Alhamisi. 21 Novemba. 2024
feature-top
Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo: Shuhuda: Ukatili mkubwa dhidi ya utu na heshima ya binadamu!

Nyanyaso hizi ni kati ya mambo ambayo yanadhalilisha utu na heshima ya binadamu; kwa kuonesha unyonge na udhaifu wa mtu kushindwa kujitetea mwenyewe kutokana na nguvu kubwa inayoshinda uwezo wake! Hapa ndipo mtu anapojiona anadhalilishwa kwa macho makavu na wala hana uwezo wa kukimbia au kupambana na nyanyaso hizi na matokeo yake, anakuwa mpole tu!

Katika Ibada ya Toba iliyoongozwa na Baba Mtakatifu Francisko, Jumamosi, jioni tarehe 23 Februari 2019 kama sehemu ya maadhimisho ya Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo uliofunguliwa rasmi tarehe 21 Februari na kuhitimishwa, Jumapili tarehe 24 Februari 2019 kwa Ibada ya Misa Takatifu na hotuba nzito kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko, walipata pia nafasi ya kusikiliza shuhuhuda za waathirika wa nyanyaso za kijinsia!

Itakumbuka tangu mwanzo kwamba, dhamana na wajibu wa viongozi wa Kanisa kuwasikiliza kwa makini waathirika wa nyanyaso za kijinsia ni jambo lililopewa msukumo wa pekee kabisa na Baba Mtakatifu Francisko. Baadhi ya waathirika wakasikilizwa na Kamati kuu ya Maandalizi ya Mkutano huu pamoja na Marais wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki, kila mmoja, alijitahidi kutekeleza dhamana hii inayopaswa kuwa ni endelevu katika maisha na utume wa Kanisa kama njia ya kupambana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia katika ukweli na uwazi!

Shuhuda wa nyanyaso za kijinsia, Jumamosi jioni alisikitika kusema kwamba, nyanyaso hizi ni kati ya mambo ambayo yanadhalilisha utu na heshima ya binadamu; kwa kuonesha unyonge na udhaifu wa mtu kushindwa kujitetea mwenyewe kutokana na nguvu kubwa inayoshinda uwezo wake! Hapa ndipo mtu anapojiona anadhalilishwa kwa macho makavu na wala hana uwezo wa kukimbia au kupambana na nyanyaso hizi na matokeo yake, anakuwa mpole kupita kiasi! Haiwezekani mtu kukimbia kivuli chake, kwani daima kitamwandama!

Ni katika mazingira na hali kama hii, mtu anaweza kutumbukia katika ombwe la upweke hasi kiasi cha kukata na kujikatia tamaa! Hii ni hali inayomchanganya na kumuumiza mtu kutoka katika undani wake, kiasi cha kushindwa kujifahamu kikamilifu na wala wale unaowaelezea madonda yaliyoko moyoni mwako wanashindwa kukusikiliza na kufahamu jinsi unavyoteseka! Si rahisi mtu kurejea tena katika maisha na ulimwengu wa hapo awali, hali ambayo inamfanya mtu aliyenyanyasika kijinsia kubaki katika uvuli wa ulimwengu uliopita na mateso yanayomwandama kwa wakati huu. Haya ni matukio ambayo yataendelea kumwandama mtu hadi anaingia kaburini.

Shuhuda huyu anasema, amejitahidi kupokea hali halisi ya maisha yake na sasa anaweza kusonga mbele kwa imani na matumaini zaidi, kwani Mwenyezi Mungu amemkirimia tena nafasi ya kuishi! Ni katika utambuzi huu, ameweza kusimama mbele ya Kanisa na kutoa ushuhuda wake! Anasema, yaliyopita si ndwele, anataka kuganga ya sasa na yale yajayo! Anataka kuona haki ikitendeka, amani ikirejeshwa tena; kwa kuzungumza katika ukweli na uwazi; kwa kujifunza kudhibiti hasira na chuki, ili kusonga mbele!


Maoni


Ingia utoe maoni