Baba Mtakatifu Francisko anawataka watawa kuwa wasikivu, wadadisi na wagunduzi, daima wakitambua kwamba, wao ni sehemu muhimu sana ya maisha na utume wa Kanisa. Kumbe, wanapaswa kushiriki katika sera na mikakati ya shughuli za kichungaji katika Makanisa mahalia, wakitambua kwamba, wao pia ni sehemu ya Familia ya Mungu inayosafiri kuelekea katika utimilifu na utakatifu wa maisha. Hapa watawa wanahamasishwa kuwa kweli ni waaminifu kwa Mungu na Kanisa. Katika maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa mbinguni mwili na roho, ndani ya Kanisa kuna utamaduni na Mapokeo ya watawa kufunga nadhiri zao za mwanzo na daima, sanjari na maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25, 50 na wale waliobahatika ni miaka 75. Maadhimisho yote haya ni nafasi ya kuangalia fursa, changamoto na matatizo yaliyopo ili yaweze kufanyiwa kazi kwa kujikita katika ari na mwamko wa kimissionari, tayari kuwatangazia watu wa Mataifa furaha ya Injili inayojikita katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko.
Ni katika muktadha huu, leo Vatican Radio inapenda kukushirikisha wosia uliotolewa na Askofu Msaidizi Eusebius Nzigilwa wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, katika maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Miaka 150 tangu alipofariki dunia Mtakatifu Maria De Mattias muasisi wa Shirika la Masista Waabuduo Damu Takatifu y. Maadhimisho haya yalifanyika kwenye Parokia ya Mtakatifu Gaspar del Bufalo na Kituo cha hija, Jimbo kuu la Dar es Salaam. Katika mahubiri yake, Askofu Msaidizi Nzigilwa alifafanua maana ya nadhiri za muda na zile za daima; umuhimu wa maisha ya kitawa ndani ya Kanisa pamoja na changamoto wanazokumbana nazo katika kutekeleza utume wao miongoni mwa watu wa Mungu. Anasema, mchango wa watawa katika sekta ya elimu, afya, ustawi na maendeleo fungamani ya jamii ni mkubwa sana. Hii ni huduma inayotolewa kama kielelezo cha upendo unaobubujika kutoka katika karama za Mashirika haya ambazo kimsingi ni zawadi ya Roho Mtakatifu kwa ajili ya Kanisa.
Anawaalika waamini walei kuwasaidia watawa na mapadre kutekeleza vyema dhamana, wajibu na wito wao katika maisha na utume wa Kanisa. Askofu Msaidizi Nzigilwa anakaza kusema, utume wao si lele mama, wanakabiliwa na magumu katika maisha, lakini ikumbukwe kwamba, lengo kuu ni huduma na sadaka kwa ajili ya watu wa Mungu. Mwaliko kwa watawa ni kuhakikisha kwamba, maisha na utume wao, unakita mizizi yake katika upendo wa kisadaka. Kamwe wasikubali kutumbukia katika kishawishi cha uchu wa mali na madaraka na kwamba, mafanikio katika maisha na utume wao kama watawa na mapadre hautegemei hata kidogo wingi wa fedha na mali walizo nazo. Askofu Msaidizi Eusebius Nzigilwa anasema, Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 14 Agosti, anafanya kumbu kumbu ya Mtakatifu Maximiliani Maria Kolbe, Padre na Mfia dini. Ni Padre aliyependa kwa dhati, akalimwilisha pendo hili kwa matendo na katika ukweli kama Padre na shahidi wa mwanga angavu wa imani inayomwilishwa katika matendo.
Ni shahidi aliyeongozwa na Mwanga wa Kristo Mfufuka, kiasi cha kuyatoa maisha yake kwa ajili ya Mungu na jirani. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kichungaji Lumen Fidei, Mwanga wa Imani anasema, huu ni mwanga wenye nguvu na uwezo wa kumwangazia mwanadamu katika maisha yake yote, kwani ni Mwanga unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu, aliye hai, Mungu ambaye ni upendo mkalimifu, unao mchangamotisha mwamini kujenga maisha thabiti katika matendo kama kielelezo cha imani pamoja na kujiaminisha kwa Kristo Yesu aliyeyamimina maisha yake kwa ajili ya kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, kielelezo cha hali ya juu kabisa cha upendo wa Mungu kwa binadamu. Mtakatifu Maximilian Maria Kolbe alizaliwa kunako mwaka 1894, akajiunga na Shirika la Ndugu Wadogo wa Mtakatifu Francisko kama mtawa. Akakuza na kuimarisha Ibada kwa Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa, kiasi hata cha kuanzisha "Jeshi la Bikira Maria".
Ni Padre aliyetekeleza utume wake kwa njia ya mahubiri ya kina yaliyokuwa yanabubujika kutoka katika Neno la Mungu. Alikuwa ni mwandishi mahiri aliyetumia taaluma yake kuendeza Habari Njema ya Wokovu na Kweli za Kiinjili. Alionesha ari na mwamko mkubwa wa shughuli za kimissionari Barani Ulaya na Asia. Wakati wa madhulumu ya Kinazi, alitupwa kizuizini na kuonja mateso na madhulumu ya utawala wa kinazi kwenye kambi ya mateso ya Auschwitz, wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Akiwa gerezani akaamua kutoa sadaka ya maisha yake kama Padre ili kuokoa maisha ya Baba wa familia, aliyekuwa mwenza pale gerezani, ushuhuda wa hali ya juu wa imani inayomwilishwa katika matendo. Akafariki dunia kwa njaa hapo tarehe 14 Agosti 1945. Mtakatifu Yohane Paulo II wakati akielezea sifa za Mtakatifu Maximilian Maria Kolbe alisema kwamba, ni msimamizi wa hali tete katika karne hii. Mama Kanisa anapofanya kumbu kumbu ya Mtakatifu Maximilian Maria Kolbe anapenda kuweka mbele ya macho ya waamini matatizo na changamoto zinazoendelea kumwandama mwanadamu katika nyakati hizi za utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia.
Licha ya maendeleo makubwa katika sayansi na teknolojia, lakini kutokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na matatizo pamoja na mahangaiko ya wengine, kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko, kuna mamillioni ya watu wanaoteseka kutokana na balaa la njaa na utapiamlo duniani. Uchu wa mali na madaraka ni kati ya mambo ambayo yameendelea kusababisha vita na madhulumu kwa watu wasiokuwa na hatia, changamoto ya kusimama kidete kulinda na kutetea misingi ya haki, amani na upatanisho wa kweli unaojikita katika toba na wongofu wa ndani. Mtakatifu Maximilian Maria Kolbe kwa ushuhuda wa maisha yake ni mwaliko kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuthamini tunu ya uhai ambayo ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu na kwamba, waamini wajitahidi kujiandaa kwa ajili ya kukabiliana na Fumbo la Kifo kwa: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu linalomwilishwa katika matendo ya huruma. Watawa wanakabiliwa na changamoto mbali mbali, ikiwa ni pamoja na kupungua kwa idadi ya miito na ongezeko la wazee na wagonjwa katika Mashirika.
Hapa watawa hawana sababu ya kukata wala kukatishwa tamaa, bali wanapaswa kuwa ni mashuhuda na manabii wa nyakati hizi, tayari kuyaangazia maisha ya mwanadamu kwa sasa na kesho iliyo bora zaidi, dhamana inayotekelezwa kwa njia ya huduma makini. Mashirika haya yanahamasishwa zaidi na zaidi kujikita katika majiundo na malezi endelevu kwa ajili ya watawa ili kuweza kuimarisha hali ya miito inayoendelea kulega lega siku hadi siku na hivyo kusababisha watawa wengi kutoona tena thamani ya maisha na wito wao wa kitawa na hivyo kuamua kuachia ngazi! Inasikitisha kuona kwamba, hata wale ambao wameishi kwa miaka mingi katika utawa wanaanza kukata tamaa na kuondoka. Askofu Msaidizi Eusebius Nzigilwa anasema, hakuna jambo kubwa linalowasikitisha Maaskofu kuona watawa ambao wamejisadaka kwa miaka mingi kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani, wakihangaika tena na mchakato wa kutaka kufunguliwa nadhiri zao, ili “waishie mitaani”.
Baraza la Kipapa kwa ajili ya Mashirika ya Kitawa na Kazi za Kitume linasema idadi kubwa ya watawa wa kiume na kike wanaoacha utawa ni dalili za mtikisiko wa maisha ya kitawa ndani ya Kanisa. Haya ni matokeo ya myumbo wa tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; imani, maadili na utu wema. Haya ni matokeo ya utandawazi yanayojionesha hata ndani ya Kanisa, kwa sababu watawa ni watu waliochaguliwa kutoka katika jamii kwa ajili ya mambo ya Kimungu, lakini bado wanaendelea kubakia na ubinadamu wao uliojeruhiwa kwa dhambi ya asili. Baadhi ya mambo yanayochangia kasi kubwa ya watawa na mapadre kuacha wito na maisha ya: Mosi ni ukavu wa maisha ya kiroho. Watawa na Mapadre wanajikuta hawana tena hamu ya kusali, kutafakari wala kushiriki Sakramenti za Kanisa zinazowakirimia neema na baraka katika maisha na wito wao. Sala za binafsi na zile za Kijumuiya hazina nafasi tena, pengine kwa kisingizio cha kuelemewa mno na kazi za kitume!
Hizi ni dalili za kumong’onyoka kwa tunu msingi za maisha ya kiroho na kiimani na matokeo yake kuitema zawadi ya utawa na upadre, waliyoipokea kwa shangwe na nderemo wakati walipokuwa wanaweka nadhiri au kupadrishwa. Katika hija ya maisha ya kitawa na kipadre, baadhi yao hupoteza utambulisho wao kwa Jumuiya, Shirika na hata wakati mwingine kwa Kanisa lenyewe. Dalili zake ni watu kutoridhika na maisha ya kijumuiya, kinzani, migogoro na hali ya kudhaniana vibaya. Ubaguzi na upendeleo unaofanywa na baadhi ya viongozi wa Mashirika na Jumuiya za Kitawa, ni mambo yanayochangia kuwafanya baadhi ya watawa na mapadre kutoshiriki kikamilifu katika maisha ya kijumuiya kwa kutindikiwa uwiano makini kati ya maisha ya mtu binafsi na yale ya kijumuiya au kishirika. Matokeo yake, watu hawa watatafuta fursa hizi nje ya jumuiya na mashirika yao, mwanzo wa kuchanganyikiwa na kuanza pole pole kupoteza dira na mwelekeo wa maisha ya kitawa na kipadre.
Maoni
Ingia utoe maoni