Tarehe 2 Februari 2019, Baba Mtakatifu Francisko ametuma ujumbe wake kwa njia ya video kufuatia na uzinduzi wa kituo cha Afya cha watoto huko Jamhuri ya Afrika ya Kati, ni kituo kinacho saidiwa na Hospitali ya Bambino Gesu. Katika ujumbe wake anawasalimia wote katika sikukuu ya furaha ya kuzindua jengo la afya ambalo linajikita kusaidia watoto wa Jamhuri ya Afrika ya Kati. Kituo hicho kimetokana na msaada wa Hospitali ya watoto Bambino Gesu’ Roma ambayo ni shughuli iliyonzishwa kunako mwaka 2016, kwanza kwa mafunzo ya wahudumu, madaktari na wengine.
Ni matarajio ya Baba Mtakatifu kuwa kituo hicho kinaweza kuwa cha kipekee, mahali ambapo watoto wanaweza kupata jibu na faraja ya mateso na upendo. Hata hivyo anaonesha ni kwa jinsi gani haweza kusahau, kwa maana bado anakumbuka macho ya uchungu wa watoto wengi ambao hawakuwa na lishe alio kutana nao katika hospitali hiyo wakati wa ziara yake nchini humo. Aidha bado anakumbuka maneno ya Daktari aliyekuwa karibu naye akimweleza kuwa: sehemu kubwa ya watoto hawa watakufa, kwa maana wana maleria kali na hawana lishe. Maneno hayo aliyasikia mwenyewe na hivyo anasisitiza kuwa, hisitokee tena! Aidha anasema ni wazi kwamba mateso ya watoto vigumu kuyakubali. Anamtaja mwandishi maarufu Dostoevskij kuwa alikuwa ametoa swali: kwanini kuna mateso ya watoto? Na Baba Mtakatifu Francisko anaongeza kusema, mara nyingi ninajiuliza swali lenyewe, kwanini watoto wanateseka? Na hakuna maelezo. Ni kuangalia msalaba tu na kuomba upendo wa huruma ya Baba kwa ajili ya mateso mengi, anathibtisha Baba Mtakatifu
Akiendelea kuelezea Baba Mtakatifu anasema, jengo hili ambalo linazinduliwa ni ishara ya dhati ya huruma ambayo asili yake ni Mwaka wa Huruma ambao yeye mwenyewe alipendelea kufungulia huko kabla ya wakati, tarehe 29 Novemba 2015 mjini Bangui. Mlango wa kwanza wa Kanisa Kuu kufunguliwa ilikuwa ni ule wa Bangui na siyo wa Mtakatifu Petro. Ilikuwa ni ishara ambayo Bwana alijalia. Kwa kupitia Mlango Mtakatifu wa Kanisa Kuu, Baba Mtakatifu anasisitiza kwamba alisema:Bangui inakuwa mji wa kitasaufi katika sala ya huruma ya Baba. Sisi sote tunaomba amani, huruma, mapatano, msamaha na upendo. Kwa maana hiyo ni upendeleo wa Baba Mtakatifu FRancisko kwamba,Mlango huo Mtakatifu uwe bado umefunguliwa na kwamba, mito ya zawadi ya huruma iweze kububujika maisha katika Hospitali ya watoto Bangui na wale ambao wanafanya kazi. Na wakumbuke daima kwamba:kuna ishara nyingi za wema wa dhati na huruma inayowatazama wadogo, wasiojilinda, waliopweke na waliotupwa. Wapo kweli wadau wa upendo ambao hawakoseshi kamwe mshikamano kwa ajili ya masikini zaidi na wasio kuwa na furaha ( rej. Barua ya misercordia et Misera, 17).
Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe wake kwa njia ya video pia anawatia moyo wote ambao wanajikita katika shughuli ya kutibu watoto, wakisukumwa na upendo kwa kufikiria daima msamaria mwema wa Injili. Wawe makini kwa mahitaji ya watoto wadogo wagonjwa, wainame kwa huruma juu ya udhaifu na katika wao wanaweza kumwona Bwana. Anayehudumia wagonjwa kwa upendo anahudumia Yesu anayetufungulia Ufalme wa Mungu. Katika Hospitali hiy , Baba Mtakatifu anasema inawakumbusha wote kuwa, kila ambacho wanaishi ni kipindi cha huruma kwa maana wale walio wadogo na wasio na walinzi, wako mbali na peke yao, wanaweza kupokea uwepo wa kaka na dada ambaye anawainua katika mahitaji yao ( rej. Barua ya misercordia et Misera, 21).Baba Mtakatifu anawapa ushauri kuw: kwa kujikita katika taaluma yao ya udaktari, wawe mafundi wa huruma!
Kwa kuhitimisha Baba Mtakatifu amsalimia Rais wa nchi Bwana Faustin-ArchangeTouadéra, Balozi wa Vatican nchini humo Askofu Mkuu Santiago De Wit Guzmán na Rais wa Hospitali ya watoto Bambino Gesu, Bi Mariella Enoc, mbaye amefanya kazi sana kwa ajili ya kituo hicho. Amsalimia Kardinali Konrad Krajewski ambaye yuko huko kwa ajili ya fursa hiyo ili aweza kuwakilisha katika dunia upendo wa Papa. Anayetubu wadogo yuko upande wa Mungu, wasisahau! Anayetibu wadogo yupo upande wa Mungu na anashinda utamaduni wa ubaguzi! Hospitali hiyo inaweza kugeuka kuwa mfano na kuwa kituo cha kufikia kwa watu wote wa nchi. Baba Mtakatifu amesisitiza wakumbuke kuwa, katika mgonjwa yupo Yesu na katika upendo kwa yule anayeinama juu ya majeraha kuna njia ya kukutana naye. Amewabariki na kuwaomba wasisahau kusali kwa ajili yake.
Maoni
Ingia utoe maoni