Unyenyekevu na utakaso ni mambo msingi yanayomwezesha mwamini kuingia kwa unyoofu katika sala. Unyenyekevu unawafanya waamini kutambua kwamba, “hakuna amjuaye Baba ila Mwana, na yeyote ambaye Mwana apenda kumfunulia. Utakaso wa moyo unahusu fikra, historia na tamaduni zinazoathiri uhusiano na mafungamano kati ya Mwenyezi Mungu na waja wake. Kumwomba Mwenyezi Mungu ni kuingia ndani ya Fumbo lake kama alivyo Yeye na kama Mwana alivyomfunua kwa binadamu!
Baba Mtakatifu Francisko wakati wa Katekesi yake, Jumatano tarehe 20 Februari 2019 ameendelea kutafakari kuhusu Sala ya Baba Yetu, Sala ya Bwana kwa kuchambua kipengele kinachosema, “Baba Yetu Uliye Mbinguni”. Hakuna mtu awaye yote anayeweza kujidai kwamba, katika maisha yake, alibahatika kupata wazazi wakamilifu kabisa, kwani kila mzazi ana mapungufu yake ya kibinadamu, kiasi kwamba, hata wakati mwingine, upendo unaweza kufifishwa kwa njia chuki, hasira na uhasama kati ya watu, kiasi hata cha kuwashangaza jirani. Hii ni kutokana na mbegu ya ubaya ambayo iko katika undani wa mtu!
Baba Mtakatifu anakaza kusema, katika Sala ya Bwana yaani: “Baba Yetu” ni jina linalochukua taswira ya wazazi hasa wale ambao walionesha upendo wa pekee kwa watoto wao, lakini pia wanapaswa kuvuka taswira hii na kwenda mbali zaidi, kwani upendo wa Mungu ni ule wa “Baba Yetu aliye mbinguni” maneno ambayo Kristo Yesu anawaambia wafuasi wake kuyatumia, kama kielelezo cha upendo mkamilifu, ambao kwa sasa waamini wanaweza kuuonja kidogo. Hii ni kutokana na ukweli kwamba, binadamu daima ana kiu ya upendo, ili kupenda na kupendwa; lakini kwa bahati mbaya, upendo wakati mwingine unapotea na kutoweka kama ndoto ya mchana!
Baba Mtakatifu anaendelea kufafanua kwamba, mungu wa upendo kwa Wagiriki, anafahamika kwa utata kidogo kama Malaika au Ibilisi! Upendo wao ni kama umande wa asubuhi unaotoweka mara kunapopambazuka! Wakati mwingine inakuwa ni vigumu sana kudumisha uaminifu katika upendo. Lakini, kuna upendo wa kweli unaobubujika kutoka kwa Baba Yetu aliye mbinguni! Huu ni upendo ambao umepitia katika hatua mbali mbali, kwa kusimama na kuanguka, kutokana na udhaifu na umaskini wa binadamu!
Hivi ndivyo ilivyokuwa hata kwa Mtume Petro, aliyetikiswa na hatimaye, akamkana Kristo Yesu. Kuna hatari kubwa kwamba, mwanadamu ataendelea kutanga tanga kiasi hata cha kushindwa kupata amana ya upendo ambayo anaitafuta tangu siku ile ya kwanza anapozaliwa! Baba Yetu aliye mbinguni ni hatima ya upendo huo kwani anafahamu kupenda kwa dhati pasi na mfano wowote duniani. Ni kutokana na upendo huu, Nabii Isaya anathubutu kusema, “Tazama, nimekuchora katika vitanga vya mikono yangu” Yaani, watu wote wamechorwa kwenye vitanga vya mikono ya Mungu na kwamba, upendo wake wadumu milele na kamwe hawezi kuwasahau waja wake!
Hiki ndicho kielelezo cha upendo mkamilifu, unaobubujika kutoka kwa Mwenyezi Mungu!Upendo wa binadamu ni sawa na moto wa mabua! Binadamu anayo kiu ya upendo anaoutafuta kwa udi na uvumba! Upendo wa kweli ni kumfahamu Mwenyezi Mungu, Baba Yetu Aliye Mbinguni! Kwa hakika, Mungu anapenda! “Uliye mbinguni si kielelezo cha umbali, bali tofauti ya kweli inayofumbatwa katika upendo unaodumu milele.Baba Mtakatifu anawataka waamini kutoogopa, kwa sababu Mwenyezi Mungu yuko daima pamoja nao. Waamini watambue kwamba, wao ni watoto wapendwa wa Mungu na wala hakuna jambo lolote linaloweza kuuzima upendo wa Mungu.!
Mwishoni mwa katekesi yake, Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kuwa kweli ni mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka!Amewakumbusha kwamba, Ijumaa, tarehe 22 Februari 2019, Kanisa linaadhimisha Ukulu wa Mtakatifu Petro, Mtume! Baba Mtakatifu anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kumkumbuka na kumwombea katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, ili aweze kuwaimarisha ndugu zake katika imani kwa Kristo Mfufuka!
Maoni
Ingia utoe maoni