Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili tarehe 24 Februari 2019 amehitimisha Mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo uliofunguliwa tarehe 21 Februari 2019 kama sehemu ya mchakato wa sera na mbinu mkakati wa Kanisa kupambana na kashfa ya nyanyaso za kijinsia iliyochafua maisha na utume wa Kanisa! Baba Mtakatifu katika hotuba yake amekazia mambo yafuatayo: Ameelezea hali ya nyanyaso za kijinsia jinsi ilivyo duniani; Utalii wa ngono; Uchu wa madaraka pamoja na mbinu mkakati utakaosaidia kufutilia mbali nyanyaso dhidi ya watoto wadogo.
Baba Mtakatifu amesisitiza kuhusu umuhimu wa kuwalinda watoto wadogo, adhabu kali kutolewa; toba na wongofu wa ndani; malezi makini; uimarishaji na mapitio ya miongozo ya Mabaraza ya Maaskofu; Umuhimu wa kuwasindikiza waathirika wa nyanyaso za kijinsia pamoja na kuangalia ulimwengu wa kidigitali na madhara yake pamoja na kupambana na Utalii wa ngono duniani unaodhalilisha utu na heshima ya watu! Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, nyanyaso za kijinsia ni janga ambalo limenea sehemu mbali mbali za dunia na wakati mwingine, linajikita katika imani za kishirikina zinazopelekea watoto wadogo kutolewa kafara.
Hali ya Nyanyaso za Kijinsia Duniani: Janga hili limegusa hisia za Mashirika ya Kimataifa kama vile: WHO, UNICEF, INTERPOL, EUROPOL na Mashirika mengine. Hata hivyo, kesi nyingi za nyanyaso za kijinsia hazitolewi taarifa kwenye vyombo vya ulinzi na usalama, kwa vile haya ni matukio yanayotendeka ndani ya familia zenyewe! Takwimu za uhakika zinaonesha kwamba, wahusika wakuu wa nyanyaso za kijinsia iwe kimwili au kihisia tu ni: wazazi wenyewe, ndugu na jamaa; baba wa kambo, makocha wa michezo pamoja na waalimu. Takwimu za Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF kwa mwaka 2017 zinaonesha kwamba, katika nchi 28, wasichana 9 kati ya 10 wamefanya ngono za lazima na watu waliokuwa karibu sana na familia zao.
Takwimu za Serikali ya Marekani zinaonesha kwamba, watoto 700, 000 kila mwaka wanaathirika kwa nyanyaso mbali mbali nchini humo. Kila kundi la watoto 10 kuna mtoto mmoja ambaye amenyanyasika kijinsia. Takwimu za Serikali ya Italia kwa mwaka 2016 zilizotolewa na Telefono Azzuro zinaonesha kwamba, asilimia 68.9% ya vitendo vyote vya nyanyaso za kijinsia vinatendeka ndani ya familia. Haya ni matukio yanayofanywa kwenye mazingira ya nyumba za jirani, shuleni, kwenye maeneo ya michezo na kwa uchungu mkubwa anasema Baba Mtakatifu hata katika maeneo ya Kanisa!
Takwimu zinaonesha kwamba, maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano yamechangia kwa kiasi kikubwa, ongezeko la nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo. Hali hii imepelekea madhara makubwa kisaikolojia, kuvunjika kwa mahusiano kati ya wanaume na wanawake; kati ya watu wazima na watoto. Picha za ngono zina athari kubwa katika utu na heshima ya watoto, kiasi kwamba, hata wakati mwingine picha hizi za utupu zinaoneshwa mubashara kwenye mitandao ya kijamii! Kongamano la Kimataifa kuhusu ulinzi wa watoto katika ulimwengu wa kidigitali lililofanyika mjini Roma pamoja na Jukwaa la Mwingiliano wa Kidini kwa ajili ya Usalama wa Jumuiya lililofanyika huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu, Novemba 2018 yanapaswa kukumbukwa!
Utalii wa Ngono kadiri ya Takwimu za Shirika la Utalii la Umoja wa Mataifa kwa Mwaka 2017 zinaonesha kwamba, kuna watu milioni 3 kutoka sehemu mbali mbali za dunia wanaofanya utalii wa ngono na kwa makusudi mazima, wanapenda kufanya ngono na watoto wadogo, matukio ambayo ni uhalifu mkubwa! Hakuna msamaha unaoweza kutolewa ikiwa kama matendo haya yanafanyika pia hata ndani ya Kanisa, kwani hii ni kashfa kwa watu ambao wamejisadaka kwa ajili ya Mungu na Kanisa wanageuka kuwa ni madalali wa Shetani!
Kanisa linapaswa kukiri na kujutia kashfa hii kwa kujikita katika sheria za Kanisa na kiraia pamoja na kuendeleza mapambano haya ndani na nje ya Kanisa, kama sehemu ya utume wake wa kuwatangazia watu Habari Njema ya Wokovu pamoja na kuwalinda watoto wadogo! Kanisa kuanzia sasa, halitakuwa na msamaha wa aina yoyote ile kwa wale wote watakaotiwa hatiani kuhusika na nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo. Inasikitisha kuona kwamba, watoto hawa badala ya kupata walezi ambao wangewasaidia katika maisha yao, wanakumbana na wadhalimu wanaowatesa kutokana na nyoyo zao kuwa ngumu kwa sababu ya unafiki na uchu wa madaraka! Kanisa lina wajibu wa kusimama kidete kusikiliza na kujibu kilio cha watoto wanaonyanyasika kijinsia!
Uchu wa mali na Madaraka umepelekea watoto wengi kutumbukizwa katika nyanyaso za kijinsia na unyonyaji wa kingono. Takwimu zinaonesha kwamba, watoto 85, 000, 000, wamesahauliwa, lakini wako mstawi wa mbele vitani kama chambo; wanatumikishwa kwenye biashara ya ngono; wanatekwa na kubakwa; wananyofolewa viungo vyao kwa ajili ya biashara ya binadamu na viungo vyake. Hawa ni watoto wanaotumbukizwa bila aibu katika utumwa mamboleo! Watoto wengine wanamezwa na utamaduni wa kifo unaofumbatwa katika sera za utoaji mimba, watoto kujikuta wakiwa wakimbizi na wahamiaji au waathirika wa vita. Yote haya ni matokeo ya uchu wa mali, utajiri na madaraka; ni kielelezo cha kiburi cha mwanadamu. Hapa, Baba Mtakatifu Francisko anasema, kuna haja ya kuchukua hatua kali!
Katika hali ya unyenyekevu mkuu, kwa kutambua dhamana na madaraka yake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, kielelezo cha upendo, Baba Mtakatifu Francisko anasema, katika matukio haya yote anaona mkono wa Shetani. Ni wakati kwa Kanisa kunyenyekea, kuchunguza dhamiri, kusali, kutubu na kumwongokea Mungu kama njia ya kupambana na Ibilisi kama alivyoonesha Kristo Yesu mwenyewe! Kanisa linataka kusikiliza kwa makini, kuwalinda na kuwahudumia waathirika wa nyanyaso za kijinsia! Wakati umewadia wa kushikamana ili kuweza kungo’a ubaya huu kutoka katika maisha ya watu, kwa kuhakikisha kwamba, Kanisa linatumia sera na mikakati ya kitaifa na kimataifa katika kupambana na uovu huu! Kanisa lazima likwepe kishawishi cha kutaka kutoa haki nyepesi nyepesi au kuangukia katika tabia ya kutaka kujilinda lenyewe dhidi ya shutuma zinazoelekezwa kwake!
Mbinu mkakati utakaosaidia kufutilia mbali nyanyaso dhidi ya watoto wadogo. Hapa Baba Mtakatifu anaorodhesha mambo makuu saba yanayopaswa kuvaliwa njuga ili kukomesha ukatili dhidi ya watoto wadogo. Mosi, ulinzi kwa watoto wadogo unapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza ili kuwalinda dhidi ya nyanyaso za kisaikolojia na kimwili. Watu wanapaswa kutubu na kuongoka; kwa kujikita katika ukweli na uwazi, ili kamwe wasiwe ni sababu ya kashfa kwa watoto wadogo, kwani watakiona cha mtema kuni! Pili, nyanyaso za kijinsia ni uhalifu mkubwa unaonesha jinsi ambavyo watu wamekengeuka kwa kukosa uaminifu kiasi cha kuandamwa na aibu. Hawa ni watu wanaochafua maisha na utume wa Kanisa.
Tatu, kuna haja ya kufanya utakaso wa kweli, kwa kujikita katika sera na mikakati ya kuwalinda watoto wadogo; kwa viongozi wa Kanisa kuendelea kupyaisha maisha yao kwa kuambata utakatifu pamoja na kuhakikisha kwamba, wanalinda na kutunza haki msingi za watu wa Mungu. Kanisa linataka kujitakasa na kusimama kidete kuwalinda watoto wadogo; kuendelea kujifunza makosa yaliyopita, ili kuondoa kashfa hii ndani ya Kanisa na jamii katika ujumla wake! Nne, Kanisa litaendelea kukazia malezi, kwa kuwateua vijana wanaostahili kushiriki maisha na wito wa Kipadre; Kanisa linataka kujikita katika malezi na makuzi yenye uwiano bora sanjari na kukazia useja kama sadaka kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani!
Tano, Kanisa litaendelea kuimarisha pamoja na kupitia miongozo mbali mbali ambayo imetolewa na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki, ili kuhakikisha kwamba, inatekelezwa vyema na Maaskofu mahalia. Ukweli, uwazi na ulinzi wa watoto wadogo ni mambo yanayopaswa kupewa uzito unaostahili. Lengo ni kuzuia nyanyaso za kijinsia katika maeneo yote ya Kanisa, ili watoto waweze kupata mali pazuri zaidi pa malezi na makuzi yao. Sita, Kanisa liwasindikize waathirika wa nyanyaso za kijinsia, kwa kuwapatia msaada wa hali na mali wanaouhitaji! Kanisa lijenge na kudumisha utamaduni wa kusikiliza kwa makini, ili kuganga na kuponya madonda ya watu kama ilivyokuwa kwa Msamaria mwema.
Saba, Ulimwengu wa kidigitali kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano ya jamii unapaswa kuangaliwa kwa umakini mkubwa. Viongozi na wafanyakazi wa Kanisa watambue madhara yanayoweza kuwakumba watumiaji wa mitandao hii. Serikali mbali mbali duniani hazina budi kudhibiti mitandao ambayo inahatarisha utu na uhuru wa kweli wa binadamu. Picha za utupu zitendelee kudhibitiwa ili kuhakikisha kwamba, majandokasisi na wakleri hawageuzwi na kuwa ni watumwa wa picha za ngono na utupu! Makosa makubwa ya uhalifu, Delicta graviora, kama yalivyofafanuliwa na kupitishwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI yapitiwe tena na kuongezewa vipengele kuhusu ununuzi, umiliki na usambazaji wa picha za ngono za watoto wadogo unaoweza kufanywa na wakleri kwa kutimia aina yoyote ile ya teknolojia. Na kwamba, umri wa watoto wadogo unapaswa kuongezwa na kufikia miaka 16.
Nane ni kuhusu Utalii wa Ngono! Watu wameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu. Wanapaswa kupewa nafasi ya kukua na kukomaa: kiroho na kimwili pamoja na kuendeleza mahusiano na mafungamano yao na jirani. Kumbe, utu, heshima na utakatifu wao vinapaswa kulindwa dhidi ya nyanyaso, unyonyaji pamoja na rushwa. Mapambano dhidi ya utalii wa ngono yaende sanjari na kuwajengea uwezo waathirika kurejea tena katika jamii na hivyo kuendelea na maisha. Taasisi za Kanisa ziwasaidie waathirika wa utalii wa ngono.
Serikali mbali mbali zisimame kidete kupambana na biashara ya binadamu na unyonyaji wa watoto wadogo kingono kwa kuhakikisha kwamba, sheria zilizopo zinatekelezwa kikamilifu. Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza wakleri na watawa ambao wamekuwa mstari wa mbele katika kuwalinda na kuwatetea waathirika wa utalii wa ngono. Baba Mtakatifu anahitimisha kwa kusema, katika usiku na giza nene, huu ndio wakati wa kuibuka kwa Manabii na Watakatifu! Unabii wa Kanisa unatekelezwa kikamilifu kati pamoja na watu wa Mungu! Zawadi kubwa inayoweza kutolewa kwa watu wa Mungu ni toba na wongofu wa ndani; unyenyekevu katika kujifunza; kusikiliza na kuhudumia sanjari na kuwalinda watoto wadogo! Baba Mtakatifu anawataka watu kusimama kidete kupambana na nyanyaso na dhuluma dhidi ya watoto wadogo! Serikali ziunge mkono juhudi hizi, ili mafanikio yaweze kupatikana!
Maoni
Ingia utoe maoni