01.2019).
Utiaji saini mkataba huo unajiri mnamo wakati wa maadhimisho ya miaka 56 ya kutiwa saini kwa makubaliano ya Elysee mjini Paris.
Mkataba huo wa Aachen unaziweka nchi hizo mbili jirani katika dhamira ya kuimarisha ushirikiano wao katika sera za Umoja wa Ulaya na kufanyakazi kuelekea katika sera ya pamoja ya mambo ya kigeni na usalama. Kufanyakazi kwa pamoja katika masuala ya kiuchumi pia kutaimarishwa. Mkataba huo utahitaji kuidhinishwa na mabunge ya nchi zote kabla ya utekelezaji wake.
Katika mahojiano na vyombo vya habari kabla ya mkutano huo, mwanasiasa mkongwe wa Ujerumani kutoka chama cha Christian Democratic Union CDU Wolfgang Schaeuble, ambaye kwa sasa ni spika wa bunge la Ujerumani Bundestag, ametoa wito wa kuwa na malengo mapana ya sera za Umoja wa Ulaya.
Ushirikiano wa karibu unahitajika
Amesema kwa mara nyingine Ujerumani na Ufaransa zinahitaji miradi ya maana na dhabiti ya ujumuisho ambayo inaweka wazi kwa wananchi kwamba Ulaya inafanikisha mambo katika kiwango tofauti kabisa na ubora kuliko kila nchi pekee yake.
Sanamu lililoko katika mji wa magharibi nchini Ujerumani wa Aachen likiwa katikati ya bendera za Ujerumani na Ufaransa
Katika uhariri ulioandikwa katika gazeti la Neue Presse leo, waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Heiko Maas ametoa wito wa ushirikiano wa karibu baina ya Ufaransa na Ujerumani mnamo wakati ambapo siasa kali za mrengo wa kulia zinaongezeka, kuna mifarakano ya kibiashara na mizozo inaliathiri bara la Ulaya.
Amesema hakupaswi kuwepo hali ya kubweteka, na kuongeza kuwa uhusiano imara wa Ufaransa na Ujerumani, unahitaji kutekelezwa ili kuwezesha kuhudumia Ulaya iliyo imara na yenye uwezo.
Chama cha Social Democratic SPD, chama kinachoshiriki katika kuunda serikali ya muungano mkuu unaoongozwa na kansela Merkel, pia kimetoa wito wa uharaka wa utekelezaji huo.
Mbunge mwandamizi kutoka chama hicho Achim Post amesema kwa muda mrefu sana, kansela Merkel hususan amesababisha juhudi za Ulaya kutoka kwa rais wa Ufaransa kuyeyuka.
Mkataba wa Elysee
Januari 22, mwaka 1963, rais wa Ufaransa Charles de Gaulle na kansela wa kwanza wa Ujerumani baada ya vita Konrad Adenauer walitia saini mkataba wa Elysee ambao uliweka njia ya mashauriano ya kila mara kati ya mahasimu hao wa zamani katika ngazi ya juu ya serikali.
Nchi hizo mbili hivi sasa zinasogea katika kuimarisha uhusiano wao wakati ambapo Umoja wa Ulaya uko katika hali ya mkanganyiko.
Talaka baina ya Umoja huo na Uingereza, maarufu kama Brexit inakaribia. Merkel, kansela wa Ujerumani tangu mwaka 2005, ameamua kuachana na uongozi wa chama chake cha CDU na hatagombea tena uchaguzi ujao.
Na Macron anakabiliwa na wiki kadhaa za maandamano ya kile kinachojulikana kama , "maandamano ya vizibao vya manjano" kutokana na kupanda kwa gharama za maisha pamoja na kodi nchini Ufaransa.
Maoni
Ingia utoe maoni