Alhamisi. 21 Novemba. 2024
feature-top
Kenya ilikuwa imejianda vilivyo kukabiliana na shambulio la kigaidi la hoteli ya DusitD2 kuliko mashambulio mengine hapo awali.

Watuhumiwa wa ugaidi waliokuwa wakisakwa na mamlaka Kenya wamejisalimisha.

Inaaminika kwamba walijisalimisha katika kituo kimoja cha polisi mjini Isiolo , kaskazini mwa mji mkuu wa Nairobi.

Wakati huohuo vikosi vya usalama nchini Kenya vinasema kuwa vimetibua shambulio katika eneo la kasakzini mashariki mwa mji wa Nairobi karibu na mpaka na Somalia. mamalaka inasema kuwa wapiganaji walikuwa wamelanga kampuni mbili za ujenzi mjini Garissa.

Wanasema kuwa maafia wa jeshi wakishirikiana na wale wa polisi walijibu shambulio hilo na kuwaua takriban wapiganaji wanne.

Hakuna afisa hata mmoja ama hata wafanyikazi wa ujenzi huo walioripotiwa kuuawa.

Kenya inaendelea kukabiliana na matokeo ya shambulio katika hoteli ambapo takriban watu 21 waliuawa. Kundi la alshabab kutoka Somali limekiri kutekeleza shambulio hilo.

Watu kadhaa kufikia sasa wamekamatwa kuhusiana na shambulio hilo na maafisa wa polisi wamechapisha picha za watu wengine wanane wanaosakwa.

Wakati huohuo wazazi wa watu watatu waliojisalmisha katika kituo cha polisi cha kaunti ya Isiolo wamesema kuwa wanao hawana hatia na wako hatarini.

Lakini licha ya kujisalimisha, wazazi wa washukiwa wamesema kuwa kesi zinazowakabili wanao zimekuwa zikiendelea na kwamba wamekuwa wakishirikiana na maafisa wa polisi, hivyobasi wakataka kujua ni kwa nini majina yao yalikuwa katika orodha hiyo ya magaidi wanaosakwa na serikali ya Kenya.

Kulingana na Daily Nation wazazi hao kutoka eneo la Tulloroba mjini Isiolo waliwasilisha malalamishi yao kwa naibu kamishna wa kaunti hiyo kufuatia kutolewa kwa rodha hiyo na shirika la huduma za polisi.

Walisema kuwa walishangazwa wakati walipoona majina ya watoto wao katika vyombo vya habari siku ya Jumapili usiku licha ya kwamba wamekuwa tayari kuwawasilisha kwa mkurugenzi wa kitengo cha jinai pamoja na kitengo kinachokabiliana na ugaidi kuhijiwa.

Bwana Abdi Bidu babake mmoja ya washukiwa hao alielezea kwamba watatu hao walijaribu kuvuka Somalia 2017 lakini wakakamatwa.

Alisema kuwa kesi zao zinaendelea lakini walikuwa wameachiliwa kwa dhamana.

Usalama wao

Wazazi hao wamesema kuwa wanao kwa sasa ni wahudumu wa boda boda katika mji wa Isiolo na kwamba wamebadilika na kuanza kuipatia serikali habari.

Ndugu mmoja wa washukiwa hao Hussein Wario ameitaka serikali kuwahakikishia usalama watatu hao.

Amesema kuwa ndugu yao alikamatwa akitazama soka katika ukumbi mmoja miaka mitatu iliopita.

Kulingana na gazeti la Daily Nation, washukiwa hao wamekuwa wakiripoti kwa kitengo cha kukabiliana na ugaidi ATPU kama walivyoagizwa.

Kulingana na wazazi hao, maafisa wa kitengo cha kupambana na ugaidi ATPU wanawafahamu washukiwa hao lakini hawana uelewa kuhusu orodha hiyo.

Bi Halima Boru amesema kuwa mwanawe alikuwa akiuza mitumba alipokamatwa miaka mitatu iliopita.

Muungano wa wazazi mjini Isiolo ambaye mwenyekiti wake aliandamana na wazazi hao hadi kwa naibu kamishna wa kaunti hiyo alihoji lengo la serikali kuchapisha orodha hiyo licha ya kesi inayowakabili wanao kutokamilika.

Uchunguzi

Maafisa wa polisi wamewakamata watu kadhaa kufuatia shambulio la tarehe 15 la al-Shabab katika hoteli ya DusitD2 iliopo katika eneo la Riverside jijini Nairobi.

Siku ya Jumapili , polisi walichapisha orodha ya picha za watu wanane waliokuwa wakisakwa kuhusu shambulio hilo la kigaidi.


Maoni


Ingia utoe maoni