Baraza la Makanisa Ulimwenguni, kwa mara nyingine tena, linachukua fursa hii kulaani vikali vitendo vyote vya kigaidi vinavyohatarisha usalama wa raia na mali zao. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, hawana budi kujitokeza si tu kulaani vitendo hivi vya kigaidi, bali kuunga mkono mchakato wa kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu.
Dr. Olav Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni katika taarifa yake kwa vyombo vya habari anasema, wamesikitishwa sana na shambulizi la kigaidi lililotokea katika hoteli ya DusitD2 eneo la 14 Riverside Drive, Jijini Nairobi siku ya Jumanne, tarehe 15 Januari 2019 na kusababisha watu zaidi ya 15 kupoteza maisha na wengine wengi kujeruhiwa. Baraza la Makanisa Ulimwenguni linapenda kutuma salam za rambi rambi kwa wale wote walioguswa na maafa haya na kwamba, linaziombea roho za marehemu zipate pumziko la milele huko mbinguni! Kwa majeruhi waweze kupona haraka na hatimaye, kurejea katika shughuli zao za kila siku!
Baraza la Makanisa Ulimwenguni, kwa mara nyingine tena, linachukua fursa hii kulaani vikali vitendo vyote vya kigaidi vinavyohatarisha usalama wa raia na mali zao. Waamini na watu wote wenye mapenzi mema, hawana budi kujitokeza si tu kulaani vitendo hivi vya kigaidi, bali kuunga mkono mchakato wa kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu na kamwe wananchi wasikubali kuvurugwa na misimamo mikali inayofumbatwa katika chuki na hatimaye, kutumbukia katika mipasuko, kinzani na migawanyiko isiyokuwa na tija wala mashiko kwa ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!
Baraza la Makanisa Ulimwenguni linawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuendelea kusali kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea watu wote walioathirika kutokana na shambulizi hili la kigaidi. Hiki ni kipindi cha kuonesha mshikamano wa dhati na familia ya Mungu nchini Kenya, ambayo kwa miaka ya hivi karibuni, imeendelea kujielekeza zaidi katika mchakato wa kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano ndani na nje ya Kenya yenyewe! Lakini sasa, Kenya yenyewe ndiyo iliyoshambuliwa na magaidi. Dr. Olav Fykse Tveit, Katibu mkuu wa Baraza la Makanisa Ulimwenguni anahitimisha salam za rambi rambi kwa kumwomba Mwenyezi Mungu awakirimie wananchi wa Kenya huruma, upendo na neema, ili waendelee kujikita katika hija inayofumbatwa katika haki na amani!
Maoni
Ingia utoe maoni