Jumatano. 11 Septemba. 2024
feature-top
Kuanzia tarehe 18-25 Januari ni Wiki ya Kuombe Umoja wa Wakristo ikiongozwa na Kauli mbiu kutoka kitabu cha Matendo ya Mitume 28,2 ambapo Paulo anasifu ukarimu wa watu wa kisiwa cha Malta

Wiki ya kuombea Umoja wa Wakristo mwaka huu imebeba kauli mbiu kutoka katika kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo28,2) inayosema:“wenyeji wakatufanyia fadhili zisizokuwa za kawaida”… kifungu hiki cha Biblia kinatuingiza katika tafakari ya ‘fadhila ya ukarimu’.Tafakari yetu ya Neno la Mungu kwa siku nane itusaidie kujichunguza nafsini mwetu ni kwa jinsi gani tunakarimu wengine?

Wakristo ulimwenguni kote tunaalikwa kukusanyika pamoja ili kusali kwa ajili ya umoja wetu wa Kiristo. Wiki ya kuombea umoja wa wakristo mwaka 2020 inaongozwa na kauli mbiu kutoka katika kitabu cha Matendo ya Mitume (Mdo 28,2) inayosema “wenyeji wakatufanyia fadhili zisizokuwa za kawaida”, kifungu hiki cha Biblia kinatuleta katika tafakari ya ‘fadhila ya ukarimu’. Fadhila hii hukosekana miongoni mwetu pale ambapo tunaanza kujitenga na Mungu, pale ambapo tunashindwa kuiishi Injili ya Kristu na kugugumia ya ulimwengu ambamo ufisadi, uchoyo, ukosefu wa haki umesababisha kukosekana kwa upendo na hatimaye kusababisha ubinafsi na mgawanyiko, kama vile Papa Francisko katika hotuba nyingi anasisitizia juu ya hilo. Sala tunazosali zisaidie kuamsha ari ya kulijua Neno la Mungu na kuungana kidugu ndani ya ulimwengu huu geugeu. Tukiwa tunaishi ndani ya ulimwengu huu uliojaa kila aina ya dhuruma, na kama Wakristo, tumeitwa kutoa ushuhuda wa Injili, na kuwa chombo cha neema ya Mungu ya uponyaji katika ulimwengu uliojaa kila aina ya dhulma. Aidha katika ulimwengu ambao ukosefu wa haki unatawala, jamii za Kikristo kupitia umoja wao zinapaswa kujitokeza katika sala ili kuombea ulimwengu na hatimaye wema, ukarimu na haki viweze kutawala. Pia ni muda wa kujitafakari sisi kama wakristo, kujichunguza na kubaini ni kwa njia gani nasi tunakurupusha kuliishi Neno la Mungu katika maisha yetu na kuwa chanzo cha mgawanyiko huu unadhihirika wazi katika jamii tunamoishi.

Kristo ndiye mwanzilishi wa sala ya kuombea umoja

Sala ya kuombea umoja wa wakaristo ilianzishwa na Kristo mwenyewe wakati akisali kuombea umoja wa Kanisa lake na ambayo ni sala maaruf ujulikanyo akisema “ili wote wawe wamoja” (Yoh 17:21). Tukizingatia sala hiyo, sisi wakristo tunapaswa kuwa mashuhuda wa Neno wa Mungu na watangazaji hodari wa Injili. Tunaweza kufanya hivyo hasa kupitia umoja wetu katika Kristo tukimtangaza kwa matendo yetu ili ulimwengu uweze kumtambua. Kama watu wa Agano lililoanzishwa na Kristo, tunaalikwa kuiishi hotuba ya Kristo ya mlimani (Mt 5:1-12) na zaidi kwa kipindi hiki cha kuombea umoja wetu ambao kauli mbiu yake ni ‘fadhila ya ukarimu’ tunaalikwa tuwe wakarimu kwani yeye alisema “heri wenye moyo safi maana hao watamwona Mungu” (Mt 5:8). Kumwona Mungu ni kuingia katika ufalme wake. Kanisa la Kristo linaitwa kuwa matunda ya kwanza ya ufalme huu. Walakini, ikiwa tutabaki katika utengano hakika tutashindwa kuwa ishara ya upendo wa Mungu kwa watu wake. Kwa hiyo, tukiwa tunaombea umoja wetu tunaalikwa kuungana chini ya msalaba wa Kristo, tukiomba neema zake kupigana na dhulma, na tukiomba rehema zake kwa dhambi zetu zinazosababisha mgawanyiko wetu.

Papa Francisko na Ukarimu

Katika tafakari ya katekesi aliyoitoa kwa mahujaji waliokusanyika ndani ya Ukumbi wa Paulo VI Vatican tarehe 8 januari 2020, Papa Francisko aliwatanabahisha waumini wasome kwa makini kitabu cha Matendo ya Mitume. Kwa kukisoma watagundua namna ambavyo Injili ya Kristo ina nguvu ya kuwafikia watu wote ulimwenguni hata kwenye mazingira hatarishi. Akielezea safari ya Mtume Paulo, Papa Francisko alisema kuwa ilikuwa safari ngumu, ilikuwa imejaa mahangaiko na majaribu mengi, bado Mungu alimsimamia kwa kumpa nguvu naye akawa mlinzi wa maisha ya wengine akiwatia moyo wa matumaini. Aliweza kusaidiwa na watu wakarimu wa nchi ya Malta kwa kupatiwa mahitaji msingi na Mungu akawabariki watu hao. Kutokana na hilo tunajifunza kuwa ukarimu hufungua baraka za Mwenyezi Mungu maishani mwetu. Sisi kama wakristo, tukiwa tunasali kwa ajili ya umoja wetu tusali pia kuomba fadhila hiyo ya ukarimu ili tuweze kupokea baraka za Mungu maishani mwetu. Hata hivyo katika mada hii ya ya ukarimu imeweza kusisitizwa. Na Ijumaa ya tarehe 17 Januari 2020 alipokutana na uwakilishi wa kiekumene wa Kanisa la Kilutheri la Finland, Papa Francisko alisisiza juu ya suala la ukarimu akisema kwamba ni sehemu ya pamoja ya kushuhudia imani yetu.

Matunda ya Ukarimu ni kubarikiwa na Mungu

Somo linalotuongoza katika wiki ya kuombea umoja wa wakristo ulimwenguni ni mwendelezo wa mafundisho ya katekesi ya Papa Francisko. Ukarimu ulioonyeshwa na watu wa Malta kwa kundi la Mtume Paulo ulikuwa wa kipekee sana ambapo Papa Francisko Jumatano tarehe 15 Januari 2020 alitumia nafasi hiyo kuomba waamini wote kuiga ukarimu huo. Mtume Paulo alipowasili katika kisiwa cha Malta akiwa na majeruhi wa merikebu, wenyeji waliwapokea vizuri na kuwapatia huduma zilizokuwa zinastahili wakati huo, mfano kuwawashia moto manusuru hao ili kuwapa joto la faraja, pamoja na kuwapa mahitaji mengine ya msingi. Ukarimu wa wenyeji wa Malta unamsukuma Paulo mfuasi wa kweli wa Kristo pia kutumia nguvu zake katika kuongeza kuni ili moto uendelee kuwaka. Wakati akiendelea kukusanya kuni hizo anaumwa na nyoka lakini haikuweza kumdhuru.

Tukio la kuumwa nyoka Paulo bila kudhurika

Tukio hilo la kuumwa na nyoka Mtume Paulo linatukumbusha ahadi ya Kristo; “Mtashika nyoka mikononi na hata kama mtakunywa sumu hamtadhurika; mtawawekea juu mikono yenu na hawa watapona” (Mk 16,18). Papa Francisko alibainisha kuwa, kufuatia historia hiyo, inasemekana kwamba tangu wakati huo nchini Malta hakuna nyoka. Hii ni baraka ya Mungu anayowatunuku watu wakarimu. Tafakari yetu ya Neno la Mungu itakayotuongoza kwa siku nane hizi katika maadhimisho ya kidini ya kuombea umoja wa wakristo imejikita kwenye mada kuu ya somo hilo. Tumwombe Mungu Roho Mtakatifu atufungue mioyo yetu ili tafakari yetu iweze kuzaa matunda na umoja wetu uweze kudhihirika wazi na Mungu aweze kupewa sifa kupitia matendo yetu.


Maoni


Ingia utoe maoni