Tarehe 16 Aprili 2019, Katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Yosefu Jijini Dar Es Salaam, Tanzania Kardinali Policarp Pengo, Askofu Mkuu wa Jimbo Kuu hilo ameongoza Misa Takatifu akiwa na Askofu Mkuu Mwandamizi Thaddeus Ruwaichi na Askofu Euzebius Alfred Nzigilwa, mapadre, mashemasi, waseminari, watawa na waamini wote. Wazo kuu limekuwa ni kufafanua juu ya maana ya tendo la siku ya kubariki mafuta matakatifu ya Krisma, lakini ambapo pia kuuliza swali juu yabaadhi ya waamini wanaoteteleka kutoka nje ya Kanisa kwenda kutafuta mipako mingine. Aidha ameelezea juu ya sikukuu ya kikuhani na kwamba, Mapadre ni washiriki wakuu wa ukuhani na sakramenti ya Upadre. Amehitimisha akiomba Mwenyezi Mungu awasaidie kutekeleze hayo yote aliyofafanua na kutambua neno hilo na ili kuwa na njia nzuri ya kufikia kuelewa vizuri maana ya upadre wao.
Nini Maana ya mkusanyiko huo katika tukio la kubariki mafuta?
Kardinali Pengo wakati wa mahubiri yake ameanza kuelezea nini maana ya mkusanyiko huo wa Jumuiya ya waamini kwa siku hiyo, kwamba inajumuisha matukio mawili. Kwanza mwenyezi Mungu anapenda kuwashirikisha waamini wake katika maisha yake ya utatu mtakatifu kwa njia ya mwanae aliyekuja kwetu. Pili ni katika kueneza na kuendeleza upendo aliodhihirisha kwa kumtuma mwane aje ulimwenguni na kufanya upendo huo uwe ni tukio la kila siku katika maisha yoyote kwa anaye mwamini. Askofu Mkuu Pengo amesema,kwamba siku hiyo wanabariki mafuta matakatifu na pia kuweka wakfu krisma. Je tendo hii lina maana gani katika Kanisa letu? Kwa kufafanua anasema: “maana yake ni kwamba, Mwenyezi Mungu alitupatia maisha mapya ndani na pamoja na mwanae, na kama ishara ya nje anatupaka mafuta yake ambayo tumesikia katika somo la kwanza na katika Injili Takatifu. Yeye akiwa mwana wa pekee alipakwa mafuta na sisi tunapakwa mafuta hayo hayo. Waamini kwa ujumla tunapakwa mafuta ya krisma takatifu tunapo batizwa au tunapozaliwa upya katika maisha hayao ambayo mwenyezi Mungu anayaweka mbele yetu. Na vile vile tunapokuwa katika safari ya kujiandaa kutekeleza majukumu kama wana wa Mungu. Ndani ya Kanisa, anatuimarisha kwa mafuta hayo hayo, mafuta ya Krima Takatifu.
Kabla ya mafuta ya Kristo kuna mafundisho
Hata kabla ya kuyajongelea mafuta ya krisima takatifu, Kardinali Pengo anabainisha kwamba, tunapewa kwanza mafundisho ya nini maana ya kuwa wana wa Mungu na hapo mwenyezi Mungu anachukua hatua ya mwanzo ya kutupaka mafuta ya kutuimarisha kama wale wanaotaka kukubali kuwa wana wa Mungu, yaani mafuta ya katekumeni, wale wanaokuwa katika daraja takatifu, wale wanaofikia hatua ya pili ya ukuhani. Mapadre wetu wanapakwa mafuta ya krisima takatifu. Mafuta yale yale wanapakwa katika viganja vya mikono yao, kusudi kila wanapoinua mikono yao, kwa niaba ya Kanisa na ndani ya Kanisa, hiyo mikono inashusha baraka za mwenyezi Mungu kwa jumuiya ya waamini. Mafuta hayo yanapakwa tena kwa wanaotakiwa katika daraja la kwanza au la tatu la ukuhani. Na Maaskofu nao wanapakwa kichwani.
Lakini hili ni tendo tofauti na tunapo batizwa, kwa maana tunapakwa katika paji la uso, makuhani wakuu wanapakwa kichwani, lakini hata paji la uso liko kichwani, anaongeza Kardinali Pengo kusisitiza, japokuwa anayepaka anaweza kuchagua sehemu yoyote ya kichwa ila hasishuke shingoni au mahali pengine, lakini iwe kichwani kwa maana, siyo tu kutoa baraka, lakini pia na kuongoza jumuiya ya waamini. Inaoongozwa na nguvu ya yule Roho Mtakatifu, kichwa cha Kanisa Jumuiya ya Makuhani wanaweza kuliongoza Kanisa ipasavyo na wakisindikizwa na yule Roho ambaye ndiye katika ishara ya mafuta hayo yaweze kuhakikisha kwamba yale yanayo fundishwa ndani ya Kanisa ni mafundisho ya Bwana wetu Yesu Kristo. Hiyo ndiyo maana ya mkusanyiko wa a subuhi hiyo ya kubariki na kuomba baraka za mwenyezi Mungu juu yake, ili Kanisa letu, Kanisa katika Jimbo la Dar Es Salaam kwa niaba ya Kanisa la ulimwenguni lote liweze kuwa ni sehemu hai ya kweli ya kudhihirisha upendo na kujali kwa Mungu mwenyewe kwa ajili ya watu wake, kama anavyo mjali na kumpenda mwanae wa pekee akampaka mafuta, ndilo hili analolifanya kwa Kanisa lake hapa kwetu na ulimwenguni kote, amesisitiza Kardinali Pengo.
Swali la Kardinali kuhusu waamini katika kutafuta mpako nje ya Kanisa katoliki
Kardinali Pengo akiendelea na mahubiri yake ameonesha dukuduku juu ya waamini wanaotoka nje kwenda kutafuta mipako na hivyo anasema:“Siku hizi nimekuwa na swali moja likinisumbua kichwani mwangu. Waamini tumejaliwa na kushuhudia kupendwa na mwenyezi Mungu kwa njia ya haya mafuta matakatifu kwa kiwango hiki! Tunapoka nje ya Kanisa na kwenda kutafuta mpako mahali pengine tunakwenda kupakwa na roho gani? Kuna mpako gani unaoweza kuwa wa ziada na wenye nguvu zaidi kuliko mpako tunao upata ndani ya Kanisa letu Katoliki? Mnatafuta nini katika mipako hiyo? na mipako itawaletea maibilisi. Kardinali Pengo amezidi kusisitiza sana swali hili linalo msumbua na hasa kulikabidhi kwa mapadre, ili waweze kuwaelezea vizuri waelewe. Hata hivyo amesema:“Tunahitaji na sisi maisha yetu yaadhihirishwe ukomavu wa imani hiyo tunayo waeleza waamini hawa”.Wapo waamini ambao wanakwenda kutafuta mipako nje na ambayo Kardinali anasisitiza, haelewi na kwamba wajue wanajitenge na Yeye kichwa cha Kanisa , kujitenga na Kristo mwenyewe. Aidha ametoa mfano kwamba: Kama mimi mwenyewe usiku natoroka na kwenda sijuhi wapi, labda Bagamoyo kwenda kupakwa mafuta, je nitajificha kwa kiwango gani? Kiasi kwamba hasijue mtu mwingine yoyote, mbona yule yule anayekupaka atakwenda kueleza: mnajidai nini hata askofu wenu amekuwapo hapa kupakwa mafuta, huko mnapoteza muda, njoni kwangu, atawambia hivyo….”.
Msisitizo wa mafundisho ya mpako kwa waamini ili waelewe
Kardinali Pengo akiendelea kusisitiza juu ya sauala hili, amewaomba mapadre wawafundishe waamini wao ukweli mtakatifu na maana ya mpako mtakatifu ndani ya Kanisa. Maisha yetu wenyewe anasema, lazima yajidhihirishe imani hiyo, na sisi wenyewe lazima tuimarike kwanza ndani ya imani na hapo tutaweza kuwaaminisha ndugu zetu”. Ninamwomba ili adhimisho tunalolifanya siku ya leo na tunalifanya kurudia mwaka hadi mwaka, liwe la manufaa, siyo tu kwa waamini wenzetu peke yao, lakini kwanza sisi makuhani wenyewe, kuanzia na yeye mwenyewe kama kuhani wa ngazi ya tatu au ya kwanza potelea mbali…Lakini muumini yoyote ambaye amekwisha kubatizwa, hasa yule aliyekwisha kupokea sakramenti ya kipaimara, tendo hilo liwaweke pamoja na kuwaimarisha.
Sikukuu ya kikuhani:Upadre unaopokelewa ni kutoka kwa Bwana Yesu
Kardinali Pengo akiendelea kufanaua katika na mahubiri yake amesisima kuelezea maana ya sikukuu ya kikuhani na kwamba : “Ni siku yetu mapadre na ningependa kueleza neno fupi kwa ajili yetu mapadre.” “Katika kipindi cha kwaresima tunakumbushwa mara nyingi kwa njia ya msalaba hasa tunapokuwa katika kituo cha tano cha njia ya msalaba, pale Simone wa Kirene anapomsaidia Yesu kuchukua msalaba, na tunaomba hivi: Wajalie vijana wengi wito wa upandre ili aweze kuchukua msalaba pamoja nawe kwa ajili ya wokovu wa dunia… kwa maana hiyo Kardinali anathibitisha: Upadre tunao upokea ni upadre wake Bwana wetu Yesu Kristo na upadre huo ulifikia utimilifu wake na kilele chake wakati ule ambapo Bwana wetu alichukua msalaba wake akaufikisha kilimani Karvario na juu ya msalaba huo akatoa sadaka timilifu ya ukombozi wa ulimwengu. Na sisi mapadre ni washiriki wakuu wa huo ukuhani wa Yesu Kristo. Ni wazi kwa ubatizo tunashirikishwa, tunaimarishwa, lakini kwa njia ya sakrametni ya upadre tunafanyika kama tulivyo kumbushwa kila mwaka, ya kwamba tunafanyika kila mmoja wetu Altar Christus. Ni Kristo mwenyewe na siyo mwingine au wa ziada, bali yeye mwenyewe. Yule anayesisima kwa niaba ya Kristo ni Kristo katika hali ya kuonekana wazi kwa jumuiya ya waamini, Amesisitiza Kardinali Pengo.
Kituo cha tano cha njia ya msalaba:Yesu anasaidiwa msalaba
Na kama Kristo alivyo chukua msalaba akapanda mpaka Karvario, katika kituo cha tano tunakumbushwa kwamba wale wanaofikia katika daraja la upadre ni wale wanaochukua msalaba pamoja na Kristo au ndani ya Kristo na hivyo akaweza kutoa sadaka juu ya msalaba huo wa Kristo kwa manufaa na kwa wokovu wa ulimwengu. Amesisitiza Kardinali pengo kwa mapadre kuelewa uzito wa maneno hayo na kusema : Hatuwezi kutafuta maisha lelemama yasiyokuwa na msalaba katika maisha yetu, na alafu wakati kila siku tunatolea Ekaristi Takatifu juu ya altare, bila kuwa na imani. Altare zinaweza kuwa zimetengenezwa kwa aina nyingi lakini lazima zidhihirishe msalaba wa Yesu Kristo, msalaba wake Yesu Kristo, msalaba huo ni ule ulio bebwa na Kristo kufikia Karvario. Amehitimisha akiomba kwamba: “Mungu atusaidie ili kutekeleza hayo, atuimarishe mahali tunapoteteleka na atusaidie kutambua hilo neno na njia nzuri kabisa ya kufikia kuelewa vizuri maana ya upadre watu”. Amewatakia maandalizi mema ya Pasaka na sikukuu njema na kuwaomba wawasaidie waamini kusherehekea vema sikukuu hii ya Pasaka ya Bwana.
Maoni
Ingia utoe maoni