Bunge nchini Burundi limeidhinisha mswada wa sheria ya kuhamisha mji mkuu ya serikali kutoka Bujumbura hadi Gitega.
Bujumbura itasalia kuwa mji wa kibishara wa taifa hilo dogo katika kanda ya Afrika Masharika.
Akielezea kwa kina mpango huo waziri wa mambo ya ndani Pascal Barandagie alisema "lengo la hatua hii kwanza ni kuwasongezea utawala wananchi wa mikoa mbalimbali, na kutenganisha makao makuu ya kisiasa na kiuchumi kwa kuacha mji wa Bujumbura kuwa mji wa kibiashara".
Mpango huo pia unalenga, kupunguza dhana ya watu wa mikoani kwamba Bujumbura ndio sehemu tu ya kufaulu maishani na hivyo kutoa fursa kwa mji huo kupumua kutokana na msongamano wa watu.
Serikali imetilia maanani suala la usalama ikisema kwamba Gitega ni mahali salama zaidi ikizingatiwa kuwa iko katikati ya Burundi tofauti na Bujumbura ambayo iko pembezoni na karibu nampaka na nchi jirani.
Tayari serikali ya Burundi imetangaza kuwa vikao vya baraza la mawaziri vitafanyika mjini Gitega kuanzia mwezi hu wa Januari.
Wizara tano za serikali pia zinatarajiwa kuhamia mji mkuu huo mpya wa Burundi.
Baraza la seneti linaelekea kukamilisha maandalizi yake ya kuhamia mji huo uliyo na wakaazi laki tatu.
Hata hivyo mji wa Gitega unakabiliwa na changamoto kadhaa za miundo mbinu.
Hali ambayo baadhi ya wabunge wanatilia shaka licha ya kuidhinisha mswada wa kuupandisha hadhi kama alivyokiri spika wa bunge Pascal Nyabenda.
"Tunahitaji Gitega kama mji mkuu wa kisasa lakini tukiri kuwa nji huo waujatimiza vigezo vyote na masharti ya kuwa mji mkuu, Gitega ilivyo kwa sasa haina uwezo wa kupokea idara zote za serikali".
"Pamoja na kuidhinishwa mswada huo spika aliongeza kuwa kuna haja ya kukamilisha maandalizi na kuepuka malalamiko ya watu" , Alisema bwana Nyabenda.
Changamoto kubwa inayokumba mji wa Gitega ni ukosefu wa makaazi, hoteli, nyumba za kiofisi pamoja na uhaba wa maji safi.
Rais Nkurunziza alipoingia madarakani mwaka 2005 aliahidi kwamba atahakikisha kuwa makao makuu ya ufalme ya hapo zamani yanarudi kuwa mji mkuu wa nchi hiyo.
Je unafahamu historia ya Gitega?
- Gitega ni moja ya mikoa 18 nchini Burundi.
- Mji wa Gitega, ulikua ukifahamika kama Kitega, upo eneo la katikati ya Burundi.
- Uko kilo mita 65 mashariki mwa mji mkuu wa Bujumbura.
- Kwa karne kadhaa Gitega imekua makao makuu ya ufalme wa mwami nchini Burundi.
- Mji huo pia ulikua makao makuu ya utawala wa wakoloni kabla ya nchi hiyo kupata uhuru.
Mwaka 2017 serikali ya Burundi ilitangaza mpango wake wa kuhamisha mji mkuu wa nchi hiyo kutoka Bujumbura hadi Gitega.
Kama mji wa pili kwa ukubwa nchini Gitega inajivunia kuwa kituo cha kidini na elimu.
Mji huo una shule za msingi, sekondari, taasisi za kiufundi,pamoja na maeneo ya ibada kwa Waislam, Wakatoliki, na Waprotestanti.
Makavazi ya Taifa, ambayo inaangazia ya historia na sanaa, pia ipo katika mji wa Gitega.
Wakaazi wa mji huo na maeneo yaliyo karibu wanajihusisha na kiliomo na ufugaji.
Maoni
Ingia utoe maoni