Baraza la Maaskofu Katoliki DRC, CENCO pamoja na Bwana Martin Fayulu kutoka Chama cha Upinzani. Wanasema, matokeo ya uchaguzi mkuu nchini humo yamechakachuliwa na hayalandani kabisa na takwimu zilizokusanywa na waangalizi 40, 000 kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki DRC, waliokuwa wamesambazwa katika vituo mbali mbali vya uchaguzi nchini humo.
Matokeo ya Uchaguzi Mkuu yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Watu wa Congo, CENI, Alhamisi, tarehe 10 Januari 2019 kwa kumtangaza Bwana Felix Tshisekedi kutoka Chama cha upinzani cha UDPS kuwa ni “mshindi wa mpito” wa Uchaguzi mkuu uliofanyika nchini humo hapo tarehe 30 Desemba 2018 yamepingwa na Baraza la Maaskofu Katoliki DRC, CENCO pamoja na Bwana Martin Fayulu kutoka Chama cha Upinzani.
Wanasema, matokeo ya uchaguzi mkuu nchini humo yamechakachuliwa na hayarandani kabisa na takwimu zilizokusanywa na waangalizi 40, 000 kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki DRC, waliokuwa wamesambazwa katika vituo mbali mbali vya uchaguzi nchini humo. Hayo yamebainishwa na Padre Donatien Nshole, Katibu mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki DRC lakini bila kutaja jina la mshindi katika uchaguzi huo. Hata hivyo, Maaskofu nchini DRC wanawataka wale wote ambao wanaona kwamba, hawakutendewa haki katika mchakato wa uchaguzi mkuu kufuata sheria, taratibu na kanuni za nchi ili haki iweze kutendeka.
Baraza la Maaskofu Katoliki DRC linaitaka familia ya Mungu nchini humo kudumisha ustaarabu, amani na utulivu kwa kuondokana na vitendo vyovyote vile vinavyoweza kusababisha uvunjifu wa amani na mipasuko ya kijamii. Hivi karibuni, Tume ya Uchaguzi nchini DRC inatarajia kutangaza matokeo ya uchaguzi mkuu. Wito kama huu, umetolewa pia na Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Bwana Antonio Guterres pamoja na Umoja wa Afrika unaotaka suluhu ya matokeo ya uchaguzi mkuu nchini DRC ifanyike kwa njia ya amani na majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kudumisha amani na utulivu!
Rais Joseph Kabila anayemaliza muda wake wa uongozi, ataendelea kubaki madarakani hadi hapo, Rais mteule atakapoapishwa na kuanza kushika madaraka, kama inavyoelezwa kwenye Katiba! Bwana Jean Yves Le Drian, Waziri wa Mambo ya nchi za nje wa Ufaransa anasema, matokeo ya uchaguzi mkuu nchini DRC hayalandani na ukweli wa mambo na kwamba, Ufaransa imeonesha nia ya kutaka kuipeleka kesi hii kwenye Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa, ili kupata ufafanuzi wa kina. Ikiwa kama mambo yote yatakwenda kama yalivyopangwa, Rais mpya anatarajiwa kuapishwa hapo tarehhe 18 Januari 2019, siku ambayo familia ya Mungu nchini DRC inatamani kuiona katika hali ya amani, utulivu na mshikamano wa kitaifa.
Maoni
Ingia utoe maoni