Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano, tarehe 17 Aprili 2019 amerejesha tena mawazo yake kwenye janga la moto lililotokea, Jumatatu, tarehe 15 Aprili 2019 na kusababisha Kanisa kuu la Notre Dame, Jimbo kuu la Paris, Ufaransa kuungua moto na hivyo kusababisha hasara kubwa. Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, amesikitishwa na kuguswa sana na janga hili ambalo limewashtua watu wengi ndani na nje ya Ufaransa na kwamba, yuko pamoja nao kwa njia ya sala.
Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza wale wote waliojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kusaidia kuzima moto pamoja na kuokoa mali ya Kanisa iliyokuwa Kanisani humo hata kwa kuthubutu kuhatarisha maisha yao. Watu wote hawa wapokee shukrani kutoka kwa Kanisa zima. Kwa njia ya maombezi na tunza ya Bikira Maria, azidi kuwaombea, ili kwamba, mchakato wa ukarabati wa Kanisa Notre Dame uanze na kusonga mbele kwa haraka kama kielelezo cha shukrani na utukufu kwa Mwenyezi Mungu!
Wakati huo huo, Baba Mtakatifu anakumbusha kwamba, Alhamisi Kuu, Kanisa linaanza kuadhimisha Mafumbo makuu ya wokovu, yaani: Siku kuu ya Ekaristi Takatifu, Daraja Takatifu na Amri ya Upendo inayomwilishwa katika huduma inayofumbatwa katika unyenyekevu. Ijumaa Kuu, Kanisa linakumbuka: mateso na kifo cha Kristo Yesu! Jumamosi, Kanisa linakesha kumsubiri Mkristo Mfufuka, kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu kwa waja wake. Fumbo la Pasaka liwe ni chemchemi ya imani, matumaini na mapendo yanayomwilishwa katika huduma kwa jirani, lakini zaidi kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii!
Maoni
Ingia utoe maoni