Katika maadhimisho ya Sherehe ya Bikira Maria Kupalizwa Mbinguni, mwili na roho, tarehe 15 Agosti 2019, Baba Mtakatifu Francisko ameridhia ombi la Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam, Tanzania la kung’atuka kutoka madarakani. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu Francisko amemteua Askofu mkuu mwandamizi Yuda Thaddeus Ruwa’ichiwa Jimbo kuu la Dar es Salaam, kuanzia sasa kuwa ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam. Hivi karibuni, Kardinali Polycarp Pengo katika maadhimisho ya kumbu kumbu ya Miaka 75 tangu kuzaliwa kwake, aliwaambia watu wa Mungu Jimbo kuu la Dar es Salaam kwamba, anasubiria wakati wowote kumtii Baba Mtakatifu Francisko atakapomwambia kupumzika katika utume wa Kiaskofu.
Anasubiria pia kumtii Mwenyezi Mungu mwingi wa huruma na mapendo, wakati wowote atakapomwita na kumwambia kupumzika katika usingizi wa amani na maisha ya uzima wa milele. Kardinali Polycarp Pengo amewaambia watu wa Mungu kwamba, kaburi lake liko pale Pugu, kwenye Kituo cha Hija, mahali ambapo wamelala mashuhuda wa imani na uinjilishaji nchini Tanzania. Amekaza kusema, Yeye ana amini katika utii, kama alivyoambiwa kwamba, baada ya Daraja Takatifu, angeteuliwa kuwa Katibu wa Askofu Jimbo Katoliki la Sumbawanga. Baada ya miaka miwili, akatumwa kwenda Roma kwa ajili ya kujiendeleza kwa masomo ya juu katika masuala ya maadili. Aliporejea nchini Tanzania, mwaka 1977 akapangiwa kufundisha Seminari kuu ya Kipalapala, iliyoko Jimbo kuu la Tabora.
Baadhi ya wanafunzi wake ni Askofu mkuu Yuda Thaddeus Ruwaichi ambaye sasa ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam pamoja na Askofu Almachius Vincent Rweyongeza wa Jimbo Katoliki Kayanga. Kunako mwaka 1978 akaitwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania na kuambiwa kwamba, ameteuliwa kuwa Gombera na muasisi wa Seminari kuu ya Segerea, iliyoko Jimbo kuu la Dar es Salaam na hapo akaendelea kuwahudumiwa watu wa Mungu nchini Tanzania katika malezi na majiundo ya majandokasisi hadi mwaka 1984. Kardinali Polycarp Pengo kwa unyenyekevu mkubwa anasema, hajawahi kuwa kiongozi seminarini, anakumbuka tu kwamba, akiwa Kaengesa alikuwa ni kiranja msaidizi, lakini hajui ni kwa sababu gani ambazo Mwenyezi Mungu amemteua kuwa ni Kiongozi wa Kanisa, kiasi cha kuwafundisha, kuwaongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu kama Kasisi, Askofu na hatimaye kama Kardinali.
Kardinali Polycarp Pengo anakiri kwamba, yeye si mpenzi sana wa michezo. Kardinali Polycarp Pengo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo kuu la Dar es Salaam anapenda kumwimbia Mwenyezi Mungu utenzi wa sifa, shukrani, enzi na utukufu kwa matendo makuu aliyomtendea katika maisha yake na kupitia kwake pamoja na waandamizi wake wote wameweza kufanya yale yaliyofanyika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu ndani na nje ya Tanzania. Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Afrika na Madagascar, SECAM itamkumbuka sana Kardinali Pengo kwa kuwa kuwa ni daraja na kiungo muhimu sana cha Kanisa Barani Afrika wakati SECAM ilipokuwa inachechemea kwa changamoto mbali mbali katika maisha na utume wa Kanisa Barani Afrika.
Maoni
Ingia utoe maoni