Alhamisi. 21 Novemba. 2024
feature-top
Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo: Papa Francisko atoa dondoo za kufanyia tafakari!

Washiriki wa mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo, wamemwombea Baba Mtakatifu ili aweze kutekeleza vyema dhamana na majukumu yake kama Mwalimu na Mchungaji mkuu wa watu wa Mungu. Hii ni dhamana ambayo Kristo Yesu alimkabidhi Mtakatifu Petro pamoja na waandamizi wake, msingi na kanuni inayooneka ya umoja wa Kanisa!

Mkutano wa Kanisa kuhusu Ulinzi kwa Watoto Wadogo, Ijumaa, tarehe 22 Februari 2019, Siku kuu ya Ukulu wa Mtakatifu Petro, Mtume, ulianza kwa kwa sala pamoja na kumwombea Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa wakati huu Kanisa linapotia kipindi kigumu katika maisha na utume wake! Washiriki wa mkutano huu, wamemwombea Baba Mtakatifu ili aweze kutekeleza vyema dhamana na majukumu yake kama: Mwalimu na Mchungaji mkuu wa watu wa Mungu. Hii ni dhamana ambayo Kristo Yesu alimkabidhi Mtakatifu Petro pamoja na waandamizi wake, msingi na kanuni inayooneka ya umoja wa Kanisa!

Baba Mtakatifu Francisko analitaka Kanisa kusikiliza kwa umakini sana kilio cha watoto walionyanyasika kijinsia, ili hatimaye, Kanisa liweze kuibua mbinu mkakati utaotumika kujenga na kudumisha malezi, makuzi, ustawi na maendeleo ya watoto: kiroho na kimwili. Katika muktadha huu, Baba Mtakatifu ametoa mapendeko yanayoweza kuongoza tafakari za wajumbe wa mkutano huu, ili hatimaye Kanisa liweze kufikia muafaka kwa kutoa jibu makini. Baba Mtakatifu anawaalika wajumbe kuangalia uwezekano wa kuandaa kitabu kitakachoonesha hatua mbali mbali zinazopaswa kufuatwa na uongozi wa Kanisa mara kunapoibuka kesi za nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa.

Anawashauri Maaskofu kujenga utamaduni wa kusikiliza kwa makini kilio cha nyanyaso za kijinsia pamoja na kuandaa kanuni na taratibu zitakazomsaidia Askofu na Wakuu wa Mashirika kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao kwa kuchunguza tuhuma zilizowekwa mbele yao na haki ya mtuhumiwa kujibu shutuma hizi. Baba Mtakatifu anawasihi viongozi wa Kanisa kufanya tathmini ya sheria, kanuni, taratibu na miongozo walizojiwekea mintarafu miundombinu ya shughuli za kichungaji kwa kuzingatia protokali iliyopo, ili kuliwezesha Kanisa kutekeleza dhamana na wajibu wake wa kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili.

Wajumbe waangalie jinsi ambavyo wanaweza kutayarisha protokali itakayoshughulikia tuhuma za nyanyaso za kijinsia kutoka kwa Maaskofu pamoja na kuangalia jinsi ya kuwasindikiza, kuwalinda na kuwahudumia waathirika wa nyanyaso za kijinsia, ili waweze kupona kabisa na madonda wanayobeba mwilini na rohoni mwao! Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu na Wakuu wa Mashirika kuhakikisha kwamba, wanaendelea kuragibisha athari za nyanyaso za kijinsia katika maisha na utume wa Kanisa kwa njia ya malezi awali na endelevu kwa majandokasisi, wakleri, watawa na wafanyakazi wa Kanisa. Wajumbe, waangalie uwezekano wa kuandaa njia za kichungaji kwa ajili ya kusaidia jumuiya ambazo zimeathirika kutokana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia.

Viongozi wa Kanisa wanapaswa kushirikiana na kushikamana na watu wenye mapenzi mema, pamoja na vyombo vya mawasiliano ya jamii ili kubainisha kesi halisi za nyanyaso za kijinsia dhidi ya shutuma zisizo za kweli zinazolenga kuwachafulia watu utu na heshima yao mbele ya umma! Wajumbe waangalie uwezekano wa kuongeza miaka ya vijana kufunga ndoa kutoka umri wa sasa na walau kufikia miaka 16. Kanisa liangalie uwezekano wa kuwashirikisha wataalam walei katika kuchunguza kesi za nyanyaso za kijinsia pamoja na matumizi mabaya ya madaraka. Watuhumiwa wapewe nafasi ya kujitetea mbele ya vyombo vya sheria. Adhabu inayotolewa, ilingane walau na kosa lililotendwa. Kwa Mapadre na Maaskofu watakapotiwa hatiani, wasimamishwe mara moja kutoa huduma za kichungaji hadharani.

Uchunguzi wa kina ufanywe kwa vijana wanaotaka kujiunga na maisha na utume wa Kipadre. Kuwepo na sheria, kanuni na taratibu zinazodhibiti uhamisho wa mseminari au padre kutoka Jimbo moja kwenda jimbo jingine, au shirika moja kwenda shirika jingine. Kuwepo na sheria, kanuni na taratibu za kimaadili na kiutu zinazopaswa kufuatwa na mapadre, watawa pamoja na wafanyakazi katika taasisi zinazosimamiwa na kuendeshwa na Kanisa pamoja na kuonesha mipaka ya mahusiano yao. Taarifa sahihi zitolewe kuhusiana na shutuma za nyanyaso za kijinsia.

Taarifa hizi zichukuliwe kwa kushirikiana na wazazi, walezi, wataalam na viongozi wa Serikali. Kuwepo na kundi ambalo waathirika wa nyanyaso za kijinsia wanaoweza kuliendea ili kuzungumzia kashfa kama hizi. Kundi kama hili anasema Baba Mtakatifu katika ushauri wake, linapaswa kuwa huru na liundwe na wataalaam wanaoweza kuelezea nia njema ya Kanisa kwa watu waliojeruhiwa na nyanyaso za kijinsia ndani ya Kanisa.


Maoni


Ingia utoe maoni