Alhamisi. 21 Novemba. 2024
feature-top

Shambulio lililotekelezwa na wapiganaji wa Kisomali jijini Nairobi tarehe 15 Januari ni mapinduzi makubwa ya Propaganda kwa upande wa wapiganaji hao na kusisitiza wasiwasi kuhusu uwezo wa Kenya kukabiliana na ugaidi.

Wapiganaji hao walitumia vilipuzi na risasi kuingia katika hoteli ya kifahari ya DusitD2 na ofisi nyengine zilizopo katika eneo la Riverside Drive 14 katika eneo la Westlands, karibu na duka la jumla la West Gate Mall ambalo lilishambuliwa 2013.

Rais Uhuru Kenyatta alisema mnamo tarehe 16 Januari kwamba watu 14 waliuawa katika shambulio hilo na kwamba magaidi wote waliangamizwa.

Kanda za kamera za CCTV zilizopeperushwa hewani na vyombo vya habari viliwaonyesha watu wanne waliokuwa wamevalia magwanda meusi wakifyatua risasi za rashasha walipokuwa wakiingia katika hoteli hiyo.

Kumbukumbu za West Gate.
Kundi la Al-Qaeda linalohusiana na wapiganaji wa al-Shabab waliodai kutekeleza shambulio la Westgate Mall ambapo takriban watu 67walifariki walidai kutekeleza shambulio hilo.

Wamedai kuwaua watu 47.

Shambulio hilo lilitokea siku moja baada ya mahakama ya Nairobi kuwashtaki watu watatu kwa mashtaka ya kuwasaidia al-Shabab kutekeleza shambulio la West gate.

Hoteli ya DusitD2 inarudisha kumbukumbu ya uwezo wa al-Shabab kushambulia ndani ya Kenya, kinyume na madai ya serikali kwamba wanajihad hao wamezuiliwa katika maeneo ya mpakani na Somalia.

Nchini Somalia , kundi la al-Shabab linasalia kuwa tishio kubwa la usalama licha ya operesheni za hivi majuzi za kijeshi na mashambulio ya angani yaliotekelezwa na vikosi vya usalama, wanajeshi wa Muungano wa Afrika AU na vikosi vya Marekani.

Kundi hilo la Kijihad linadhibiti maeneo mengi ya Somali ya kati pamoja na kusini.

Kwa nini Kenya inalengwa?
Al-Shabab iliimarisha mashambulio yake nchini Kenya wakati serikali ilipotuma wanajeshi wake nchini Somalia kukabiliana na kundi hilo 2011.

Wapiganaji hao waliitaka Kenya kuondoka nchini humo na kuapa kulipiza kisasi.

Wito wa serikali kuondoa wanajeshi wake nchini Somalia umekandamizwa na madai kwamba ujumbe huo una wajibu wa kizalendo.

Wengine wamesema kuwa kuondoka kwa wanajeshi wa Kenya nchini Somalia ni sawa na ushindi wa al-shabab.

Mamia ya wanajeshi wa Kenya wameuawa na wapiganaji wa Alshabab nchini Somalia katika kipindi cha miaka minane iliopita.

Serikali imetetea uwepo wa wanajeshi wake nchini Somalia licha ya wito wa mara kwa mara wa kutaka kuondoka kwa mpangilio, ambao baadhi ya wanaharakati wanasema haufanyiki.

Mpaka wa Kenya na Somalia.
Kenya inagawana mpaka mrefu na wenye mwanya mkubwa na Somalia. Taifa hilo lililopo katika upembe wa Afrika limekosa uthabiti tangu rais Siad Barre aondolewe madarakani 1991.

Mwaka 2017, serikali ya kenya imesema kuwa itajenga ukuta katika mpaka na Somalia ili kuwazuia wapiganaji kuingia nchini.

Ujenzi wa ukuta huo wenye kilomita 700 ulisitishwa mnamo mwezi Machi 2018 kufuatia mgogoro kati ya Wakenya na Wasomalia wanaoishi katika eneo hilo.

Alshabab limekiri kutekeleza baadhi ya mashambulio ya kiwango cha chini nchini Kenya , ijapokuwa baadhi yao huenda yalitekelezwa na baadhi ya makundi ambayo hayashirikiani na kundi hilo lakini yanafuata itikadi yao.

Tangu kisa cha West gate Mall, al-Shabab limetekeleza shambulio moja katika taifa hilo na mengine ya viwango vya chini katika maeneo ya kaskazini mashariki na maeneo ya pwani karibu na mpaka na Somalia.

Mnamo mwezi Aprili 2 2015, kundi hilo liliwaua watu 148 , wengi wao wakiwa wanafunzi katika chuo kikuu cha Garissa katika eneo la Kaskazini mashariki.


Athari za shambulio la DusitD2
Shambulio hilo litapiga jeki propangada ya kundi la al-Shabab nchini Somalia pamoja na mataifa ya Afrika mashariki yanayochangia wanajeshi wake katika vita dhidi ya ugaidi.

Wapiganaji hao watalitumia shambulio hilo kuonyesha uwezo wao kushambulia nchini Kenya hususan maeneo yanayotembelewa mara kwa mara na wageni pamoja na maafisa wa serikali.

Pia wana uwezo wa kutumia shambulio hilo kuonyesha uwezo wao mbele ya makundi mengine yanayotii kundi la Islamic State.

Kutakuwa na wito nchini Kenya wa kuimarishwa kwa usalama katika majumba kadhaa na hususan maduka ya jumla ambayo huenda yakapoteza biashara.

Duka lolote linalopendwa sana na wageni pamoja na majumba yenye afisi za kampuni za kigeni yatazua wasiwasi kuhusu usalama uliowekwa baada ya shambulio la West Gate.

Je raia wa Kenya wenye mizizi yao Somalia watashutumiwa?

Kufuatia shambulio hilo, vikosi vya ujasusi pamoja na washirika wao wa magharibi watalazimika kukabiliana na seli za kigaidi nchini.

Huenda kukawa na shinikizo ya kuangazia upya kitengo cha ujasusi ili kujilinda dhidi ya mashambulio mengine katika siku za usoni.

Vikosi vyya usalama vimepongezwa kwa kuchukua hatua mwafaka ikilinganishwa na hatua walizochukua wakati wa shambulio la West Gate ambalo lilitajwa kuwa janga.

Haitarajiwi kwamba kutakuwa na vita dhidi ya Waislamu ama hata dhidi ya raia wa Kisomali kufuatia shambulio hilo.

Hatahivyo mamlaka itakuwa katika shinikizo la kujadiliana na jamii hizo zaidi ili kusaidia katika ujasusi.

Waislamu na raia wa kabila la Somali katika siku zililzopita wamelalamika kuhusu kukandamizwa na kunyanyaswa na vikosi vya usalama.

Wakati huohuo wito wa serikali kuondoa wanajeshi wake Somalia huenda ukaanza tena kutolewa.

Maoni


Ingia utoe maoni