Alhamisi. 21 Novemba. 2024
feature-top
Vikosi vya ulinzi wa angani Syria vinasema vimezuia makombora ya Israel

Jeshi la Israel linasema limeanza kushambulia maeneo yanayodhibitiwa na jeshi la Iran nchini Syria.

Kikosi cha ulinzi Israel (IDF) kinasema operesheni yake ni dhidi ya kikosi cha Quds - kikosi maalum katika jeshi la mapinduzi la Iran.

Haikutoa ufafanuzi zaidi. Lakini kuna taarifa kuhusu makombora yaliofyetuliwa katika maeneo yanayo uzunguka mji mkuu wa Syria, Damascus mapema Jumatatu.

Vyombo vya habari nchini Syria vinasema vikosi vya ulinzi wa angani vimezuia 'shambulio la Israel'. Siku ya Jumapili jeshi la Isarel lilisema limezuia kombora katika eneo la Golan Heights.

Tunafahamu nini kuhusu operesheni hiyo?

Kikosi cha Israel IDF kilitangaza kuanza kwa operesheni hiyo kupitia ujumbe wa tweeter mapema leo Jumatatu.

Televisheni ya taifa nchini Syria Sana imenukuu duru katika jeshi kwamba kikosi cha ulinzi wa angani nchini humo kimedhibiti 'makombora kutoka kwa adui'.

Shirika linaloangalia haki za binaadamu nchini Syria lililo na makao yake nchini Uingereza (SOHR) linasema makombora ya Israeli yalikuwa yanalenga "maeneo ya mji mkuu Damascus".

Watu walioshuhudia mjini Damascus wanasema walisikia milipuko mikubwa angani usiku.

Shirika hilo la SOHR baadaye lilieleza kwamba makombora ya Israel yameharibu maghala ya silaha na kambi za kijeshi zinazomilikiwana Iran na kundi linaloungwa mkono na Iran la Hezbollah.

SOHR limeongeza kwamba kuna watu waliofariki kutokana na shambulio hilo.

Onyo la Netanyahu

Operesheni hiyo inajiri baada ya Israeli kusema kwamba 'kombora la roketi lililofyetuliwa kaskazini mwa eneo la Golan Heights na lilidhibitiwa na mfumo wa ulinzi ".

Eneo ambalo ni kivutio kikubwa msimu wa baridi katika mlima Hermon katika eneo hilo la Golan Heights lilifungwa kutokana na yaliotukia.

Waziri mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu alitoa onyo kali wakati wa ziara yake nchini Chad hapo jana Jumapili.


"Tuna sera iliyopangwa, kulenga maeneo yanayodhibitiwa na Iran nchini, na kumdhuru yoyote aliyejaribu kutudhuru," alisema.

Ni nadra kwa Israel kukiri kueteleza mashambulio katika maeneo nchini Syria.

Lakini mnamo Mei 2018, Israel ilisema ilishambulia karibu miundo mbinu yote ya kijeshi ya Iran huko katika shambulio lake kubwa tangu kuanza kwa vita vya kiraia nchini Syria mnamo 2011.

Maoni


Ingia utoe maoni