Jumanne. 03 Desemba. 2024
feature-top
Baba Mtakatifu Francisko tarehe 24 Juni 2019 amekutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Australia wakati wa hija yao ya kitume mjini Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Jumatatu tarehe 24 Juni 2019 amekutana na kuzungumza na Baraza la Maaskofu Katoliki Australia linalofanya hija ya kitume, inayofanyika mjini Vatican walau kila baada ya miaka mitano. Hii ni fursa kwa Maaskofu kujadiliana na Baba Mtakatifu pamoja na waandamizi wake maisha na utume wa Kanisa mahalia; matatizo, changamoto na fursa zilizopo katika mchakato mzima wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Kanisa Katoliki nchini Australia, linaendelea kujikita katika majadiliano ya kidini na kiekumene ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu! Katika mazingira ya utandawazi, maendeleo ya sayansi na teknolojia, kumeanza kuibuka kundi kubwa la wakanimungu nchini Australia, changamoto inayohitaji mbinu mkakati wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko!

Kanisa Katoliki nchini Australia limekuwa ni mdau mkubwa wa: ustawi, maendeleo na mafao ya wengi nchini Australia hasa katika sekta ya elimu, afya na maendeleo fungamani. Taasisi zote zinazomilikiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki zimekuwa ni jukwaa la majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni. Kanisa limeendelea kujipambanua kwa huduma makini kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Baraza la Maaskofu Katoliki Australia limekuwa na mchango mkubwa katika kugharimia miradi mbali mbali ya huduma ya uinjilishaji katika nchi changa zaidi duniani. Takwimu zinaonesha kwamba, Shirika la Misaada la Kanisa Katoliki Australia, Caritas Australia katika kipindi cha mwaka 2017 limechangia huduma kwa watu zaidi ya milioni mbili.

Sera na mikakati ya shughuli za kichungaji nchini huko zinatoa kipaumbele cha pekee kwa wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum bila kuwasahau wananchi asilia wa Australia yaani Waaborigen. Maaskofu wako mstari wa mbele pia katika sera na mikakati ya utunzaji wa mazingira nyumba ya wote, kutokana na ukweli kwamba, mara nyingi familia ya Mungu nchini humo, imekuwa ikiathirika vibaya kutokana na majanga asilia kama vile: ajali za moto, ukame wa kutisha au mafuriko. Baraza la Maaskofu Katoliki Australia linabainisha kwamba, changamoto kubwa kwa wakati huu ni uinjilishaji mpya, kadiri ya sera na mikakati iliyobainishwa na Mtakatifu Yohane Paulo II katika Wosia wake wa Kitume, “Ecclesia in Oceania” yaani “Kanisa katika nchi za Oceania” uliotolewa kunako mwaka 2001.

Idadi ya waamini wa Kanisa Katoliki wanaohudhuria na kushiriki Ibada ya Misa Takatifu kikamilifu inaendelea kupungua kila kukicha! Hii inatokana na ukweli kwamba, kumekuwepo na upungufu mkubwa wa Mapadre nchini Australia na kwamba, shughuli nyingi za kitume zinaendeshwa na waamini walei, kama sehemu ya ushiriki wao katika maisha na utume wa Kanisa. Utamaduni wa kifo unaokumbatiwa na sera pamoja na mikakati ya utoaji mimba imechangia kwa kiasi kikubwa kuporomoka kwa idadi ya watoto wanaozaliwa nchini Australia. Kifo laini au (Eutanasia) pamoja na huduma ya kifo ni kati ya mambo yanayosigana na haki msingi za binadamu nchini Australia wanasema Maaskofu. Hii ni huduma ambayo inalindwa na sheria za nchi ambazo zimeanza kutumika rasmi tarehe 19 Juni 2019.

Hata katika changamoto hizi zote, Kanisa limeendelea kusimama kidete kulinda, kutetea na kuwahudumia kwa unyenyekevu na moyo mkuu wagonjwa waliokuwa kufani pamoja na kuhakikisha kwamba, hospitali, vituo vya afya na zahanati zinazoongozwa na kumilikiwa na Kanisa Katoliki zinazingatia kanuni, maadili, utu, heshima na haki msingi za binadamu kama zinavyofafanuliwa na Mafundisho Jamii ya Kanisa. Kumong’onyoka kwa maadili, utu wema pamoja na kushamiri kwa ukoloni wa kiitikadi, Australia imejikuta ikiridhia ndoa za watu wa jinsia moja, jambo ambalo Maaskofu nchini humo wanalipinga kwa nguvu zote kwani ni kinyume kabisa cha utu wema, maadili na kadiri ya mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu! Maaskofu wanakaza kusema, hakuna ndoa kati ya watu wa jinsia moja!

Ili kuweza kukabiliana na changamoto mamboleo, Baraza la Maaskofu Katoliki Australia linaendelea kukazia kwa namna ya pekee kabisa: Katekesi makini kuhusu: Imani, Sakramenti za Kanisa, Maisha Adili na Sala! Majiundo awali na endelevu kwa wakleri, watawa na waamini walei yanaendelea kupewa msukumo wa pekee kwa kukazia kanuni maadili, utu wema, ustawi, maendeleo na haki msingi za binadamu. Majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni ni muhimu sana katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu. Kanisa linaendelea na toba pamoja na wongofu wa ndani kama sehemu ya kujitakasa kutokana na kukumbwa na kashfa ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo zilizochafua maisha na utume wa Kanisa nchini Australia, kiasi cha kuwatikisa hata viongozi wakuu wa Kanisa.

Mpango mkakati wa malezi na majiundo ya waamini walei nchini Australia ni kadiri ya Mafundisho ya Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican kuhusu walei na Fumbo la Kanisa; Waraka wa Kitume wa Mtakatifu Yohane Paulo II kuhusu: wito na utume wa waamini walei ndani ya Kanisa “Christifideles laici” pamoja na Wosia wa Kitume wa Baba Mtakatifu Francisko “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili”. Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Australia, linaendelea kuwekeza pia katika utume miongoni mwa vijana wa kizazi kipya! Itakumbukwa kwamba, kunako mwaka 2008, Australia ilikuwa ni mwenyeji wa maadhimisho ya Siku ya Vijana Kimataifa.


Maoni


Ingia utoe maoni