Ilikuwa ni tarehe 1 Novemba 1950, Baba Mtakatifu Pio wa kumi na mbili katika Waraka wake wa kitume “Munificentimus Deus” yaani “Mungu Mkarimu” alipotangaza kuwa fundisho la imani kwamba “Bikira Maria, Mama wa Mungu ambaye daima ni Bikira, amepalizwa mbinguni mwili na roho baada ya kuhitimisha safari yake ya hapa duniani”. Hii ilitokana na sababu kwamba tangu mwanzo kabisa, Kanisa limekuwa linamwadhimisha Mama Bikira Maria kama Eva mpya huku akihusianishwa na Adam mpya, mwanaye Bwana wetu Yesu Kristo. Katika tamko hili tunaambiwa kwamba Bikira Maria, anashiriki kikamilifu, uzima wa milele na Mwanae mpendwa Kristo Yesu, lengo ambalo sote tunatarajia. Tunaambiwa kuwa sherehe hii inaunganisha sherehe zote za Bikira Maria kadiri ya mapokeo ya Kanisa Katoliki. Katika masomo yetu ya leo tunaona mwanga kuhusu kinachoadhimishwa leo – mwanamke aliyevikwa jua na mwezi chini ya miguu yake na taji ya nyota 12 .... ule uzao wake unabeba utukufu na uzima wa milele. Huyu mtoto ni masiha, Yesu Kristo. Hakuna mwingine ye yote mwenye sifa kama hizo na huyo Mama ni Bikira Maria. Huku kuondoka kwake katika mazingira ya ajabu na kwenda jangwani ila mahali penye utukufu na palipoandaliwa panaelezwa kama kupalizwa kwake mbinguni.
Pia tunasikia katika masomo ya leo hitaji la mama aina ya Bikira Maria na tunapata habari ya uwezekano wa kupalizwa mbinguni. Na jambo hili tukufu linawezekana kwa njia ya ufufuko wa Kristo mwenyewe. Katika Kristo vyote vinapata uzima tena, lakini kwa mpangilio - Kristo kwanza halafu atakapokuja tena, wote walio wake. Kanisa linaamini kwamba Bikira Maria, ambaye ni Mama wa Kristo kwa namna ya pekee, tayari ameshapata utukufu huo. Na ndiyo sikukuu yetu ya leo. Kwa kupalizwa mbinguni Bikira Maria – tunatafakari yule ambaye kwa upendeleo wake Mungu, alipendelewa kushiriki mwili na roho, utukufu wa ushindi wa Kristo. Tunaambiwa katika fundisho la Kanisa Katoliki kuwa, baada ya maisha yake hapa duniani, Bikira Maria alichukuliwa mwili na roho katika utukufu wa mbingu na akitawazwa na Kristo kama Malkia juu ya vitu vyote, ili aungane zaidi na Mwanae – Ufu. 19,6 na kushinda kabisa dhambi na kifo – Mwanga wa Mataifa (LG. 59). Kupalizwa Mbinguni Bikira Maria huthibitisha utukufu wa mwili na mpango wa Mungu kuhusu mwanadamu. Unamwajibisha mwanaume na mwanamke kuhusu hatima ya maisha yake kimwili na kiimani. Hutualika kutafakari sana fumbo la ukombozi kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Nafasi ya Maria ni ya pekee katika ukombozi na wokovu wa mwanadamu. Angalia aliyosema Maria na kilichotokea pale Kana – fanyeni yote atakayowaambia – Yoh. 2,5.
Katika Injili tunaona jinsi ambavyo tokea mwanzo Mungu Baba kwa njia ya Kanisa, anavyomtumia Bikira Maria. Vizazi vyote vitamwita mbarikiwa. Angalia unyenyekevu wa Maria – moyo wangu wamtukuza Bwana na roho yangu inashangilia katika Mungu mwokozi wangu......Kwa njia ya Kristo na pamoja na Mama Bikira Maria, tunaona uwezekano wa kufika mbinguni. Muungano wa utukufu na Bwana wetu ndiyo lengo letu. Bikira Maria tayari anashiriki utukufu huo. Nasi tunaitwa kuishi katika sasa na Mungu ili kuupata huo uzima wa milele. Ndiyo matumaini yetu na ndicho tunachosherehekea leo. Baada ya kupata habari kuwa atakuwa mama wa Mungu, Maria anaharakisha kwenda kwa Elizabeti. Mwinjili atuonesha unyenyekevu wa Maria, anaacha njia yake, maisha yake na kufuata sauti ya Mungu. Mt. Ambrose – katika Expos. Evang. Sec. Lucam, ii, 19: PL 15, 1560 – akiandika kuhusu hii haraka ya Maria, anasema huonesha kuwa neema ya Mungu kwa njia ya Roho wake haihitaji kusitasita. Lile itikio lake, Mimi ni Mtumishi wa Bwana linamuwajibisha na baadaye inaonekana wazi katika uhusiano wake na Mwanae. Wajibu huo anautimiza kwa uaminifu na kuukamilisha bila kusita. Daima Maria anamfuata Mwanae na hii inaonesha pia jinsi alivyojiandaa kutoka chini kwenda juu – Mwanga wa Mataifa (LG, 64-65).
Kupalizwa mbinguni kwake Bikira Maria kunaonesha kuwa maisha ya mkristo ni safari ya ufuasi, kumfuata Kristo, safari ambayo mwisho wake unajulikana hata kwa akili, mwisho ambao unafahamika kuwa ni ushindi mkamilifu dhidi ya dhambi na kifo na kuwa na uhusiano mkamilifu na Mungu. Katika Efe. 2:6 Mt. Paulo anaandika – Mungu ametukweza pamoja na Kristo na kutuketisha pamoja naye katika utukufu katika Kristo Bwana. Tunasherehekea ushindi huu wa imani, wa safari ya imani – Yoh. 14; 2-3 – nyumbani mwa Baba yangu mna makao mengi. Kama sivyo, je, ningaliwaambia kwamba nina kwenda kuwatengenezea mahali? Baada ya kwenda na kuwatengenezea mahali nitakuja tena niwachukue kwangu, mpate kuwapo nilipo mimi. Ndugu wapendwa, maisha yetu na Mungu huanza na sakramenti ya ubatizo. Maisha yetu hapa duniani kama tuonavyo katika masomo yetu ya leo yatupa nafasi ya kujua mapenzi na mpango wa Mungu wa ukombozi. Mtakatifu Agustino anapoongea kuhusu falsafa ya historia, yaani maana ya kweli ya historia, anaongea vizuri sana kuhusu huu mpango wa Mungu wa ukombozi. Anasema chanzo chake ni Mungu kwa njia ya Mwanae na Roho Mtakatifu. Anasema wazi kuwa sisi sote tutasalimika tu kama tutabaki katika mduara huu ambao chanzo ni Mungu na hukamilika kwake Mungu mwenyewe.
Tukitoka nje ya mduara huu basi tumekwisha. Katika kuishi mpango huu wa Mungu, Bikira Maria anakuwa nyota yetu ya kutuongoza kwake Mwanae, jua liangazalo vivuli vyote na kutupatia matumaini. Tunasoma hayo katika waraka wa Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI – Spe Salvi (katika matumaini tumekombolewa) no. 49. Mtume Paulo katika barua yake kwa Rum. 8:24 anaandika hivi; ni matumaini yanayotusalimisha. Lakini matumaini tunayoyaona yametekelezwa, si tena matumaini. Inawezekanaje kutumainia kitu tunachokiona kimekwisha kuwepo? Kanisa linaamini kwamba Bikira Maria, ambaye ni mama wa Kristo kwa namna ya pekee, tayari ameshapata utukufu huo kwa sababu aliishi hayo matumaini. Na ndiyo maana ya adhimisho la sherehe yetu ya leo. Sisi katika matumaini tumekombolewa. Tumsifu Yesu Kristo na Bikira Maria aliyepalizwa Mbinguni mwili na roho!
Maoni
Ingia utoe maoni