Alhamisi. 21 Novemba. 2024
feature-top
Papa Francisko: Ekaristi Takatifu ni chemchemi ya baraka, neema, upendo, huruma na mshikamano kati ya watu wa Mungu, tayari kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Baba Mtakatifu Francisko katika maadhimisho ya Sherehe ya Ekaristi Takatifu, “Corpus Domini”, Jumapili, tarehe 23 Juni 2019 ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwenye Parokia ya Bikira Maria Mfariji, iliyoko katika kitongoji cha Casal Bertone nje kidogo ya Roma. Kardinali Angelo De Donatis, Makamu Askofu mkuu Jimbo kuu la Roma akaongoza Ibada ya Maandamano makubwa ya Ekaristi na hatimaye, Baba Mtakatifu Francisko akatoa baraka ya Ekaristi kwenye Uwanja wa michezo ulioko, pembeni mwa nyumba ya Serena inayotoa huduma kwa maskini na watu wanaosukumiziwa pembezoni mwa jamii.

Hii ni nyumba inayoongozwa na kusimamiwa na Wamisionari wa Upendo, maarufu kama Watawa wa Mama Theresa wa Calcutta! Baba Mtakatifu Francisko katika mahubiri yake amekazia umuhimu wa kusema na kutoa baraka, tema muhimu sana katika Sherehe ya Ekaristi Takatifu mintarafu Liturujia ya Neno la Mungu. Melkisedeki mfalme wa Salemu alimbariki Abramu na kwa njia yake, familia zote duniani zikapata baraka! Kristo Yesu, katika muujiza wa kuwalisha watu elfu tano, alitwaa mikate mitano na samaki wawili akavibariki, akavimega na akawapa wanafunzi wake ili wawaandikie mkutano. Muujiza huu ukawa ni chemchem ya baraka kwa watu wengi.

Baraka ni chemchemi ya huduma ya upendo kwa Mungu na jirani. Ni baraka inayobubujika kutoka katika Sakramenti za Kanisa na kwa namna ya pekee, Ekaristi Takatifu ni shule ya baraka kutoka kwa Mungu kwa ajili ya watoto wake, ili kuweza kusonga mbele katika imani, matumaini na mapendo. Baraka ni utenzi wa sifa, unaoganga na kuponya moyo uliovunjika na kupondeka, changamoto na mwaliko kwa waamini kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa baraka duniani! Baba Mtakatifu anawahimiza wakleri kuendelea kutoa baraka, kwani Mwenyezi Mungu anataka kuwapatia upendo, wema na faraja waja wake.

Kinyume cha baraka anasema Baba Mtakatifu ni laana, makelele, kiburi na uchungu wa moyo! Waamini wanaposhiriki kikamilifu Fumbo la Ekaristi Takatifu, wanaonja wema, huruma, upendo na msamaha unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu! Kwa hakika, waamini wanapenda kumsifu na kumtukuza Mungu. Kristo Yesu kwa njia ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, amekuwa ni mkate unaounda na kujenga Fumbo la Mwili wake, yaani Kanisa. Waamini wanahamasishwa kujifunza kubariki kile ambacho Mwenyezi Mungu amewakirimia katika maisha; waendelee kubariki yale yaliyopita katika historia ya maisha yao na kutoa maneno ya faraja kwa wengine badala ya kuwalaani!

Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, Melkisedeki mfalme wa Salemu, baada ya kumbariki, Abramu akampa fungu la kumi la vitu vyote! Yesu baada ya kubariki ile mikate na wale samaki wawili, akawapa Mitume wake, ili wawaandikie watu, chakula kinakuwa ni alama ya upendo na mshikamano wa dhati unaofumbatwa katika sala, baraka pamoja na kujiaminisha mbele ya Baba yake wa mbinguni, kiasi kwamba, watu wote wakala, wakashiba na kusaza vikapu kumi na viwili. Uchumi wa Kiinjili unafumbatwa kwa namna ya pekee katika umoja na mshikamano; kwa kurutubisha maisha ya walimwengu na kwa namna ya pekee kabisa, msamihati anaotumia Kristo Yesu ni ule wa kutoa, mwaliko wa kutoa baraka kwa njia ya huduma ya upendo kwa jirani, kama ambavyo Kristo Yesu aliwataka Mitume wake kuwalisha wale watu elfu tano!

Baba Mtakatifu anakaza kusema, jambo hili liliwashangaza sana. Yesu alikuwa anawaalika kumegeana na kushirikishana hata kile kidogo walichokuwa nacho kama chemchemi ya baraka. Muujiza wa kuwalisha watu elfu tano, ulitendeka katika hali ya unyenyekevu, upendo na huruma kwa watu waliokuwa na njaa! Ekaristi Takatifu ni chemchemi ya upendo unaobubujika kutoka kwa Mungu, changamoto kwa waamini ni kuwa watu wa Ekaristi, yaani tayari kujimega na kujisadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya jirani zao. Baba Mtakatifu anasema kwamba, Jiji la Roma lina kiu ya upendo na huduma!

Jiji la Roma, linateseka sana kutokana na uchafuzi mkubwa wa mazingira; kuna wazee wanaoteseka kutokana na upweke hasi; familia nyingi zinaogelea katika: umaskini, hali mbaya ya kiuchumi na ukata mkubwa na kwamba, kuna vijana wengi wasiokuwa na fursa za ajira, kiasi kwamba, wamepoteza ile ndoto ya maisha bora zaidi. Wote hawa wanahitaji majibu muafaka, yanayohitaji ushiriki na uwajibikaji wa kila mtu, kwa kugeuka kuwa ni Ekaristi inayowashirikisha watu katika hija ya maisha; chakula kilichoshuka kutoka mbinguni, kinachowalisha waja wake.

Kwa njia ya maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi takatifu, waamini wanaonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao. Wanasukumwa kwa namna ya pekee, kubariki na kupenda, kuanzia mahali pale walipo. Maandamano makubwa ya Ekaristi Takatifu katika sehemu mbali mbali za dunia ni alama ya baraka; chemchemi ya ujasiri ili hata wao waweze kuwa ni sehemu ya baraka na sadaka takatifu inayopendeza machoni pa Mungu!


Maoni


Ingia utoe maoni