Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kulihamasisha Kanisa kutoka huko lilikojificha na kuwaendea watu wanaoishi pembezoni mwa jamii kutokana na hali yao ya maisha, ili wao pia waweze kuonja huruma, upendo na mshikamano unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa. Mwelekeo huu unajionesha katika maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko ambaye amekwisha kufanya hija za kitume kadhaa Barani Asia ili kuwaimarisha ndugu zake katika Kristo kwa kuwaonjesha huruma, upendo na mshikamano unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake! Baba Mtakatifu Francisko ameridhia uamuzi wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu wa kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha “Redemptoris Mater kwa ajili ya Bara la Asia”, kitakachokuwa na makao yake makuu huko Macau, Magharibi mwa mji wa Hong Kong, nchini China. Chuo hiki kitaanza kufanya kazi mwezi Septemba 2019 kwa kuwapokea wanafunzi kutoka sehemu mbali mbali za dunia.
Hili ni jibu makini kwa changamoto iliyotolewa na Mtakatifu Yohane Paulo II, aliyeonesha kwamba, Bara la Asia linapaswa kupewa msukumo wa pekee katika mchakato wa uinjilishaji. Kwa upande wake, Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume, “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili” analihamasisha Kanisa kutoka kifua mbele kwenda kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa. Malezi na majiundo ya Majandokasisi yataendelea kuzingatia kanuni na taratibu za Jumuiya ya Njia ya Ukatekumeni Mpya. Lengo ni kukuza na kudumisha ari na mwamko wa kimisionari, tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, Mkombozi wa Ulimwengu, aliyeteswa, akafa na kufufuka kutoka kwa wafu!
Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu akizungumzia kuhusu kuanzishwa kwa Chuo Kikuu cha “Redemptoris Mater" kwa ajili ya Bara la Asia”, anasema haya ni matunda ya ubunifu wa kitume unaojikita katika mchakato wa uinjilishaji kwa kuendelea kusoma alama za nyakati. Kuna njia mbali mbali ambazo Mama Kanisa katika maisha, historia na utume wake, amekuwa akizitumia kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, Barani Asia. Tangu mwanzo mashirika ya kitawa na kazi za kitume yalijifunga kibwebwe katika mchakato wa uinjilishaji wa awali na baadaye, wakafuata Mapadre wa zawadi ya imani “Fidei donum” pamoja na ushirikiano kati ya majimbo mbali mbali duniani.
Kardinali Filoni anasema, huu ni wakati wa kujikita katika majiundo na malezi makini kwa ajili ya mihimili ya uinjilishaji Barani Asia. Chuo hiki ni matunda ya changamoto iliyotolewa na Mtakatifu Yohane Paulo II aliyeona na kugundua changamoto changamani za Bara la Asia mintarafu uinjilishaji na utamadunisho, ili kweli imani ya Kristo Yesu na Kanisa lake, iweze kugusa na kutakasa baadhi ya tamaduni zinazosingana na tunu msingi za Kiinjili na utu wema. Bara la Asia limebahatika kuwa na tamaduni, lugha, mila na desturi mbali mbali ambazo zinapaswa kuzingatiwa katika mchakato mzima wa uinjilishaji na utamadunisho.
Lakini, ikumbukwe kwamba, Habari Njema ya Wokovu ni kwa ajili ya watu wote. Wazo la kujenga Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbanian lilitolewa na Papa Urbano VIII kunako mwaka 1627, ili kusaidia malezi na majiundo ya majando kasisi katika nyanja ya falsafa, taalimungu na maisha ya kiroho, ili wakisha kufuzu masomo yao, warejee nchini mwao, tayari kushiriki kikamilifu katika mchakato wa uinjilishaji. Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbanian, bado kipo na kinaendelea kusongesha libeneke la majiundo kwa majandokasisi na mapadre kutoka katika nchi za kimisionari duniani. Baba Mtakatifu Francisko ameamua kuivalia njuga changamoto ya uinjilishaji Barani Asia, kwa kulitaka Kanisa kutoka na kuwaendea watu kwenye viunga vya maisha na vipaumbele vyao.
Hiki ni kipindi cha Kanisa kutoka na kwenda kuinjilisha badala ya kukaa na kuanza kujitafuta lenyewe! Huu ni wakati wa kugawanya dhamana na majukumu kwa kuyawezesha Makanisa mahalia kushiriki kikamilifu katika malezi na majiundo ya mihimili ya uinjilishaji sehemu mbali mbali za dunia anasema Kardinali Fernando Filoni. Jumuiya ya Njia ya Ukatekumeni Mpya ikaonesha na kutangaza nia ya kusaidia malezi na majiundo ya mihimili ya uinjilishaji Barani Asia na Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu likaridhia nia hii njema na hatimaye, kupata kibali na baraka kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko. Hata hivyo, Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu kisheria, ndiye mhusika mkuu wa Chuo hiki na kwamba, ni Baraza ambalo lina uzoefu mkubwa katika malezi, makuzi na majiundo ya majandokasisi na wakleri kutoka Barani Asia. Kumbe, Chuo Kikuu cha “Redemptoris Mater kwa ajili ya Bara la Asia” kinapania kusaidia mchakato wa uinjilishaji Barani Asia.
Jimbo Katoliki la Macau lina historia na utajiri mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa, historia ambayo inapata chimbuko lake kunako mwaka 1576 na utume wake ulienea: China, Japan na Vietnam. Kimsingi Jimbo Katoliki la Macau ni kitovu cha malezi na uinjilishaji wa awali Barani Asia. Askofu Stephen Lee Bung-sang, baada ya kushauriana na mapadre wake, Jimbo likaridhia kuwa mwenyeji wa Chuo hiki. Huu ni mwanzo wa utekelezaji wa changamoto kama hizi katika Mabara mengine. Ikumbukwe kwamba, Chuo Kikuu cha Kipapa Cha Urbanian kina jumla ya wanafunzi 170 kutoka Asia na Afrika. Jumuiya ya Njia ya Ukatekumeni Mpya ni ubunifu wa kitume ambao umeridhiwa na Baba Mtakatifu Francisko kama msaada mkubwa kwa Makanisa mahalia katika mchakato wa malezi na majiundo ya mihimili ya Uinjilishaji.
Kwa kuingizwa katika majimbo mbali mbali, mapadre hawa wataweza pia kujifunza: lugha, mazingira, mila na tamaduni za watu mahalia kwa urahisi zaidi. Baba Mtakatifu Francisko ameridhishwa sana na mwelekeo huu katika maisha na utume wa Kanisa. Hii ni chachu ya kutoka kimasomaso kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu hadi miisho ya dunia. Pengine, wengi walizoea kuwasikia wamisionari kutoka katika Mashirika kama ya Wadominikani, Wayeusuit na Wafranciskani, wakiwa mstari wa mbele kuchakarika kutangaza na kushuhudia Injili, lakini wakati huu ni uzoefu wa Jumuiya ya Njia ya Ukatekumeni Mpya inayoshirikisha amana na utajiri wake katika maisha na utume wa Kanisa katika mchakato wa uinjilishaji Barani Asia.
Maoni
Ingia utoe maoni