Alhamisi. 21 Novemba. 2024
feature-top
Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania: Ujumbe wa Kwaresima 2019: Kauli mbiu: Familia Kanisa la Nyumbani na ni Shule ya Imani na Maadili

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania limetangaza kwamba, Mwaka 2019 kuwa ni Mwaka kuwa ni Mwaka wa Familia: Matunda ya Adhimisho la Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji. Haya yamo kwenye Ujumbe wa Kwaresima kwa Mwaka 2019 unaoongozwa na kauli mbiu “Familia Kanisa la Nyumbani na ni shule ya imani na maadili. Maaskofu wanakazia tunu msingi za maisha ya ndoa na familia!

Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania limetangaza kwamba, Mwaka 2019 kuwa ni Mwaka wa Familia: Matunda ya Adhimisho la Jubilei ya Miaka 150 ya Uinjilishaji. Haya yamo kwenye Ujumbe wa Kwaresima kwa Mwaka 2019 unaoongozwa na kauli mbiu “Familia Kanisa la Nyumbani na ni shule ya imani na maadili. Maaskofu wanakazia kwa namna ya pekee familia kama msingi wa jamii ya binadamu kama inavyofafanuliwa na Mapokeo ya Kanisa. Maaskofu wanadadavua dhana ya familia mintarafu Maandiko Matakatifu: Ukuu na Utakatifu wa Ndoa kadiri ya Agano Jipya. Maaskofu wanakiri kwamba, familia ni shule ya imani na maadili inayofumbatwa katika maisha ya: Sala, Sakramenti za Kanisa na Liturujia; mambo msingi yanayoiwezesha Familia kuwa ni Kanisa dogo la nyumbani, mahali pa makuzi na elimu makini kwa watoto! Familia ya Kikristo ni kituo cha maendeleo jamii na endelevu na mwishoni, Maaskofu katika ujumbe wa Kwaresima wanahimiza kuhusu Amri kuu ya Upendo, elimu ya dini; kulinda na kudumisha tunu msingi za maisha ya ndoa na familia na kwamba, Bikira Maria ni Malkia wa familia! Mwishoni, wanahitimisha kwa Sala kwa ajili ya kuombea familia bora na imara!

UTANGULIZI: 1.1. Ujumbe wa Kwaresima 2019

Kama ilivyo ada kila mwaka, sisi Maaskofu Katoliki hutoa ujumbe mahsusi katika kipindi cha Kwaresima. Kila ujumbe huwa na dhamira maalum ya kuzingatia, ili katika kujitafakari na kuamsha upya maisha yetu ya Imani Katoliki na Maadili yake, tutambue zaidi na tukiri kwa dhati jinsi hali yetu ilivyo mbele ya Mungu ambaye ndiye chanzo cha utakatifu, na sisi kama wadhambi tulio safarini kuelekea huo utakatifu. Hivyo basi, kwa mwaka huu wa 2019 baada ya kuadhimisha miaka 150 ya Kanisa Katoliki Tanzania mwaka jana 2018, tumeona ujumbe wa mwaka huu uzingatie dhamira inayohusu familia zetu. Dhamira hii ni “Familia kama Kanisa la Nyumbani na Shule ya Imani na Maadili”.  Kwa mwaka huu basi, tutafakari kwa namna gani hili lifanyike kwa kuzingatia kuwa Familia ya Kikristu ni Shule ya Imani Katoliki na Maadili yake.

 SURA YA KWANZA: FAMILIA NI MSINGI WA JAMII YA KIBINADAMU

Mwaka 2019 kuwa Mwaka wa Familia: Matunda ya Adhimisho la Jubilei, Miaka 150 ya Uinjilishaji.

Kwa kuzingatia hayo, sisi Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania, pamoja na kuwa na dhamira hiyo, tumeuteua mwaka huu wa 2019 kuwa ni Mwaka wa Familia, kama ishara na fursa ya kutafakari kwa undani zaidi matunda ya adhimisho la Jubilei ya Miaka 150 ya Kanisa Katoliki Tanzania kama Familia ya Mungu. Uamuzi huo unajengwa juu ya sababu kuu nne za msingi kuhusu mwaka huu wa 2019. Kwanza,ni miaka ishirini na mitano tangu ilipoazimishwa Sinodi ya kwanza ya Afrika, ambapo Kanisa lilikubaliana na mtazamo wa Kiafrika kuwa Kanisa ni Familia ya Mungu. Kwa hivyo, kiimani na kijamii binadamu anakiri kwamba familia ndiyo msingi wa jamii ya kibinadamu, na hivi kuijenga familia imara ni kuwa na jamii na Kanisa imara. Mababa wa Kanisa walielezea familia kuwa ni kiini cha kwanza na cha uhai wa jamii. Kama tunavyosoma kutoka Ecclesia in Africa, “Kwa kuwa Muumba wa vitu vyote ameanzisha ushirika wa mume na mke kama asili na msingi wa jamii ya kibinadamu, familia ni kiini cha kwanza cha uhai wa jamii.” (Ecclesia in Africa no. 85). Lakini Kwaresima hii tunaalikwa kutambua utume wa Familia kupitia wanafamilia ambao wengi wao ni walei, kama Mababa wa Kanisa wanavyotuambia kwenye Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican: “Ni juu ya walei , kutokana na wito wao, kutafuta ufalme wa Mungu wakiyashughulikia mambo ya dunia na kuyaelekeza kadri ya Mungu. Wanaishi ulimwenguni, yaani katika kazi zozote na shughuli za kidunia na katika mazingira ya kawaida ya maisha ya kifamilia na ya kijamii, ambayo maisha yao yamefungamanishwa nayo.

Hapo wanaitwa na Mungu kusaidia kuutakatifuza ulimwengu, kama kutoka kwa ndani, mithili ya chachu, katika kuyatimiza majukumu yao wenyewe, wakiongozwa na roho ya kiinjili, na hivyo wamdhihirishe Kristo kwa wengine, waking’aa hasa kwa ushuhuda wa maisha yao, imani, matumaini na mapendo. Kwa hiyo yawahusu hao kwa namna ya pekee kuyatangaza na kuyapanga mambo yote ya kidunia, ambayo wamefungamana nayo, ili daima yafanyike na kukua kadri ya Kristo na kuwa kwa sifa ya Muumba na Mkombozi”(Lumen Gentium no. 31). Ili hiki kitelezeke inabidi familia iwe imara kiimani na kimaadili. Pili, mwaka huu ni kumbukumbu ya miaka ishirini na tano tangu pale Umoja wa Mataifa ulipotamka kuwa mwaka 1994 ni mwaka wa familia. Ni vema tukanukuu maneno ya msingi kuhusu nia ya Umoja wa Mataifa kwa kutenga mwaka huo kuwa ni mwaka wa familia. Umoja wa Mataifa ulitamka kwamba: “Familia inaunda kitengo cha msingi cha jamii na kwa hiyo inahitaji kuhakikishiwa uangalizi maalum. Hivyo basi, ulinzi mpana kabisa iwezekanavyo na msaada husika lazima vitolewe kwa familia zote ili nazo ziweze kuchukua majukumu yake ndani ya jamii, kutokana na matakwa ya  Tamko la Ulimwengu la Haki za Binadamu, Tamko kuhusu Ustawi na Maendeleo ya Kijamii, na Mkataba wa Kufutilia Mbali Namna Zote za Ubaguzi dhidi ya Wanawake"

Familia ni kitovu/kiini cha jamii (cell of the society) na ni lazima ijengeke katika hadhi ya binadamu kadri ya hulka ya binadamu iliyokusudiwa na Muumba, na sivyo inavyotafsiriwa bila kurejea kwa Mungu.Hii ndiyo italeta umaana wa familia kuwa msingi wa jamii. Mtakatifu Yohane Paulo wa Pili anathibitisha kuwa ukweli unaojikita kwenye hulka upo kwenye jamii tayari kama wote tuko kwenye hulka aliyoitengeneza Mungu kama wote tunakubaliana naye. “The splendour of truth shines forth in all the works of the Creator and, in a special way, in man, created in the image and likeness of God (cf. Gen 1:26). Truth enlightens man's intelligence and shapes his freedom, leading him to know and love the Lord” (Veritatis Splendor page no.1).

Tatu, mwaka huu pia ni mwaka wa Jubilei ya Miaka 50 tangu Halmashauri ya Walei ya Kanisa Katoliki ilipoanzishwa mwaka 1969. Kwa kuwa Halmashauri ya Walei katika ngazi zake zote inayo Kamati Ndogo inayohusika na Familia na Malezi, ni haki na ni vema Dhamira ya Familia ikawa ndiyo kiini mwafaka cha ujumbe wa Kwaresima kwa mwaka huu tunapoidhimisha Jubilei hiyo. Na hasa kwa sababu zaidi ya asilimia 90 ya Waumini Wakatoliki ni walei wanaotakatifuza malimwengu kupitia maisha ya kitume katika familia zao, kama baba na mama, au babu na bibi, au mjomba na shangazi, au kaka na dada, shemeji au binamu. (Gaudium et Spes, no. 43 / Lumen Gentium, no. 31, 33).

Nne, mwaka huu pia ni adhmisho la mwaka wa Jubilei ya Dhahabu (Miaka 50) tangu chama cha kitume kinachowaunganisha wanafunzi wote Wakatoliki walioko sekondari; chama kinachojulikana kwa jina la Young Catholic Students, au kwa kifupi YCS. Kwa kuwa vijana bado wako chini ya wazazi wao na familia kwa upana wake kimalezi na kimakuzi, ni mwafaka basi tukatafakari kwa namna gani familia zinaweza kuwa kweli shule za Imani Katoliki na Maadili Yake kwa vijana hawa ambapo kwa sasa tunaona wengi. Idadi yao kitakwimu ni takribani zaidi ya milioni moja na laki saba kidato cha kwanza hadi cha sita. Hiki chama cha kitume katika jubilei yao ya miaka hamsini hatuna budi kama familia tutafakari upya tuwaongezee malezi gani ili wawe raia wema zaidi, na hatimaye waweze kuwa msingi katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani na mbinguni.

Haja na Hoja ya Kuitafakari Familia: Leo hii, baada ya neema, baraka na mwanga zaidi wa Jubilei ya miaka 150 kuhusu nini maana ya kuwa Mkristo; maana na utume wa Familia ya kikristo ni vitu ambavyo haviwezi kuendelea kuchukuliwa juu juu tu. Ni lazima vitamkwe kwa dhati, vielezwe upya, vitetewe bila mashaka yoyote, na wanafamilia wenyewe watoe ushuhuda kwa jamii nini maana ya familia, kuwa ni Kanisa la nyumbani, na hivyo kuwa ni Shule ya imani na maadili. Sababu kuu ya kuwa na msimamo thabiti juu ya familia ni nini na ndoa na maana halisi ya ndoa, ni kwa sababu leo hii kuna dhana potofu na hata nadharia zisizo sahihi zinazolenga kuhalalisha vitendo vinavyopelekea kutenganishwa kwa ndoa na familia. Kutenganisha huku kunatokana na dhana yenye maana potofu ya ndoa inayotolewa kwamba ndoa ni maridhiano ya wawili bila kufungamanishwa na jinsia zao. Hii ni maana potofu inayotetewa na baadhi ya jamii. Hii ni dhana iliyopotoka kihulka (unnatural), kiimani na kimaadili. Imani Katoliki na maadili yake inapingana kabisa na mtazamo wa namna hii, au hoja zinazoweza kutokana na mtazamo kama huo.

Hii ni kwa sababu Muumba wa vitu vyote ameisimika taasisi ya familia kwa kuweka muungano wa kindoa kati ya mwanaume na mwanamke kuwa ndiyo chanzo na msingi wa jumuiya ya kibinadamu, yaani familia. Kwa maana hiyo, familia ndiyo kiini cha kwanza cha uhai wa jamii. Siku zote tutilie maanani kuwa katika mpango wake Mungu Muumba, mahali pa msingi ambamo watu wanajifunza kuwa watu ni kwenye familia. Hii inamaanisha kuwa ni katika familia ambamo kila mtoto kwanza anajifunza uwepo wa Mungu, kumpenda Mungu huyu, kutenda yanayoendana na huyu Mungu na mtoto huyu kutamani kuungana na Mungu huyu milele. Mtoto hupokea haya kutoka kwa wazazi wake na walezi wake, yaani kutoka kwenye familia.

1.3 Changamoto Zinazoikabili Familia ya Sasa

Kazi kubwa ya Kristo ilikuwa ni kumkomboa mwanadamu dhidi ya dhambi na matokeo yake mabaya (Rej.Lk. 4:18-19; Lk. 5:20, 27-32). Kanisa kama mwili wa fumbo wa Kristo linao wajibu wa msingi wa kuendeleza kazi ya Kristo kwa wanadamu.  Mahali pazuri pa kufanya kazi hiyo ni kupitia familia ambapo mtu hupata uhai na malezi ya kiutu na kiroho. Kwa kuzingatia hali ya sasa na changamoto zake katika familia na ndoa jitihada zozote za kuelimisha jamii juu ya mpango wa Mungu kwa kila binadamu hapa duniani, lazima familia zetu zijipange kukabiliana na changamoto zile zinazoukabiri ulimwengu wetu wa sasa katika karne ya ishirini na moja na nchi yetu ya Tanzania ikiwemo.

Changamoto hizo ni kama vile: Talaka, Ndoa za utotoni, Uchumba sugu, Ndoa za mitaala, Kukosa uaminifu ndani ya ndoa, Ndoa za kurithi wajane, Ndoa za Jinsia moja, Ndoa baada ya ndoa ya kwanza halali, Ndoa zisizo na watot, Kubadili maumbile. Matatizo mengine ni pamoja na: Familia za mzazi moja, Familia zenye mchanganyiko wa Imani, Familia zinayoishi katika mazingira magumu ya uchumi, Familia zenye watoto walemavu, Familia zisizo na mzazi hata mmoja, Familia zisizoishi imani, Familia zisizo na maadili, Familia zilizopoteza uwezo wa kulea, Familia zisizo na kipato. Asili ya matatizo katika ndoa na familia ni pamoja na:-

1.3.1        Utamaduni na Mazingira: Tunaishi katika historia yenye mazoea, mila, desturi na mapokeo ya wazee wetu.  Iko sehemu ya utamaduni wetu isiyokubaliana na ukweli wa kimungu ambao ni wa lazima katika kuishi ndoa safi na familia bora. Mpaka sasa katika mazingira yetu zipo tamaduni zinazoruhusu talaka, ndoa za utotoni, uchumba sugu, ndoa za mitaala, “nyumba ndogo”, ndoa za kurithi wajane, ndoa za jinsia moja na ndoa baada ya ndoa ya kwanza halali. Ni jukumu la kila mkristu, ndani ya familia, kuchekecha utamaduni wake, kwani kumekuwa na chenga zisizopita katika chujio la Kristo aliye Mwanga wa maisha yetu.

1.3.2. Harakati za kila mmoja ambazo zinalenga moja kwa moja kuibomoa familia: Harakati hizi zinatangaza na kupigia upatu uhuru usio wa kweli kwa mwanadamu.  Zinapotosha ukweli kwa kutenganisha ukweli wa maisha na ukweli wa asili katika viumbe na maumbile yao.  Maisha ya kiroho, maisha ya ndoa na familia, yanakuwa ni jambo binafsi na la faragha bila kuhusisha jamii na wala kumhusisha Mungu.  Uhusiano wa mtu na jamii unahuishwa katika sheria tu ambazo jamii inazitunga na kuzibadili mara kwa mara. Matokeo mabaya ya harakati  hizi ni kukithiri kwa ubinafsi, kuenea na kuzagaa kwa matukio yenye kuchochea waziwazi tamaa za ngono kati ya watu wa rika zote. Wimbi kubwa la maisha huria, bila malengo wala kanuni na nidhamu ya kukataa malengo mema. Kuongezeka kwa mifarakano ya ndani ya nafsi na hivyo mifarakano kati ya mtu na mtu ndani na nje ya familia kunakoshuhudiwa na matatizo ya msongo wa mawazo, hali ya kukata tamaa.

Harakati hizi zimejaa kwa wengi, na pia mtazamo potofu kuhusiana na maadili katika ndoa na familia. Na hivi mtu kufikia mahali kujiaminisha kwamba maisha yanawezekana bila Mungu na bila utu. Msimamo huu haumwezeshi mtu kupokea na kudumisha tunu njema za maisha ya ndoa na familia, ambazo kuasisi tunu hizo huzifanya ndoa na familia zifanyike katika kweli na zidumu na kusitawi na kuzaa matunda. Changamoto za ndoa na familia kimsingi ni changamoto za kukubali na kupokea tunu za maisha ya ndoa na familia. Tunahitaji kujihoji mbele ya Kristo juu ya wito wa kuwa wavumilivu, wasamehevu, wenye kiasi na wenye subira Rej. 1Kor.13:1-8). Tunahitaji kujipima tena kama tunazithamini na kuvutiwa nazo zile heri nane alizozitangaza Bwana wetu Yesu Kristo ambazo ni usafi wa moyo, upole, unyenyekevu, upatanisho, kuudhiwa kwa ajili ya haki, kukubali kushindwa/kudhulumiwa kwa sifa na utukufu wa Mungu (Mt.5:3-12).

Tunahitaji kujithamini mbele ya Mungu, kuona thamani ya upendo wa Kristo kwetu na wa yule aliyetupatia Kristo.  Maana “Yeye asiyemwachilia Mwana wake mwenyewe, bali alimtoa kwa ajili yetu sisi sote atakosaje kutukirimia na mambo yote pamoja naye” (Rum.8:32). Hakuna anayeweza kututenga na upendo wa Kristo (Rum.8:35-39). Utatuzi wa matatizo mengi katika ndoa unajikita kimsingi katika changamoto ya kurudisha sura njema ya maagano kati ya Mungu na katika utakatifu kati ya Kristo na Kanisa lake (Rej.Waefeso 5:21-25).

Wakristo wenye ndoa na ni wazazi kwa njia ya ubatizo wao wanawajibika kutoa mchango wao wa pekee kwa ajili ya kufafanua mafundisho na tunu za kiinijli katika mazingira na tamaduni mbalimbali za leo ambamo kwazo wanafamilia huishi maisha ya familia. Wanandoa kwa namna ya pekee wamestahilishwa jukumu hilo kwa sababu ya karama yao na jukumu lao la kisakramenti hasa sakramenti ya ndoa. Wanandoa kwa kuheshimu mpango wa Mungu hubeba jukumu kuu la kuwa wazazi ambapo hukubaliana na wito wa Mungu kuwaleta duniani watoto. Mungu huendeleza kazi yake ya uumbaji na kuendeleza uhai wa kimwili na kiroho kwa kuwatumia wazazi. Hivi kukubali kuwa mwanandoa ni kukubali jukumu la kuuweka uhai wa binadamu kuwa ni jukumu la kimungu linalomtaka mtu amsikilize Mungu Muumbaji na anaye- takatifuza.

1.4 Hali ya Familia katika Ulimwengu wa Leo: Katika ulimwengu wa leo, familia hujikuta katika hali ambayo uhuru wa mtu binafsi huonekana kuwa na nguvu kubwa katika kufanya maamuzi juu ya maisha ya ndoa. Kwa watu wenye kufuata utamaduni huu huathiri tunu za ndoa zinazotokana na Injili. Hulka ya binadamu na utu wa mwanandoa huonekana kutenganishwa na kusudio la Mungu la kumuumba mwanadamu. Mungu amemuumba mwanadamu kwa sura na mfano wake yaani ukutanapo na mwanadamu kwa kutumia milango ya fahamu na akili unapaswa kuuona uwepo wa Mungu aliye hai.

Ni dhairi ya kuwa leo hii ipo hali mbaya ya udhalilishaji wa tunu za msingi kama vile: Maana isiyo ya sahihi ya kinadharia na kiutendaji kuhusu uhuru wa wote waliooana kwa kuhusiana wao kwa wao. Mawazo potofu kuhusu uhusiano wa mamlaka kati ya wazazi na watoto. Hali halisi ya matatizo ambayo kwayo familia hupata katika kurithisha tunu za familia.  Kuongezeka kwa idadi ya talaka. Pigo la uharibifu wa mimba. Utumiaji wa daima wa madawa ya kuua kizazi. Kujitokeza dhairi mwelekeo wa fikra za uzuiaji wa mimba n.k. Kwa hiyo maisha hayatambuliwi kama ni zawadi na baraka, bali kama ni hatari kuu ambayo inabidi kujihadhari nayo.

Hali hii ndiyo imetufanya sisi Maaskofu wa Tanzania kuwaletea tafakari juu ya familia ili Kanisa liweze kupambana na hali ya upotoshaji wa matumizi ya uhuru binafsi juu ya ndoa na familia. Mwanadamu aliye nje ya mpango wa Mungu juu ya ndoa na familia amesababisha uvunjivu wa mahusiano kati ya mtu na Mungu na hata kati ya mtu na mtu kadri ya msemo wa Mt. Augustino, mgongano wa hali ya mapendo ya kumpenda Mungu kiasi cha kudharau nafsi na kupenda nafsi kiasi cha kumdharau Mungu (St. Augustine, De Civitate Dei, XIV, 28: CSEL, 40: II56-57). Licha ya mchango chanya wa utandawazi na mwingiliano wa tamanduni mbalimbali mwanafamilia aliyelelewa na kujilea kwa kuheshimu mpango wa Mungu amejikuta katika giza pale anapojikuta katika utamaduni ambapo mtu anajipangia kila kitu juu ya ndoa na familia bila kumhusisha muumba wake. Tuliwaona wana waisraeli na hata desturi za jamii mbalimbali siku za nyuma walivyompa Mungu nafasi ya pekee katika kufanya maamuzi yao juu ya ndoa na familia.

Hali ya kumweka Mungu pembeni katika masuala yahusuyo ndoa na familia inasababisha upotoshaji mkubwa juu ya maana ya ndoa na familia. Kupotosha huku kumepelekea kuwa na baadhi ya watu kushindwa kujenga mshikamano na Kristu aliye mkombozi pekee wa mwanadamu. Watu wanaopotosha mpango wa Mungu juu ya ndoa na familia wanaweka mazingira magumu kwa kazi ya Yesu Kristo na hata kusababisha utawala wa Yesu Mfufuka usiwe bayana kwenye jamii. Yesu amekuja kuunda jamii inayotokana na familia zinazoongozwa na Neno la Mungu ambalo ni chakula kiletacho uzima wa milele kwa wanafamilia. Ili kurejesha uelewa sahihi na maisha sahihi ya wanandoa na wanafamilia watu wote tunaalikwa na Huruma na Upendo wa Mungu unaotualika kuongoka. Na hapa kitakachotupatia mwanga katika safari ya kuuelekea wongofu, ni Maandiko Matakatifu, yaani Biblia Takatifu pamoja na nyaraka mbali mbali za Mababa Watakatifu.

 SURA YA PILI

2.0 FAMILIA KATIKA BIBLIA KWA UJUMLA

 Kwa kuwa chimbuko la Imani Katoliki ni Kristu Mfufuka, ambaye anaendelea kuilea jamii ya kibinadamu kama Mkombozi pekee wa binadamu wote hatuna budi kuyatumia Maandiko Matakatifu katika kuielewa familia. Yesu huyu aliyezaliwa Nazareti katika jamii na familia ya Kiyahudi anaendelea kuongea na binadamu kupitia maisha katika yeye, na kupitia Maandiko Matakatifu, tunayoyapata kwenye Biblia Takatifu. Turejee baadhi ya sehemu za Maandiko Matakatifu na desturi za Kiyahudi ili kujenga msingi na hoja ya kiimani kuhusu maana ya kuiona familia kuwa ni shule ya Imani na maadili.

2.1 Nafasi ya Familia katika Agano la Kale

Uelewa wote wa Kiyahudi juu ya maisha ya familia, uwe mzuri au mbaya ulitegemea sana Maandiko Matakatifu hasa kitabu cha Mwanzo 1:26-28: “Mungu akasema, ‘Na tufanye mtu kwa mfano wetu, kwa sura yetu, wakatawale samaki wa baharini, na ndege wa angani, na wanyama, na nchi yote pia, na kila chenye kutambaa kitambaacho juu ya nchi.’ Mungu akaumba mtu kwa mfano wake, kwa mfano wa Mungu alimwumba, mwanamume na mwanamke aliwaumba. Mungu akawabarikia. Mungu akawaambia, ‘Zaeni, mkaongezeke, mkaijaze nchi na kuitiisha, mkatawale samaki wa baharini na ndege wa angani, na kila kiumbe chenye uhai kiendacho juu ya nchi’”. Kadiri ya Maandiko Matakatifu familia ni taasisi inayounganisha mwanaume na mwanamke, na hawa ndiyo wanaoleta mwendelezo wa uhai wa binadamu wengine na kuunda jamii ya kibindamu inayotawala dunia.

2.1 Nafasi ya Familia katika Agano la Kale

Wayahudi walifurahia na kuheshimu familia, lakini hasa familia pana ilikuwa tunu ya pekee. Kwa namna hii hakukuwa na nafasi ya walea pweke wala watu wa jinsia moja kuoana kwa maana katika hali kama hizo kusingewezekana kujenga familia yoyote. Kupata watoto wengi tangu mapema kulikuwa jambo muhimu na la baraka. Haya ndiyo yanayofafanuliwa na Zaburi ya 127. Zaburi hii inasifia baraka ya kupata watoto wengi mtu angali kijana maana angeliweza kusaidiwa nao mapema, mathalani, kutetewa mahakamani. Mzazi aliruhusiwa kuwatumia watoto wake wa kiume kama mashahidi wa upande wake. Ndipo tunaposoma, “Watoto ni riziki kutoka kwa Mungu Mwenyezi, watoto ni tuzo lake kwetu sisi. Watoto walio na nguvu ni kama mishale mikononi mwake askari. Heri mtu aliye na mishale hiyo kwa wingi. Hatashindwa atakapokabiliana na adui mahakamani” (Zab 127:3-5). Kwa namna hii inaeleweka kwa nini kuzaliwa kwa watoto kulikuwa matukio ya furaha kubwa ndani ya familia.

2.3 Maisha ya Ndoa kadiri ya Sheria ya Kiyahudi

Awali ya yote, Wayahudi walilichukulia suala la kuoa na kuolewa kama amri ya kimungu kwa sababu ya amri iliyotolewa wakati wa uumbaji. Mwa 1:28 ilieleweka kama uanzishwaji wa taasisi ya ndoa na maisha ya familia. Hivi useja uliokuwa ukifanyika huko Qumran lilikuwa jambo la nadra sana. Ni kwa sababu hiyo, Yesu na Paulo, hapo mbele, walipoeleza kwamba mtu angeliweza kuacha kuoa au kuolewa kwa ajili ya ufalme wa Mungu, waliwashtua Wayahudi wengi (rej. Mt 19:1-12, 1Kor 7:1-16. 25-35). Kwa kadiri ya uelewa wa Kiyahudi au wa kirabbi, maisha ya ndoa ndiyo yalikuwa hali mujarabu kwa kila mwanaume na mwanamke. Ndipo, kwa Wayahudi, mtu kuoa au kuolewa lilikuwa wajibu wa kidini. Wayahudi walifundishana kwamba maisha ya familia ndiyo yalikuwa utimilifu wa utu. Hata hivyo, aliyewajibika kuingia katika maisha ya ndoa alikuwa mwanaume siyo mwanamke. Kwa mwanamke haikuwa lazima kuolewa isipokuwa alishauriwa asiishi peke yake. Hivyo ndivyo ilivyotafsiriwa katika Kitabu cha Mwanzo 1:28.  

2.4 Jinsia ya wenye Kuoana

 Je, wenye kuoana wawe watu wa jinsia zipi? Mintarafu watu wa jinsia gani, Biblia nayo haina utata, ni mume na mke yaani watu wawili wa jinsia tofauti. Hao ndiyo watu wanaoweza kuzaana na kutimiza agizo la kuijaza dunia (Mwa 1:28). Matakwa ya Mungu ni watu wawili wa jinsia mbili tofauti. Tena, watu wawili wakitofautiana jinsia ndipo tunapoweza kusema mmoja anaoa na mwingine anaolewa. Wanaume wawili hatuwezi kusema mmoja anaoa na mwingine anaolewa mpaka mmoja ahesabiwe kuwa mume na mwingine ageuzwe kuwa mke, jambo linalogeuza maumbile aliyowatakia Mungu. Watu wa jinsia mmoja ni kama chanya na chanya au hasi na hasi, hawawezi kutimilizana. Mwanamume na mwanamume hawawezi kuwa mwili mmoja wala wanawake wawili hawawezi kuwa mwili mmoja.

Marufuku ya Biblia ambayo hatuna mamlaka ya kuibadili imeandikwa katika Kitabu cha Mambo ya Walawi 18:22-24 hivi, Kamwe usilale na mwanamume mwenzio kama kwamba ni mwanamke. Hilo ni chukizo. Kamwe usilale na mnyama ili usijitie unajisi, mwanamume au mwanamke yeyote kamwe asifanye hivyo, kufanya hivyo ni upotovu.  Msijitie najisi kwa kufanya mambo hayo kwani kwa sababu ya mambo hayo nayafukuza mataifa  yaliyo mbele yenu kwa vile  hufanya hayo na kujitia najisi. Nchi yao ilitiwa najisi nami nikaiadhibu nayo ikawakataa wakazi wake.”

Hii ndiyo kawaida ya neno la Mungu kwenda kimuhtasari.Kumbe, haikuwa lazima kuorodhesha hapa kila aina ya dhambi.Maovu ya aina hii tunayosema yote yanamedokezwa na kumaanishwa hapa. Lakini, kwa kuwa neno la Mungu linapokezana mafundisho, maovu ya sampuli hii, yaani dhambi hizi, zimedokezwa na kukemewa kwa msimamo usioyumba siyo tu katika Agano la Kale bali hata kwenye Agano Jipya. Tunasoma, “Kwa sababu walipomjua Mungu hawakumtukuza kama ndiye Mungu wala kumshukuru bali walipotea katika uzushi wao, na mioyo yao yenye ujinga ikatiwa giza. Wakjinena kuwa wenye hekima walipumbazika,wakaubadili utukufu wa Mungu asiye na uharibifu kwa mfano wa sura ya binadamu aliye na uharibifu, na ya ndege na ya wanyama na ya vitambaavyo. Kwa ajili ya hayo, Mungu aliwaacha katika tamaa za mioyo yao waufuate uchafu, hata wakavunjiana heshima miili yao. Kwa maana waliibadili kweli ya Mungu kuwa uongo, wakakisujudia kiumbe na kukiabudu badala ya Muumba anayehimidiwa milele. Amina.

“Hivyo Mungu aliwaacha wafuate tamaa zao za aibu, hata wanawake wakibadili matumizi ya asili kwa matumizi yasiyo ya asili, wanaume nao vivyo hivyo waliyaacha matumizi ya mke, ya asili, wakawakiana tamaa, wanaume wakiyatenda yasiyopasa, wakapata nafsini mwao malipo ya upotevu wao yaliyo haki yao. Na kama walivyokataa kuwa na Mungu katika fahamu zao, Mungu aliwaacha wafuate akili zao zisizofaa, wayafanye yasiyowapasa…. Wakijua sana hukumu ya haki ya Mungu ya kwamba wayatendao hayo wastahili mauti, wanatenda hayo, wala si hivyo tu, bali wanakubaliana na wayatendao” (Rum 1:21-28,32).

2.5 Nyumba ya Familia: Maisha ya familia yaliwekewa makazi. Heshima ya familia ilikuwa pia kuwa na nyumba, yaani makao. Basi, mintarafu mahali familia zilipoishi, zamani hizo, familia nyingi za Kiyahudi ziliishi kwenye nyumba ndogo ambazo kimsingi zilikuwa chumba kimoja tena kisichokuwa na dirisha (Rej. Lk 15:8). Nyumba ilikuwa haifungwi; stoo peke yake ndiyo iliyokuwa ikifungwa (rej. Mt 6:6). Usiku familia nzima ililala pamoja na kujifunika shuka moja (Rej. Lk 11:7). Kwa kuonesha uhai wa familia, taa za majumbani mwa Wayahudi zilikuwa hazizimwi siku zote. Kuzimika kwa taa hizo kulimaanisha kifo cha familia. Ilikuwa wajibu wa mama kutafuta mafuta taa ya familia isizimike. (Mit 31:18).

2.6 Malezi ya watoto katika imani na maadili kwa Wayahudi: Katika sehemu tuongelee kwa karibu zaidi jinsi Biblia inazungumzia makuzi ya watoto wa Kiyahudi, malezi yao na kufundishwa kwao hata kuwa watu wa imani na maadili stahiki. Tuanzie mwanzoni kabisa, yaani tuanzie tangu kuzaliwa kwa watoto.

2.6.1 Masuala ya Kuzaliwa Mtoto: Mojawapo ya furaha za familia ya Kiyahudi ilikuwa ni kupata uzao. Ndipo familia za Kiyahudi zilifurahia sana ujauzito wa mama kwa sababu zilitambua kwamba ujauzito ulikuwa ndiyo ishara ya Mungu kuwabariki na kuwajalia kushiriki kazi ya uumbaji kwa ajili ya kuijaza dunia (Rej. Mwa 1:27-28). Lakini kwa kutokana na ufinyu wa elimu ya viumbe (biolojia), walikuwa na miiko mingi waliyodhani inalinda ujauzito.

2.6.2 Siku ya Kuzaliwa Mtoto: Siku ya kuzaliwa mtoto ilikuwa na mambo yake pia. Katika siku yenyewe ya kuzaliwa mtoto, wakunga na tabibu walihitajika kumsaidia mwanamke anayezaa katika utungu wake. Wahudumu hao walisamehewa mambo mengi hata shughuli za Sabato. Yaani waliruhusiwa hata kuivunja Sabato.

2.6.3 Malezi ya Watoto: Kimsingi, malezi ya mtoto wa Kiyahudi yalikuwa ya kidini. Kupanga uzazi kuliendana na kipindi cha kunyonyesha. Wayahudi walihimizana kuwanyonyesha watoto wao kwa miaka miwili au mitatu na walipaswa kulelewa kidini kabisa. Watoto walipoanza kusema tu, walifundishwa kutamka mambo matakatifu na majina mbadala ya Mungu, ndiyo Adonai, Maqom, Shem na Shamaim. Mintarafu sala, “Shema” (Kum 6:4-9) ilikuwa ndiyo sala ya msingi. Watoto walipofikisha miaka mitano walifundishwa kusoma Maandiko Matakatifu.

Watoto wa kiume, tofauti na watoto wa kike, walipaswa kuhudhuria masomo ya chekechea kwenye sinagogi ya karibu. Watoto wa kiume walipofikisha umri wa miaka 12 walipaswa kushika sheria ya Musa. Walipofikisha umri huo, walifanyiwa ibada maalumu (Bar Mitzvah) na tangu wakati huo waliruhusiwa rasmi kusoma masomo ya kiliturujia kwenye sinagogi. Shuleni kwao wanafunzi wote walitakiwa kujifunza masimulizi ya tukio la Kutoka Misri.

Injili ya Luka 2:41-45 inasimulia jinsi Maria na Yosefu walivyomlea Yesu Kristo kidini. Walimlea kwa kadiri ya sheria ya Kiyahudi. Utamaduni wa kitalmudi ulielekeza kwamba watoto hata wadogo sana walitakiwa kufika hekaluni wakati wa sikukuu. Ndiyo kisa Yesu hakuachwa pembeni. Kwa kawaida, wavulana walifikia balehe walipofikisha umri wa miaka 12 na ni kuanzia wakati huo walipoanza kuwa huru kwa kiasi fulani. Jambo hili ndilo linaloeleza, siku ile ya kupotea Yesu, kwa nini wazazi wake mwanzoni hawakuwa na wasiwasi sana na mahali alipokuwapo kwa vile “walidhani kuwa yumo katika msafara”. Wazazi hao walianza tu kuhangaika mwishoni mwa safari ya siku moja.  

2.6.4 Malezi Endelevu ya Watoto: Wazazi waliwaanzishia watoto wao, hasa wa kiume, malezi ya imani na maadili au dini kwa ujumla. Baada ya kufundishwa dini nyumbani na kuzoeshwa sala na kuingizwa katika desturi ya kushika sheria ya Musa, watoto wa kiume walipenda wenyewe kujifunza dini kwa kina kutoka kwa marabbi maarufu. Ndipo watoto walipojichagulia wenyewe walimu na kujipatia elimu kutoka kwao. Kujipatia elimu huku kuliitwa “kukaa chini ya miguu ya mwalimu” au “kumfuata mwalimu.” Shuleni, ndiyo katika kumfuata mwalimu, Myahudi alijifunza sheria ya Musa, historia ya kutoka Misri, namna ya kufafanua Torati, mambo ya imani kwa ujumla na maadili. Kwa kufundishwa maadili, Wayahudi walitumia vitabu vya hekima, hususan, kitabu cha Yoshua ben Sira, kama vitabu vya kiada.

Ndani ya vitabu vya Hekima Wayahudi walifundishwa mambo mbalimbali, mathalani, mambo ya kuwaheshimu watu, kulea watoto, kazi, urafiki, afya, furaha, nidhamu katika kunywa divai, ukweli wa mateso, ukweli wa kifo, ujasiri na sifa za watu wa zamani, utawala, umuhimu wa hekima na kadhalika. Mambo hayo yalifundishwa kwa mitindo ya kukaa pamoja kwa amani, kuulizana maswali, kujadiliana na kupeana mifano. Mtu alikaa chini ya miguu ya mwalimu au alimfuata mwalimu kwa takribani miaka 38 ndipo alipofuzu na mtu akawa Farisayo au Mwandishi wa sheria. Aliyefuzu kama Farisayo aliweza kuwa mwalimu na yeye kufuatwa na wanafunzi wa kwake. Aliyefuzu kama Mwandishi wa sheria aliweza kuwa mnakili vitabu vitakatifu na kufanya kazi za uwakili au uhakimu. Hata hivyo, matokeo ya jumla ya kujiendeleza katika dini yalikuwa kila baba kuweza kumudu vyema shughuli ya kuisimamia familia yake katika kuikuza, kuilea na kuidumisha katika mambo ya dini kama tulivyoona wajibu za baba.

2.6.5 Ukomo wa Watoto Kuwatunza Wazazi Wao: Watoto walipaswa kuwatunza wazazi wao maisha yao yote, yaani mpaka kufa kwao (rej. Mit 23:22 na YbS. 3:1-16). Kutokuwa na mwisho kwa wajibu huo wa kuwatunza wazazi ndiko kulikowafanya watoto jeuri au wakorofi kutumia vibaya kanuni ya “korbani”, yaani kuweka wakfu mali zao ili kukwepa kuzitumia katika kuwatunza wazazi wao (rej, Mk 7:9-13). Kanuni hiyo ilisema mtu akiweka mali yake wakfu, yaani kumwekea Mungu, alikuwa haruhusiwi kuitumia kuwasaidia wala kuwatunzia wazazi wake.  Kwa namna hii kanuni hii ilitumika vibaya na Yesu alifuta tabia hii (rej. Mk 7:8-13).

Kutokana na ukweli wa wajibu wa watoto kuwatunza wazazi wao mpaka kufa kwao, tunapata ushahidi kwamba Yesu alikuwa mtoto wa pekee kwa Bikira Maria na Yosefu, maana kama angelikuwa na kaka na dada zake wa damu, Yesu asingelimkabidhi mama yake kwa mwanafunzi aliyempenda. Kama wangelikuwapo ndugu zake wa damu, Yesu angelipata urahisi mkubwa wa kuwakumbusha wajibu wao wa kumtunza mama yao mpaka kufa kwake. Tena mahangaiko hayo hayo ya Yesu, ya kumkabidhi mama yake kwa mwanafunzi aliyempenda, yanatudokezea kwamba wakati Yesu anakufa, Yosefu alikuwa ameshakufa, vinginevyo asingelithubutu kumtenganisha mama yake na baba yake huyo (rej. Yn 19:25-28).

2.6.6 Uonevu kwa Akinamama: Maisha ya ndoa ya Kiyahudi yalihusisha mambo mawili magumu, talaka na kurithi wajane. Kati ya Wayahudi kulikuwa na uonevu mkubwa uliojengwa juu ya maisha ya ndoa. Wayahudi walipojaribu kufafanua Kumbukumbu la Torati 24:1-4 iliyotoa ruhusa mume kumwandikia talaka mkewe na kumfukuza toka nyumbani mwake, yaani kumwacha, marabbi wawili wakubwa waliwagawanyisha watu. Suala lenyewe lilikuwa juu ya maana ya “neno ovu” (erwat dabar) ambalo lilimruhusu mume kumwacha mkewe kwa sababu yake.  Rabbi Hillel aliwafundisha Wayahudi kwamba waliruhusiwa kuwaacha wake zao kwa sababu yoyote (erwat dabar) walioiona wenyewe kuwa nzito. Rabbi Shamai hakuleta nafuu yoyote maana naye aliruhusu talaka ingawa yeye alisisitiza kuwepo sababu nzito inayohusiana na kuonekana kwa uchi wa mke, kama vile, ugoni au kuvaa ovyo mbele ya watu.

Kuhusu hili, hata Yesu mwenyewe alipinga sana desturi ya talaka kama tunavyosoma katika Maandiko Matakatifu; “Wafarisayo kadhaa walimjia, wakamwuliza kwa kumtega, “Je, ni halali mume kumpa talaka mkewe kwa kisa chochote?” Yesu akawajibu, “Je, hamkusoma katika Maandiko Matakatifu kwamba Mungu aliyemuumba mtu tangu mwanzo alimfanya mwanamume na mwanamke, na akasema: kwa sababu hiyo mwanamume atamwacha baba na mama yake, ataungana na mke wake nao wawili watakuwa mwili mmoja?” Kwa hiyo wao si wawili tena bali mwili mmoja. Basi alichounganisha Mungu, binadamu asitenganishe!”  (Mt. 19:3-6). Shauri la kurithi wajane lilikuwa la ajabu sana. Wayahudi walikuwa wanahimizana kurithi wajane kwa sababu walau tatu. Mosi, walitaka kuhakikisha mali ya ndoa iliyokoma kwa kifo cha mume haiendi mbali. Pili, walikusudia kumsitiri mjane asifikwe na taabu sana.

Tatu kwa kuwa waliamini kwamba Mungu atakuwa anawataka watu walioona ushahidi wa kumwonesha mtoto waliomzaa walitaka kutatua tatizo la kukosekana ushahidi wa aina hiyo kwa watu waliopata bahati mbaya ya kutokuwa na mtoto walipoishi pamoja. Ilikuwa kwamba kama kaka alimwacha mjane pasipo mtoto, ndugu yake au jamaa yake alipaswa kumchukua mjane na kumzalia mtoto, mtoto alihesabika kuwa mali ya marehemu (rej. Kum 25:5-10). Jambo hili liliwakandamiza akina mama kwa sababu waliweza kufedheheshwa kwa kukataliwa na shemeji au ndugu za marehemu na pengine alitakiwa kumgonja shemeji mdogo akue hadi aweze kuamua kumchukua au kutomchukua. Kuhusu kurithi wajane, Yesu katika Luka 20:27-38 alijibu swala la Mjane kuwa ni mke wa nani baada ya ufufuko.

2.6.7 Majumuisho ya Maelezo ya Agano la Kale

1.     Kuthamini familia: Maisha ya familia yalithaminiwa sana na Wayahudi hivyo kuoa na kuolewa zilikuwa hali zilizotegemewa kutokea katika maisha yao.

2.     Kutayarisha uchumba mwema: Waliotarajia kuoana walijipatia kipindi cha walau mwaka mmoja kujiandaa kwa maisha ya familia.

3.     Kufunga ndoa vizuri: Maisha ya familia yalianzishwa rasmi siku ya harusi, bibi harusi alipoingizwa nyumbani mwa bwana harusi.

4.     Kukataa mahusiano ya kujamiiana kati ya ndugu: Mipaka ya kujamiiana iliainishwa katika Torati ya Musa (rej. Law 18).

5.     Kukataa mahusiano ya kujamiiana yasiyo ya kawaida: Kujamiiana kinyume na maumbile au na wanyama kulikatazwa na Torati (rej. Law 18).

6.     Kukataa ndoa za jinsia moja: Watu wa jinsia moja walikatazwa kujamiiana sembuse kuoana.

7.     Kudumu katika maagano ya ndoa: Kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao, Musa aliwaruhusu Wayahudi kuachana, lakini ilikuwa kinyume na matakwa ya Mungu (Kum 24:1-4, Mt 19:1-12).

8.     Kutunza usafi na utakatifu wa ndoa: Ugoni ulipata adhabu kali. Aliyefumaniwa alipewa adhabu ya kupiga mawe hadi kufa.

9.     Kutunza mimba vyema: Mimba zilitunzwa kwa miiko kadhaa iliyopaswa kushikwa na mama mjamzito.

10. Kuangaliwa watoto na kupewa majina mazuri: Watoto waliangaliwa sana, wakanyonyeshwa kwa kipindi cha kufaa na walipewa majina yenye maana fulani kusudi wapate kuhamasika na sifa zinazoendana nayo.

11. Kupanga uzazi: Miaka miwili au mitatu ya kunyonyesha watoto ndiyo iliyowatumika kupanga uzazi. Idadi ya watoto haikuwa na ukomo.

12. Kulea watoto vyema: Watoto walilelewa na wazazi wote wawili, lakini baba aliwaangalia watoto wa kiume kwa namna ya pekee na mama watoto wa kike. Mintarafu kusoma, watoto wa kiume walijichagulia wenyewe walimu wa kuwafundisha Torati kwa kina.

13. Wanafamilia kutunzana na kushika majukumu husika: Wanafamilia waligawana majukumu. Baba alikuwa na majukumu yake na mama sawia. Hata watoto walikuwa na yao.

14. Kusaidiana kwa udumifu: Wazazi waliwalea watoto mpaka walipoanza maisha ya familia wenyewe. Kutoka hapo kazi iliwageukia watoto kuwatunza wazazi wao mpaka walipoaga dunia. Watoto kukwepa majukumu ya kuwatunza wazazi wao kwa kuweka mali zao wakfu (“korbani”) ilikuwa ni uhuni wa kusikitikiwa.

15. Kutoachana ovyo: Ijapokuwa talaka iliruhusiwa, ugumu wa kulipa mahari ulipunguza talaka za ovyo ovyo. Mara nyingi ni kifo kilichomaliza maisha ya ndoa.

2.6.8 Usafi wa Ndoa na Maisha ya Familia.

Ya kwamba ndoa inatakiwa kuwa na usafi wa pekee inadokezwa katika maneno ya Kristo pale alipokuwa anajibu swali aliloulizwa na Mafarisayo kama ni kweli kwamba waume wanaweza kuwapa talaka wake zao na kuwaacha kwa sababu yeyote. Yesu alifuta misimamo ya akina Hillel na Shammai akisisitiza kwamba agano la ndoa halifunguliki (Mt 19:3-6). Kwa kusema hivyo alimaanisha vile vile kwamba ndoa ni agano la watu wawili tu, mume mmoja na mke mmoja. Kwa kusema hivyo alionesha uharamu wa mitara. Hapo hapo kwa kusema hivyo alidokeza uharamu wa mahusiano yoyote yasiyozingatia jinsia hizo tofauti za mume na mke. Na hiyo maana yake lilikuwa dokezo la uharamu wa mahusiano yote yaliyo kinyume na mume na mke, yaani mahusiano kama ya mwanaume na mwanaume, mwanamke na mwanamke au mwanadamu na hayawani. Aidha, maneno yake hayo yalifunga mwanya wa mtu kujibadili jinsia au mtu kujitengeneza ili awe na jinsia zote mbili. Haya yote yanasomeka katikati ya mistari ya Mt 19:1-12. Soma aya hizi huku ukitafakari vyema nawe utaona jinsi kina chake kilivyo kirefu.

2.6.9 Utakatifu wa Ndoa na Maisha ya Familia

Mintarafu utakatifu wa ndoa na maisha ya familia yanatafsirika katika mlinganisho wa mahusiano ya kindoa au maisha ya familia. Tumeshadokeza kwamba mlinganisho huo umo katika Agano la Kale. Mungu amelinganishwa na bwana harusi na Israeli na bibi harusi wake katika Hos 1:2-9. Mlinganisho huu hauwezi kuwa mchafu, ndiyo maana ni ishara ya utakatifu wa maisha ya ndoa na maisha ya familia. Ndiyo maana basi Agano Jipya halisiti kutumia mlinganisho huo huo lilipoingia suala la mahusiano ya Yesu na Kanisa lake. Yesu amelinganishwa na bwana harusi na Kanisa na bibi harusi katika Agano Jipya (Rej. Efe 5:21).

Katika Agano Jipya, Mwana wa Mungu, Neno aliyefanyika mwili (Rej. Yn 1:14) katika tumbo la Mama Bikira, aliishi na kukua katika familia ya Nazareti, na alishiriki matukio ya kijamii akionesha nafasi yake kama Mungu Mtu katika jamii. Kwanza kabisa katika harusi ya Kana aliitunukia sherehe “ishara” yake ya kwanza (Rej. Yn 2:1-11) ya kugeuza maji kuwa kinywaji bora cha divai kwa washerehekeaji wa harusi. Yeye pia alipokea kwa furaha kukaribishwa na wanafunzi wake wa kwanza katika familia zao (Rej. Mk 1:29-31; 2:15-17), na aliifariji familia ya rafiki zake huko Bethania wakati wa msiba (Rej. Lk 10:38-42; Yn 11,1-44).

Hivyo basi, kwa kushiriki katika maisha ya kifamilia, Yesu alitengeneza upya uzuri wa ndoa kwa kutangaza tena mpango mzima wa Mungu, uliokuwa umeachwa kwa sababu ya ugumu wa mioyo ya watu (Rej. Mt 5:31-32; 19:3-12; Mk 10:1-12; Lk 16:18). Kwa kurudia kwenye mpango wa asili, Yesu aliufundisha umoja na uaminifu wa wanandoa, akikataa talaka na uzinzi. Hasa kwa kupitia uzuri wa ajabu wa upendo wa kibinadamu – ambao ulikuwa umeshaadhimishwa katika Wimbo Ulio Bora kwa mikazo iliyovuviwa – na kwa kupitia uzuri wa kifungo cha ndoa – kilichodaiwa na kulindwa na Manabii kama Hosea (Rej. Hos 1:2, 3:3) na Malaki (Rej. Mal 2:13-16). Yesu aliithibitisha hadhi ya asili ya upendo wa kindoa wa mwanamume na wa mwanamke.

Naye Mtume Paulo ameelezea kwa undani kuhusu Familia iliyokwisha kupokea Enjili ya Yesu Kristo, katika nyaraka zake kadhaa, hususan kuhusumshikamano thabiti baina ya waume na wake, baina ya wazazi na watoto, na baina ya wenye nacho na walio maskini (Rej. Efe 5:21-6:9; Kol 3:18-4:1; 1Tim 2:8-15; Tit 2:1-10; 1Pet 2:13-3:7; Rej.pia Waraka kwa Filemoni).

Kwa namna ya pekee, Waraka kwa Waefeso unatambua upendo wa kindoa baina ya mwanamume na mwanamke kama “siri kubwa”, inayodhihirisha duniani upendo wa Kristo na wa Kanisa (rej. Efe 5:31-32). Hata katika jumuiya za awali za Kikristo familia ilionekana kuwa “Kanisa la nyumbani” (rej. KKK na. 1655), ambalo lilikuwa mahali pa mshikamano thabiti baina ya waume na wake, baina ya wazazi na watoto, na baina ya wenye nacho na walio maskini (Rej. Efe5:21-6:9; Kol 3:18-4:1; 1Tim 2:8-15; Tit 2:1-10; 1Pet 2:13-3:7; rejea pia Waraka kwa Filemoni). Hususan, Waraka kwa Waefeso unatambua upendo wa kindoa baina ya mwanamume na mwanamke kama “siri kubwa”, inayodhihirisha duniani upendo wa Kristo na wa Kanisa (Rej. Efe 5:31-32).

Ndiyo maana Mt. Paulo katika waraka wake kwa Waefeso, anasisitiza kwamba “kila mtu mmoja-mmoja kati yenu na ampende hivyo mke wake kama vile anavyojipenda mwenyewe; kwa upande mwingine, mke anapaswa kumheshimusana mume wake.  Enyi watoto, watiini wazaziwenu katika muungano na Bwana, kwa maana hilo ni jambo la uadilifu: “Mheshimu baba yako na mama yako”; ambayo ndiyo amri ya kwanza yenye ahadi: “Ili mambo yakuendee vema nawe ukae muda mrefu duniani.” Nanyi, akina baba, msiwe mkiwakasirisha watoto wenu, bali endeleeni kuwalea katika nidhamu na mwongozo wa akilini wa Bwana. (Waefeso, 5:21-6:4)

2.6.10 Malezi Bora: Ukweli kwamba maisha ya ndoa au familia yanaushuhudia Ukristo, unakuwa ni thabiti endapo tu mume na mke wanapendana kikristu na watoto wanapewa malezi bora. Maisha ya ndoa yataushuhudia ukristo endapo watoto waliomo ndani yake wanalelewa na kuelimishwa kikristo. Maana yake watoto wanafundishwa sala, wanapewa elimu ya dini na wanakuzwa kama waamini.

2.6.11 Hadhi ya Sakramenti: Katika Agano Jipya Yesu ameipa hadhi ndoa kuwa sakramenti, yaani tendo la wanandoa katika Kristu linakuwa ni njia yao ya kujitakatifuza na kumtukuza Mungu yaani njia ya wokovu. Kwa kitendo cha Yesu kukubali kuhudhuria sherehe ya harusi huko Kana na kwa ombi la mama yake kukubali kuwaongezea furaha wanaharusi na wageni waalikwa wote kwa kuwageuzia maji kuwa divai (Yoh. 2: 1-11), ndoa iliongezewa hadhi hata kuwa kitu kibarikiwa na chanzo cha neema kwa wanaooana, yaani ndiyo kuwa Sakramenti. Hivi simulizi la muujiza wa Kana ndiyo rekodi ya kuasisiwa kwa sakramenti ya Ndoa. Kwa maana hiyo, ndoa au maisha ya familia yana kibali mbele ya Mungu na wote watakaoyapokea maisha hayo kwa usafi na uelewa watafikishwa mbinguni kwayo.

2.6.12 Kufutwa kwa Talaka na Desturi ya Kurithi Wajane: Yesu alikabiliana kwa uchungu na uonevu wa akinamama. Kufutwa kwa talaka na desturi zenye uonevu, uliojengwa juu ya maisha ya ndoa, kulianzisha enzi mpya kwa akina mama. Yesu aliona jamii ya Wayahudi ikiwakandamiza wanawake kwa masuala kadhaa ya kifamilia. Mawili makubwa kati ya hayo, yalikuwa talaka na wajane kurithiwa. Yesu alitangaza kutokuwepo kwa mwanya wa talaka (Mt 19:1-12) na desturi ya kurithi wajane (Mt 22:23-33).

SEHEMU YA TATU

 3.0 FAMILIA SHULE YA IMANI NA MAADILI

Familia nyingi za Kiyahudi zilifuzu kuwa shule za imani na maadili. Zilifundisha imani zikawa shule za imani. Zilifundisha na kuhimiza maadili zikawa shule za maadili mema. Sasa ni zamu ya familia zetu katika kudumisha Ukristo. Familia zetu zikifundisha watoto dini, kuanzia na kumwamini Mungu wa kweli ambaye ni Baba, Mwana na Roho Mtakatifu kadiri alivyodhihirishwa na Yesu wa Nazareti, Mkombozi pekee wa binadamu wote, watoto hawa wakawa watu wa sala na ibada za kumwabudu Mungu, hakika familia zetu zitakuwa shule za imani. Zaidi sana familia zikafundisha na kuhimiza utu wema, kufanya mema na kuyakataa mabaya, zitakuwa shule za maadili.

Tumeshaona ili familia zifuzu kuwa shule za imani na maadili ni lazima zenyewe ziundwe na wenza walioleleka vyema katika hayo hayo wanayowajibika kuwapa watoto wao. Hivi ni jambo muhimu kukazia mafundisho ya misingi ya imani na maadili mema kwa wanandoa na wazazi wenyewe. Hakuna mtu anayeweza kutoa kitu ambacho yeye mwenyewe hana. Hivyo, kabla ya ndoa na wakati wote wa ndoa ni lazima wazazi kupewa mafundisho juu ya imani yao kupitia Katekisimu ya Kanisa Katoliki, na hili lifanyike kwa njia mbalimbali zikiwemo semina ili wajue na watimize majukumu yao na wahimizwe kuyatimiza kikamilifu. Wajawe na fadhila zitakazo wasaidia kupendana, kuvumiliana, kusameheana na kusaidiana. Na hivi wajengewe uwezo wa kuwalea watoto wao kadiri ya miongozo ya Kanisa Katoliki.

 Familia zenye kuwajibika hujitahidi kuhakikisha watoto wao wanalelewa vizuri kabla ya kwenda kusoma shule ya msingi na kisha kuingia shule kuwasindikiza kwa malezi mazuri. Familia nzuri hazikubali malezi ya watoto wao yakatikie njiani maana hunuia kuwasaidia watoto wao waingie mbinguni pia. Mahali pengine, zamani, watoto wa Kikristo walikuwa wakipata mafundisho kutoka kwa wazazi wao, hususan, katekisimu, sala, ibada na namna ya kuheshimu wengine. Baada ya hapo walipelekwa kwa makatekista na masista kupata mafunzo kamili ya katekesi na kupatiwa mafundisho ya sakramenti za msingi, yaani Ubatizo, Ekaristi, Kipaimara na Kitubio. Yalikuwa malezi mazuri sana; laiti familia nyingi zingerudi huko!

Matokeo ya kupata mafundisho nyumbani na kisha kufundishwa dini na makatekista na masista ni watoto husika kukomaa vyema tayari kwa kuanza masomo ya “elimu dunia” katika shule ya msingi, sekondari, vyuo na vyuo vikuu.  Watoto waliokomazwa kwenye familia zao huwa vigumu kupeperushwa na mafundisho ya kigeni wanapokuwa wakubwa. Pasipo kusahau, kama ilivyokuwa katika familia za Kiyahudi, walimu wakuu na wazuri sana katika masuala ya dini nyumbani ni akina mama. Akina baba huchukuliwa mno na pilikapilika za kutafuta chochote kwa ajili ya familia. Kumbe, katika familia yoyote, mama anapoamua na kutimiza vyema wajibu wake wa kuwafundisha dini watoto wao, dini hustawi sana kwa vile watoto “hukamatika” vizuri sana.

Kimalezi, mtoto anayekamatwa na kulelewa vizuri katika miaka sita ya mwanzo hukua kwa misingi bora kabisa. La sivyo, uzembe au kuchelewa kokote ndani ya miaka hiyo hufadhaisha juhudi za malezi za hapo mbele. Matokeo ya jumla huwa kutokea kwa watoto sugu wasiojali imani wala maadili wakawa hawana faida kwa Kanisa na hata kwa wazazi wenyewe. Na katika matokeo hayo huwa haifai wazazi kulalamika maana mchimba shimo huingia mwenyewe.

3.1 Utume wa Familia katika kukuza Imani

Familia ya Kikristo hutekeleza wajibu wake wa kinabii kwa kukaribisha na kulitangaza Neno la Mungu ndani ya familia. Kwa kufanya hivyo kila siku, inakuwa ni jumuiya inayoamini na yenye kuhubiri. Watu wa ndoa walio wakristo na wazazi wanapaswa kuonesha utii wa imani kwa kulikaribisha Neno la Bwana lenye kuwafunulia Habari Njema inayohusu maisha yao ya ndoa na familia yao kwa ujumla. (Rej. Dei Verbum no. 1). Maandalizi yenyewe ya Ndoa ya Kikristo ni safari ya imani.  Ni safari ya pekee kwa wachumba kugundua na kuongeza kina cha imani iliyopokewa katika ubatizo na kulishwa kwa malezi ya Kikristo.  Kwa njia hii wanatambua na kupokea kwa hiari wito wao na kumfuata Kristo na kutumikia Ufalme wa Mungu katika hali ya ndoa.

Vilevile adhimisho la Sakramenti ya ndoa ni muda wa msingi wa imani ya watu wa ndoa.  Sakramenti, katika umaana wake, ni utangazaji wa Habari Njema kuhusu pendo la ndoa. Mungu mwenye kuwaita mume na mke kwa ndoa huendelea kuwaita waiungame imani yao hata wanapokabiliana na matatizo, shida na hali za maisha kila siku zilivyo. Kwa kuitafakari “Habari Njema” Mungu huwajia wanandoa akifunua na kuwaonesha “matwaka” halisi ya kushiriki kwao katika pendo la Kristo kwa ajili ya Kanisa lake ndani ya familia yao na jamii.

Kama asemavyo Papa Paulo VI “Familia kama vile Kanisa budi pawe ni mahali ambapo Injili hupitishwa; na baadaye hiyo Injili hutufanya nuru yake katika familia ambayo ina ufahamu wa utume huu. Wanajumuiya wote wanahubiri na kuhubiriwa habari njema.  Wazazi sio tu wanawashirikisha Injili watoto wao, bali toka kwa watoto wao wanaweza kupokea Injili ileile kama wanavyoishi wao wenyewe kwa undani. Familia ya namna hii huwa ni mhubiri kwa familia nyingine zilizo nyingi. (Evangelii Nuntiandi, no. 71). Hii ni kutimiza amri ya Kristo iliyo wazi,: “mkahubiri Habari Njema kwa kila mtu (Mk. 16:15).

Sakramenti ya ndoa pia hubeba jukumu la kutetea na kueneza imani; kazi ambayo ina mizizi yake katika ubatizo na kipaimara (Lumen Gentium, no. 11) na huwafanya mume na mke na wazazi wakristo wawe mashahidi wa Kristo hata kwenye mipaka yote ya dunia (Mdo.1:18); wawe wamisionari katika maana ya kweli na yenye kuongozwa na upendo wa Kristo.

Umisionari ndani ya familia waweza vilevile kutekelezwa hasa pale inapotokea mwanajumuiya wa familia hana imani au haishi kwa uthabiti. Katika hali ya namna hii wanajumuiya wengine lazima watoe ushuhuda kwa jinsi wanavyoishi imani yao wenyewe ili kumtia nguvu na kumsaidia mwenzao katika njia ya kuelekea ukubali kamili wa Kristo Mwokozi (1 Petro 3:1-2).  Na hapo ndipo Kanisa la nyumbani huwa ishara ya uwepo wa Kristo na wa pendo lake kwa wale ambao wako mbali sana na mambo ya Kimungu. Ushuhuda huu pia huwafikia familia ambazo bado haziamini na vilelvile familia za Kikristo ambazo haziishi kufuatana na imani waliyoipokea wakati wa ubatizo (Ad Gentes no. 39). Kwa namna hii, familia ya Kikristo ambayo ina wajibu wa kikuhani hualikwa kutakatifuzwa na kutakatifuza jumuiya ya kikanisa na ulimwengu. Aidha Sakramenti ya ndoa huwapa wanandoa neema na jukumu la kimaadili ya kuyabadilisha maisha yao yote kuwa “sadaka ya kiroho” (Rej. 1Pet. 2:5; Lumen Gentium no. 34).

3.2 Wanandoa na Ekaristi: Ekaristi ambayo ni zawadi ya mapendo, ni msingi wa ushirika wa familia ya Kikristo. Kwa kushiriki Ekaristi, wanandoa wa familia ya kikristo wanafanywa mwili mmoja, wenye kufundisha na kushiriki katika umoja mpana zaidi wa Kanisa. Kushiriki kwao katika mwili wa Kristo ambao umetolewa na katika Damu yake ambayo imemwagwa pale msalabani, huwa ni chanzo kisichokwisha cha nguvu ya ushuhuda wa maisha ya Kristo mfufuka aliyeshinda dhambi na mauti.

3.3 Wanandoa na Sakramenti ya Kitubio: Familia ya kikristo inawajibika kujitakatifuza hasa kwa kuitikia mwaliko wa Kristo wa kuongoka kila siku kwa kutekeleza agizo lake la “Tubuni na kuiamini Injili” (Mk.1:15). Mtaguso wa Pili wa Vatikano kwa kuhimiza umuhimu wa sakramenti ya kitubio kwa sehemu inayohusu “Maisha ya Binadamu” unaagiza: “Na kama dhambi itazidi kuwashika, wasikatishwe tamaa bali zaidi wakimbilie kwa uthabiti na unyenyekevu huruma ya Mungu ambayo humiminwa kwa thabiti katika Sakramenti ya Toba” (Sacrasanctem Consilium no. 60). Hivyo basi wanandoa wanahimizwa kutumia neema za Sakramenti ya kitubio ili waweze kudumu daima katika kudumisha maagano yao ya ndoa.

3.4 Familia ni Jumuia ya Sala: Pamoja na msaada wa sakramenti ya kitubio, mabadiliko yoyote ya kiroho hupatikana kwa njia ya maisha ya sala. Lengo la sala ya familia ni kuimarisha maisha yenyewe ya familia.  Ndiyo maana wakati wa ibada ya ndoa kwenye sala ya waamini tunawaombea waliofunga ndoa tukisema, “…daima wasali pamoja na kuombeana kwa Mungu” na nyumba yao iwe Kanisa ndogo: Familia yao iwe msingi kwa taifa (Rejea – Ibada ya Ndoa – SALA YA WAAMINI). Kwa sababu ya heshima ya utume wao, wazazi wakristo wanao wajibu wa pekee wa kuwalea watoto wao katika sala. Katika Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatikano tunaambiwa: ‘Ni hasa katika familia ya kikristo ikipatanishwa kwa neema na msaada wa Sakramenti ya ndoa, kwamba toka miaka ya awali kabisa watoto budi wafundishwe kufuatana na imani ile waliyopewa katika ubatizo wawe na elimu ya Mungu, waweze kumwabudu Mungu kwa njia ya sala na kuwapenda jirani zao (Gravissimum Educationis no. 3).

Sala hufanya sehemu kubwa ya maisha ya kikristo yaeleweke katika ukamilifu na umaana wake.  Sala vile vile ni sehemu muhimu ya ubinadamu wetu wenyewe; ni maelezo ya kwanza ya ukweli wa ndani wa mtu, hali ya kwanza kwa uhuru halisi wa roho (Yohane Paulo II, Hotuba kwenye Madhabahu ya Montrella (29 Oktoba 1978): Mafundisho ya Yohani Paulo II (1978), 78-79). Sala huunganisha familia ya Kikristo katika maisha ya Kanisa na Kristo aliye mzabibu wa kweli na wenye kuzaa sana (Apostolicam Actuositatem no.4).

3.5 Familia na Liturujia: Pamoja na kwamba familia ya kikristo itaadhimisha nyumbani sala za faragha; ni wajibu ikawa pamoja na  wanajumuiya wenzake kushiriki maadhimisho ya kilitrujia kama zilivyo nyakati na sikukuu za mwaka wa kiliturjia. Mazoezi haya ya kiliturjia ndiyo yatakayowawezesha wanafamilia kukua na kukomaa kiroho, kiimani na kimaadili.

3.6 Familia ni jumuiya ya watu: Katika ndoa na katika familia uhusiano kati ya watu husimikwa; maisha ya mume na mke, ubaba na umama, hali ya kuwa ndugu ambamo binadamu huingizwa katika “familia ya kibinadamu” na katika “familia ya Mungu” ambayo ni Kanisa hukamilika. Ndoa ya Kikristo na familia ya Kikristo hujenga Kanisa. Katika familia binadamu hapati tu uhai wa kuishi bali pia huingizwa katika jumuiya ya kibinadamu kwa njia ya malezi na makuzi. Kwa njia ya ubatizo na kuelimishwa katika imani, mtoto hupata kuingizwa katika familia ya Mungu iliyojengwa na Kristo ambaye ni kichwa cha Kanisa.

3.7 Jukumu la Familia ya Kikristo: Mungu huitaka familia ya Kikristo kutekeleza jukumu ambalo katika historia hutokana na hali ya familia ilivyo; jukumu ambalo laonesha maendeleo thabiti na yenye uhai. Kila familia sharti ijionee yenyewe ule wito ambao hauwezi kupuuziwa, ambao hupambanua hadhi yake na wajibu wake. Hapa mambo mawili yanahusika: (i) Familia sharti irudi vyema kwenye mwanzo wa tendo la Mungu la kuumba (Mw. 1:26-27, 28) ndipo itaweza kufikia lengo lake la kujijua na utimilifu wake katika historia ya uumbaji. (ii) Familia sharti itambue kuwa ina utume wa kuwa zaidi na zaidi jinsi ilivyo, yaani kuwa jumuiya ya maisha ya mapendo, katika jitihada itakayoiwezesha kupata utimilifu, katika ufalme wa Mungu. Kwa hiyo jukumu kubwa la familia ya Kikristo ni ule utume wa kulinda uhai, kufunua na kushirikisha upendo halisi katika pendo la Mungu kwa wanadamu.

3.8 Kujenga Jamii kwa Njia ya Upendo wa Kifamilia: Familia ambayo imeanzishwa na kupata uhai kwa njia ya pendo, ni ushirika wa watu, yaani wa mume na mke (wazazi) na watoto na ambao wanaunda jamaa moja.  Kazi yake ya kwanza ni kuishi kwa uaminifu ule ukweli wa ushirika katika juhudi thabiti ya kukuza jumuiya halisi ya watu.   Bila upendo, familia siyo jumuiya ya watu, na kwa namna hiyo haiwezi kuishi, kukua na kujikamilisha yenyewe kama jumuiya ya watu. Kama Mt. Papa Yohani Paulo II asemavyo: “Mtu hawezi akaishi bila upendo.  Hubakia kiumbe kisichotambulikana kwa chenyewe, uhai wake hauna maana, ikiwa upendo haukufunuliwa kwake, ikiwa hakutani na upendo, ikiwa haonji na kuufanya uwe wake, ikiwa hashiriki kwa moyo ndani yake” (Redemptor Hominis no. 10). Yesu pia aliagiza kupitia amri mpya: “Pendaneni kama nilivyowapenda ninyi; mkipendana watu wote watajua kwamba ninyi ni wanafunzi wangu” (Yoh. 13: 34-35).

3.9 Umoja usiogawanyika kati ya Mume na Mke: Kwa nguvu ya agano la maisha ya ndoa mwanaume na mwanamke hawako tena wawili bali mwili mmoja (Mt. 19: 6; Mw. 2: 24); na wanaitwa kuendelea kukua katika ushirika wao kwa njia ya uaminifu wa siku hata siku kwa njia ya ahadi yao ya ndoa. Kwa mantiki hiyo ni wajibu wa kimsingi wa Kanisa kutilia mkazo, na tena kwa nguvu, mafundisho juu ya kutotenguliwa kwa ndoa. Yesu mwenywewe amesema, “Basi alichokiunganisha Mungu, binadamu asitenganishe(Mt.19:6).  Ni vizuri mume na mke, kwa kupitia Sakramenti ya ndoa na kwa kujengewa moyo mpya, wawe na uwezo wa kushinda ugumu wa mioyo yao (Mt.19:8); na juu ya yote wawe na uwezo wa kushiriki upendo kamili wa Kristo.

3.10 Familia huunda Kanisa la Nyumbani: Ushirika wa mume na mke huweka msingi wa ushirika mpana zaidi wa familia: wazazi na watoto, kaka na dada, pamoja na kila mmoja anayehusiana na familia hiyo. Familia ya Kikristo huleta ufunuo halisi wa utimilifu wa ushirika wa kikanisa, na ni kwa sababu hii familia huitwa “Kanisa la nyumbani” (Lumen Gentium No.11.). Wanafamilia kila mmoja kwa kadri ya karama yake, wanao wajibu wa kujenga “shule ya ubinadamu wenye kina zaidi (Gaudium et Spes, no. 52); na hilo hutokea palipo na uangalizi wa upendo kwa wadogo, vijana (hasa kwa upande wa malezi), wagonjwa, wazee, na pale ambapo pana uhitaji wa huduma ya upendo kila siku kwa yeyote yule (Rej.Efe: 6: 1-9).

Pamoja na kuyaangalia mahitaji ya wanafamilia wengine, tunaalikwa katika kipindi hiki kuwaangalia wanafamilia walio watoto na vijana hawa kwa sasa wanahitaji sana mifano ya tabia nzuri za kiutu na ubinadamu ulivyonyanyuliwa na Kristo. Wazazi wanaagizwa kuwapa watoto mifano ya tabia njema kimatendo, desturi na mazoea ili waweze kujenga mfumo wa maadili mema kijamii. Viongozi wa serikali na wa Kanisa wanawajibika kuwa mifano ya baba na mama mwaadilifu ili wawe kielelezo kwa wazazi na walezi wengine kama vile Yesu alivyoonyesha alipokuwa kati ya wanafamilia huko Nazareti, alisema: “Waacheni hao watoto waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana utawala wa Mungu ni wao(Lk:18:16). Utume huu unamjali mtoto hata kabla ya kuzaliwa yaani toka dakika ya kwanza ya kutungwa mimba na kisha muda wote wa miaka ya uchanga na ujana.

3.11 Wazee katika Familia: Wazee katika familia wanatarajiwa kuwa mashahidi wa mila nzuri na wenye kudhihirisha jinsi Injili ilivyoweza kumtengeneza mfuasi aliyekomaa wa Yesu. Wao ni chanzo cha hekima na busara kwa vijana na kwa wakati ujao. Shughuli za kichungaji za Kanisa sharti zisaidie kugundua na kutumia vizuri darasa la wazee katika jumuiya za kiserikali na kikanisa hasa katika familia. Tujue kwamba maisha ya wazee husaidia kudhihirisha tunu za binadamu; huonesha mfululizo wa vizazi na huonesha kutegemeana kwa watu wa Mungu. Kwa mantiki hiyo tuwasaidie wazee wetu katika uzee wao; na wala tusiwahuzunishe; hata wakiwa wamepungukiwa na ufahamu tuwawie kwa upole, na wala tusioneshe dalili yoyote ya kuwadharau (rej. YbS. 3:12-14).

3.12 Familia ni Walinzi na Watetezi wa Uhai: Mwanaume na mwanamke walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu ni washiriki hai wa pendo la Mungu Muumba.  “Mungu akawabariki, Mungu akawaambia, “zaeni mkaongezeke, mkaijaze nchi na kuitiisha” (Mwa 1:28). Kumbe baraka ya uzazi, ni tunda na ishara ya upendo la mume na mke. Kanisa limepokea utume wa kusimamia na kuheshimu ndoa na kulinda uhai wa binadamu. Wanandoa sharti wajue wajibu wao wa kuzaa watoto, kuwa ni jukumu la kiimani na ni sharti kuzingatia uzazi kadri ya mpango wa Mungu.

Wanandoa wanao wajibu wa kujali afya zao na kuzitunza kwa kuongozwa na wataalamu wa afya ili katika kuishi ndoa yao watunzane kiuhai na wasisababishiane mateso ya kimaisha kimwili kwa makusudi kwao na kwa watoto wao. Licha ya kuwepo utamaduni mbovu dhidi ya uhai wa mwanadamu kutokana na maendeleo ya sayansi na teknolojia, Kanisa kwa dhati linaamini kuwa uhai wa kibinadamu daima ni zawadi bora ya wema wa Mungu. Kanisa linaitwa kudhihirisha utume wake wa kukuza uhai wa binadamu kwa kila njia na kuutetea dhidi ya mashambulizi yoyote ya kimwili na kiroho.

Katika kutetea uhai, Kanisa litaendelea kulaani makosa makubwa yanayotendeka dhidi ya haki Msingi ya uhai wa kibinadamu. Katika mazingira ya utamaduni ambao hupotosha sana au kutoa tafsiri tofauti kabisa ya maana ya kweli ya jinsia ya binadamu kwa kuiondolea vipengele muhimu vya utu, Kanisa linapinga watu kujiundia namna zao za kijinsia, ambazo zinapinga mpango wa Mungu aliye muumba mtu mume na mke kwa sura na mfano wake.

3.13 Haki na Wajibu wa Wazazi juu ya Malezi na Elimu ya Watoto wao: Kazi ya kutoa malezi imesimikwa katika wito wa kwanza wa watu wa ndoa wanohusika katika shughuli za Mungu za uumbaji.  Kwa vile wazazi wameridhia kuwazaa watoto, wanalo jukumu zito la kuwalea watoto wao kwa kuwapatia malezi mazuri pamoja na elimu itakayowafaa katika maisha yao yote. Vile vile ni jukumu la jamii nzima, yaani serikali na Kanisa kuhakikisha zinazisaidia familia, ili familia hizo ziweze kuwaelekeza watoto wao katika kupata elimu na mafunzo bora ya kukuza vipaji walivyonavyo ili waweze kumudu maisha yao hapa duniani (Gaudium et Spes nos. 35, 52). Watoto hawana budi kujifunza mengi, kukuza uwezo wao kitaaluma, hali wakisukumwa na vipawa vyao vyenye kuwaingiza katika utaratibu wa utendaji wa binadamu.

3.14 Haki ya Wazazi Kuchagua aina ya Elimu na Shule ya watoto wao: Mojawapo ya mambo muhimu naya lazima yanayopaswa kupewa kipaumbele kwa wazazi kuhusu watoto wao ni haki ya wazazi kuchagua aina ya elimu wanayotaka watoto wao waipate. Kwa hiyo, ni haki ya wazazi kuchagua elimu na malezi yenye kupatana na imani na maadili yao ya kidini (Rej.Can. 867#1).Kwa hiyo Kanisa na Serikali sharti vitengeneze na kutegemeza taasisi na mfumo wa malezi wenye kuwawezesha wazazi kuchagua aina ya elimu inayowafaa watoto wao kadiri ya vipaji, mazingira, makuzi na maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Katika jamii watoto wote wanapaswa kupata fursa sawa ya kujijengea makuzi kielimu, kitabia na kiutamaduni. Hii ni haki msingi kwa kila familia ambayo serikali sharti iwapatie wanafamilia wote bila kuweka matabaka (Gaudium et Spes no. 52).

Vilevile wale walio na mamlaka ya shule katika jamii wasisahau kwamba wazazi wamewekwa na Mungu mwenyewe kama walezi wa kwanza na wakuu wa watoto wao na kwamba haki yao hiyo haiwezi kabisa kutenganishwa nao na serikali inapaswa kulinda haki hii na kuwapa fursa wazazi kushiriki katika kutayarisha mitaala ya majifunzo hasa katika elimu ya msingi. Katika elimu ya sekondari na elimu ya ujuzi wazazi washirikishwe kuonesha matarajio yao juu ya malezi na makuzi ya kitaaluma ya watoto wao. Ushirikishwaji wa wazazi utawawezesha wazazi kujenga familia iliyokusudiwa na Mungu kwani maamuzi waliyofanya ya kuitikia wito wa kuzaa yalinuia kuwaleta duniani watoto na kuwatayarishia mafanikio hapa duniani.

SEHEMU YA NNE

4.0 FAMILI YA KIKRISTU: KITUO CHA MAENDELEO-JAMII ENDELEVU

Kwa hulka yake, familia badala ya kujifungia yenyewe, familia inao wito wake wa kuwa wazi kwa familia nyinginezo na kwa jamii; na kwa njia hiyo nayo huweza kuchukua majukumu yake katika jamii. Na kwa sababu hiyo maisha ya kifamilia humtambulisha na humwingiza mtu katika maisha ya jamii, kama vile ambavyo maisha ya familia ya kikristu humwingiza mtu katika maisha ya Kikristu. Kama Kristo Mfalme anavyotuhudumia, vivyo hivyo na mwanafamilia aone maana halisi ya kushiriki kwake katika ufalme wa Kristo hapa duniani katika kujitoa kikamilifu kumhudumia binadamu mwenzake. Ni jukumu la mwanafamilia hasa anayeongozwa na Kristo kutoa huduma yake akimwiga Kristo ili wenye mahitaji hasa maskini, wadhaifu na wale wenye kuteseka na kuteswa, wanaotendewa bila haki, wanaonyimwa haki zao za msingi, wanaoonewa na kubaguliwa waonje kuwa sote tumeumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu na hivi kujenga familia na jamii inayopendana (Rej.Mt.25:31-40; 1Yoh.4:19-21: Mw.1:26-27; Familiaris Consortium No. 63).

Familia za Kikristu, zikitambua kwa imani kuwa binadamu wote ni watoto wa Mungu Baba mmoja, zitaitikia kwa ukarimu mahitaji ya watoto wa familia nyingine zenye kuishi katika mazingira magumu, kwa kuwategemeza na kuwapenda kama watoto wa familia moja ya Mungu. Hivyo basi, jukumu la familia ya Kikristu katika jamii haliwezi kuishia katika uzazi na malezi (elimu), hata kama haya ndiyo majukmu asilia ya familia. Familia hii bado, au kwa yenyewe au pamoja na familia nyingine, ina wajibu wa kuleta maendeleo endelevu ya kumuondolea mwanadamu mateso ya kimwili na kiroho. Wajibu huu unatekelezeka vizuri hasa katika maeneo ambayo, kwa sababu moja au nyingine, hayawezi kuhudumiwa au kufikiwa na mamlaka ya kiraia. Familia ya Kikristo inapaswa pia kujihusisha katika maswala ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na kiutamaduni ili sera na sheria zinazotungwa ziweze kuakisi sura ya familia na jamii ya binadamu inayotokana na mpango wa Mungu kwa maisha ya mwanadamu hapa duniani.

SURA YA TANO

MAHIMIZO KWA FAMILIA

5.1 Himizo la Amri Kuu ya Mapendo

Katika mwaka huu wa familia, mahusiano ndani ya familia na kwenye jamii yaongozwe na Amri kuu ya upendo (Lk.6: 27-36). Utu wa binadamu na zawadi ya Mungu ya uhai vilindwe kwa sheria za kimungu na za kidunia. Wanafamilia hawana buni kupambana dhidi ya utamaduni mbovu unaodhalilisha utu na uhai (1Yoh 4:19). Lakini, kama ambavyo kauli mbiu ya mwaka huu wa Familia inavyotukumbusha, tunakua Familia Moja katika kazi moja ya umisionari: kazi hii itusukume kutangaza na kuonesha kwa wengine Upendo wa Watoto wa Familia ya Mungu mpaka mwisho wa dunia! Umisionari wa Injili ya Upendo ndiyo kielelezo muhimu cha kwamba sisi ni Familia ya Mungu, na tunapenda kila binadamu awe mwanafamilia katika Familia hii. “Kwa njia hii tunajua kuwa tunawapenda watoto wa Mungu tunapompenda Mungu na kutii amri zake” (1Yoh. 5:2).

5.2 Mkazo Mpya katika Elimu ya Dini: Tunazipongeza familia zilizodumisha hadhi yao ya kuwa shule za imani na maadili. Mchango wa familia hizo umekuwa mkubwa. Wapo watoto wanaoleleka na watu wazima walioleleka vyema. Kumetokea pia miito mizuri kutoka kwao. Lakini wakati tukizipongeza familia bora, yafaa tutahadharishane katika yafuatayo ili tuzidi kupata familia bora zitakazochangia malengo ya Kanisa zaidi na zaidi. Wanafamilia wafanye uamuzi wa makusudi kujidumisha katika misingi ya Kanisa na kuwalea watoto katika imani na maadili. Watoe ushirikiano wa karibu kwa viongozi wa kanisa, makatekista, watawa na walimu kusudi kuwahimiza watoto kuendelea kuthamini tunu za Injili wapate kujiepusha na utamaduni wa ubinafsi ambao si tu unampeleka mtu mbali na Mungu bali pia unamfanya asione sababu ya kudumisha imani na maadili yaletayo wokovu. Wazazi wajitahidi kufikiri pamoja na Kanisa. Yaani kile kinachofundishwa na Kanisa kiwe ndicho wanachokifahamu, wanachokilinda, wanachokipenda, kufundisha na kuelelea watoto pamoja na kufunda dhamiri za wanafamilia.

Wazazi washikane katika kuwafundisha vyema watoto wao kusali, kupokea sakramenti, kutumia visakramenti na kuhudhuria ibada. Wawapangie watoto ratiba na kuwadhibiti katika matumizi ya vyombo vya habari na vitu kama simu, intaneti, mitandao, magazeti na vitabu. Kamwe wasiache ulimwengu au wenzao wawe walimu wao (rej. Mit 7:22 na YbS 30:1-13). Wazazi   wawe na desturi ya sala, sala binafsi na ibada kwa Bikira Maria na watakatifu wengine ili watoto waweze kujifunza kimatendo moyo wa sala.

5.3 Kupaza Sauti dhidi ya uharibifu wa familia: Sasa hebu tupaze sauti zetu za kinabii tupate kuhimiza kudumu katika wema na tuonyane tuache dhambi. Tuelewane vyema; katika kuifanya kazi hii tuna sababu nzito mbili: Mosi, wote tumefanywa walinzi wa nyumba ya Mungu na tuna wajibu wa kuhimizana na kuonyana tusije tukaangamia sote. Ezekieli anasema, “Hata ikawa mwisho wa siku saba, neno la Bwana likanijia, kusema, ‘Mwanadamu nimekuweka kuwa mlinzi wa nyumba ya Israeli. Na siku neno hili litokalo katika kinywa changu, ukawape maonyo haya usimpe maono, wala husemi na huyo mtu mbaya ili kumwonya, kusudi aache njia yake mbaya na kujiokoa roho yake, mtu yule mbaya atakufa katika uovu wake, lakini damu yake nitaitaka mkononi mwako. Lakini ukimmwonya mtu mbaya, wala yeye hauachi ubaya wake, wala njia yake mbaya, atakufa katika uovu wake, bali wewe umejiokoa roho yako.

“Tena mtu mwenye haki aiachapo haki yake na kutenda uovu, nami nikaweka kikwazo mbele yake atakufa, kwa sababu hukumwonya, atakufa katika uovu wake, wala matendo yake ya haki aliyayotenda hayatakumbukwa lakini damu yake nitaitaka mkononi mwako. Basi, ukimwonya mwenye haki kwamba yule mwenye haki asitende dhambi, tena ikiwa yeye hatendi dhambi, hakika ataishi, kwa sababu alikubali kuonywa na wewe umejikoa roho yako” (Eze 3:16-21). Pili, ni jukumu la pekee wa viongozi wote wa Kanisa kwa mujibu wa sakramenti ya Daraja. Ndiyo, kwa nguvu hiyo hiyo Paulo alimtahadharisha Timotheo. Na kwa kweli alimtahadharisha kwa niaba ya Kanisa na wahudumu wake wote, ifuatavyo:“Nakuamuru mbele ya Mungu na mbele ya Kristo Yesu atakayewahukumu watu walio hai na wafu, na kwa sababu anakuja kutawala akiwa Mfalme, hubiri huo ujumbe, sisitiza kuutangaza (iwe ni wakati wa kufaa au wakati usiofaa), karipia, onya na himiza watu ukiwafundisha kwa uvumilivu wote. Utakuja wakati ambapo watu hawatasikiliza mafundisho ya kweli, ila watafuata tamaa zao wenyewe na kujikusanyia waaalimu tele watakaowaambia mambo yale tu ambayo masikio yao yako tayari kuyasikia. Watakataa kuusikia ukweli, watageukia hadithi za uongo. Wewe, lakini, uwe macho katika kila hali, vumilia mateso, fanya kazi ya mhubiri wa Injili, timiza kikamilifu utumishi wako” (2Tim 4:1-5).

Si siri tangu karne iliyopita dunia imevamiwa na watu wenye agenda ya kugeuza imani na maadili. Kuna propaganda kubwa kwenye vyombo vya habari, redio, magazeti, televisheni, mitandao na kadhalika. Pesa nyingi na nguvu kubwa vinatumika kufikia malengo maovu. Yanakusudiwa mambo matatu: kuozesha akili na mioyo ya walimwengu wakubaliane na uovu kama tunu, kuwafunga vinywa wanakanisa na wenye wajibu wa kukemea uovu duniani na kuwavuruga wateolojia wasisimamie tena walivyopaswa kusimamia na kufundisha. Yakifanikiwa mambo haya, Mungu atakuwa amenyang’anywa umiliki wa mti wa ujuzi wa mema na mabaya (Rej.Mwa. 2:9.17, 3:3). Wanadamu watakuwa wanampangia Mungu atake wanayopanga wanadamu kuwa mema au mabaya. Hatuna budi kupiga vita uasi wa namna hii unaofanana na uasi wa waisraeli waliojitengenezea mungu wa ndama wa dhahabu.

5.4 Uhitaji wa uongofu endelevu wa kupitia Familia.

Familia ina msaada mkubwa wa kuwasaidia wanafamilia kuongoka. Ili kupambana na dhambi, ukosefu wa haki uliopenya kwenye muundo wa ulimwengu wa leo na mara nyingi unaoizuia familia kujitambua kikamilifu na ule unaozuia familia kuzitambua haki zake za msingi, ni sharti kuikuza mioyo yetu kwa njia ya wongofu wa akili na mioyo, tukimfuasa Kristo Msulubiwa, kwa kujishinda ubinafsi na uchoyo.  Jambo linalotakiwa ni uongofu endelevu ambapo mtu hukuza tabia na mazoea ya kuwa na wema wa kiutu na kiMungu unaojidhihirisha katika tabia ya mtu na katika utamaduni na mahusiano ndani ya jamii husika.

5.5 Bikira Maria, Malkia wa Familia        

Katika Arusi ya Kana (Yoh 2:1-11), Mama huyu mtakatifu alitupa ufunguo wa kutakatifuza na kuimarisha familia zetu. Kauli yake ni isiyopitwa na wakati kamwe: “Lolote atakalowaambia, fanyeni.” Familia zetu zinakabiliwa na changamoto nyingi, tuziweke chini ya maombezi na ulinzi wa Familia Takatifu. Kila siku tuifungue mioyo yetu kulisikiliza, kulitafakari na kuliishi Neno la Mungu. Miaka mia Hamsini ya uinjilishaji nchini mwetu, ni mingi ya kutosha, kuifanya Imani yetu iote mizizi ndani ya familia zetu. Tumeona kirefu jinsi familia za Kiyahudi zilivyoleana na hata kuweka mizizi ya malezi endelevu katika watu. Jambo hilo lilifaa litokee katika familia za Kikristo kwa vile tunatamani tuwe na malezi ya imani na maadili yenye kudumisha waamini. Familia yoyote iliyokaa vyema lazima itafaulu kama shule ya imani na maadili na Kanisa likafaidi utakatifu na miito iliyo timamu.

HITIMISHO: Tunawatakia Neema na Baraka za Mwenyezi Mungu katika kipindi hiki kitakatifu cha Kwaresima.  Ni kipindi cha toba, kuongoka, kujipatia neema na fadhila na kujenga familia imara kiimani na kimaadili yaani kumtengenezea Mungu makazi yake ndani ya kila familia.

SALA: Ee Baba wa mbinguni, / tunakuomba utujalie familia imara,/zenye kufuata mfano wa familia takatifu ya Nazareti/ ya Yesu, Maria na Yosefu. /Familia zetu ziwe Kanisa la awali la nyumbani, shule ya Imani, Matumaini na Mapendo, / Nyumba ya Sala na malezi yenye tunu / za maadili mema kwa wazazi na watoto. AMINA. Na maneno haya niliyokuamuru leo yatakuwa katika moyo wako; nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyanena uketipo katika nyumba yako na utembeapo njiani na ulalapo na uondokapo. (Kumb. 6: 6-7)


Maoni


Ingia utoe maoni