Kardinali Giovanni Angelo Becciu, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu, Jumamosi tarehe 22 Juni 2019 kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumtangaza Mtumishi wa Mungu Sr. Maria Carmen Lacaba Andía pamoja na watawa wenzake 13 wa Shirika la Wafranciskani wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili kuwa wenyeheri. Hawa ni watawa waliouwawa kikatili kutokana na chuki dhidi ya imani (Odium fidei) huko Madrid, nchini Hispania kati ya mwaka 1936 hadi mwaka 1939; wakati wa vita ya wenyewe kwa wenyewe nchini Hispania.
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Sala ya Malaika wa Bwana, amewakumbuka watawa hawa wa ndani; Mabikira wenye busara, waliomngoja Bwana harusi wa mbinguni kwa imani thabiti. Kifodini chao ni mwaliko kwa waamini wote kuwa imara na wadumifu, hasa wakati wa majaribio katika maisha! Itakumbukwa kwamba, hata Wakristo nchini Mexico na Urussi, walijikuta wakikabiliana na dhuluma pamoja na mauaji ya kikatili. Watawa waliouwawa, wengi wao walikuwa bado ni vijana wabichi kabisa na wengine, walikwisha kukomaa katika sadaka na majitoleo kwa Mungu na jirani. Moyo wa mwanadamu, utaendelea kubaki kuwa ni fumbo la maisha.
Watawa wakaonesha unyenyekevu, wakatoa msamaha na kujikabidhi kwa watesi wao! Ni watawa ambao walikita maisha yao katika: Sala, Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa zilizowajalia ukomavu wa imani, kiasi hata wakawa tayari kukabiliana na kifo cha kikatili kiasi hiki! Amana na ushuhuda endelevu wa wafiadini hawa ni moyo wa kusamehe kama alivyofanya Kristo Yesu, bila kutaka kulipiza kisasi, changamoto endelevu hata katika ulimwengu mamboleo, ambamo watu wanauana kwa kulipizana kisasi! Ushindi unapatikana kwa njia ya msamaha na wala si vinginevyo kama Kristo Yesu anavyofundisha kwenye Sala ya Baba Yetu, Sala ya Bwana, kwa kujiaminisha kwa ulinzi na tunza ya Baba wa milele, hata katika shida, magumu na changamoto za maisha. Wakati mwingine, waamini wanapaswa kujifunza kukaa kimya, ili Mwenyezi Mungu aweze kuzungumza nao kutoka katika undani wa maisha yao!
Kardinali Giovanni Angelo Becciu katika mahubiri yake amekaza kusema, wafiadini hawa ni watu ambao katika maisha yao, wamemwilisha maneno ya Mtume Paulo ambaye anasema “Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, ufidhuli, na misiba, na adha, na shida kwa ajili ya Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu”. 2 Kor. 12: 10. Ni watawa ambao wamekuwa na imani thabiti wala hawakuteteleka kwa madhulumu, kiasi hata cha kuwa tayari kutangaza na kushuhudia ukweli kwa kuyamimina maisha yao, huku wakiyahusianisha maisha yao na yale ya Kristo Yesu. Huu ushuhuda wa imani, matumaini na mapendo! Mashuhuda hawa waliteswa na hatimaye kuuwawa kikatili kutokana na imani yao kwa Kristo Yesu, Kanisa na maisha ya kitawa kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani!
Ni mashuhuda wa imani waliotoa kipaumbele cha kwanza kwa ajili ya ufalme wa Mungu, haki na amani duniani, kiasi hata cha kufanikiwa kuonja wema na huruma ya Mungu katika maisha yao. Kwa hakika, anasema Kardinali Becciu, watawa hawa walijiandaa kukabiliana na kifo kwa moyo thabiti na ujasiri, wakitambua kwamba, walikuwa wanayamimina maisha yao kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake! Waliuwawa wakiwa wanamwimbia Yesu Kristo Mfalme, utenzi wa sifa na shukrani! Walipoulizwa na watesi wao, Je, jeuri hii walikuwa wanaitoa wapi? Wao wakajibu kwa ushupavu wakisema, hii ilikuwa ni neema ya Mungu, iliyowawezesha hata kusamehe na kusahau kama alivyofanya Kristo Yesu pale Msalabani! Huu ni ushuhuda wa waamini wanajisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutekeleza mpango wa Mungu katika maisha yao, kwa ajili ya wokovu wa walimwengu.
Ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Kristo Yesu kwa waja wake, changamoto na mwaliko kwa waamini kuendelea kuwa waaminifu kwa Kristo na Kanisa lake, kila mtu kadiri ya wito na utume wake ndani ya Kanisa. Kwa waamini walei, wajenge utamaduni wa kusikiliza, kutafakari na hatimaye, kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao, chemchemi ya ukuhani, unabii na ufalme, unaobubujika kutoka katika Sakramenti ya Ubatizo! Walei wanahamasishwa kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko! Imani, matumaini na mapendo ni fadhila ambazo zimedhihirisha kuwa na nguvu kubwa zaidi kuliko vita, chuki na uhasama. Hawa ni mashuhuda wa imani ambao wameandamana na Kristo Yesu katika hija ya maisha hadi kifodini; kielelezo cha nguvu ya Fumbo la Pasaka, yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu!
Hili ni fumbo ambalo ni endelevu katika maisha na utume wa Kanisa, kwani damu ya mashahidi ni mbegu ya Ukristo kama ambavyo aliwahi kusema Tertullian “Sanguis martyrum semen christianorum”. Tunu msingi za maisha na wito wa Kikristo ni nyenzo msingi dhidi ya: uchoyo na ubinafsi; kutopea kwa imani; tabia ya ukatili dhidi ya maskini na wanyonge; tabia ya kutaka kusambaratisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia; tabia ya kukumbatia utamaduni wa kifo, dhidi ya Injili ya uhai. Neno la Mungu na Mafundisho msingi ya Kanisa hayana budi kuzama katika akili na nyoyo za watu, ili yaweze kushuhudiwa na wengi! Kardinali Giovanni Angelo Becciu anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, wanamwilisha tunu hizi msingi katika maisha na utume wao, ili kweli waweze kuwa ni mashuhuda amini wa Kristo Yesu na Kanisa lake.
Wakristo wawe ni mashuhuda na vyombo vya imani, matumaini, mapendo na furaha ya Injili; tayari kutangaza na kushuhudia upendo na huruma ya Mungu inayomwambata mwamini hadi dakika ya mwisho ya maisha yake! Kwa mfano wa ushuhuda na maombezi ya mashahidi wapya wa imani, familia ya Mungu nchini Hispania, iwe ni nguzo ya mwanga thabiti wa Injili inayomwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu kwa njia ya ujasiri na ushuhuda wa imani unaovuka kuta na kizani zote tayari kuwafungulia waamini mwono mpana zaidi wa matumaini na udugu wa kibinadamu!
Maoni
Ingia utoe maoni