Alhamisi. 21 Novemba. 2024
feature-top
Mpango Mkakati wa Kanisa Kuwalinda Watoto Wadogo: Historia yake kwa ufupi na matarajio ya Kanisa!

Kanisa limekuwa likikabiliana na kashfa hizi, tangu zilizopoanza kuzuka na kwamba, Kanisa katika miaka kumi 18 iliyopita lilichapisha sheria, kanuni na taratibu. Kumekuwepo na matamko ya viongozi mbali mbali wa Kanisa, lakini hayakufua dafu. Mwaka 1992 kulichapishwa hati “Kutoka katika mateso, kuelekea katika matumaini” na hapa mapendekezo 50 yaliyotolewa.

Mbinu mkakati wa ulinzi wa watoto wadogo ni juhudi ambazo zimekuwa zikitekelezwa na Mama Kanisa sehemu mbali mbali za dunia. Baba Mtakifu Francisko anasema, ameitisha mkutano wa Kanisa Kuhusu Ulinzi wa Watoto Wadogo kuanzia tarehe 21-24 Februari 2019 kama kielelezo makini cha wajibu wa kichungaji ili kuweza kukabiliana na changamoto hii nyeti katika ulimwengu mamboleo. Hii ni sehemu ya utekelezaji wa “dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa”. Lengo ni kuwasikiliza waathirika, kutambua madhara yake katika: maisha na utume wa Kanisa; katika utu na heshima ya waathirika; ili hatimaye, kuibua: sheria, kanuni na taratibu zinazopaswa kufuatwa ili kudhibiti kashfa hii ambayo inadhalilisha utu na heshima ya binadamu!

Kwa miaka mingi sasa, Kanisa limekuwa likijitahidi kukabiliana na kashfa hizi, tangu zilizopoanza kuzuka huko Canada, Marekani, Ulaya na kwamba, Kanisa katika miaka kumi 18 iliyopita lilichapisha sheria, kanuni na taratibu. Kumekuwepo na matamko ya viongozi mbali mbali wa Kanisa, lakini hayakufua dafu. Mwaka 1992 kulichapishwa hati “Kutoka katika mateso, kuelekea katika matumaini” na hapa mapendekezo 50 yaliyotolewa. Hapa ikamriwa kwamba, watuhumiwa wasimamishwe na kuacha kutoa huduma mara moja, ili kutoa nafasi kwa sheria na madaktari kutekeleza wajibu wao bila kuingiliwa.

Kashfa ya nyanyaso za kijinsia iliyolitikisa Kanisa Katoliki nchini Ireland, ilipelekea Baraza la Maaskofu Katoliki nchini humo kujizatiti katika kupambana na kashfa hii na hatimaye, kukachapishwa hati iliyoanza kutumika kunako mwaka 1997. Baba Mtakatifu Yohane Paulo II, mnamo mwaka 2001 kwa Barua binafsi Motu proprio, Sacramentorum sanctitatis tutela, yaani Ulindaji wa Utakatifu wa Sakramenti, alitoa taratibu za mchakato wa kuendesha kesi hizo katika Mahakama za Kanisa. Mnamo mwaka 2010 Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kwa Tamko, Reformatio Normae gravioribus delictis, juu ya marekebisho ya kanuni za makosa makubwa ya uhalifu, aliziboresha taratibu hizo kwa baadhi ya vipengele ambavyo vilikuwa havikueleweka barabara! Akatambua na kukiri kwamba, nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo ni kosa kubwa la kimaadili na linapaswa kushughulikiwa na Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa.

Lengo ni kuliwezesha Kanisa kuendeleza Utume wake wa kutaka kudhibiti uhalifu unaoweza kutendwa na waamini; pamoja na kumrekebisha mhalifu; kutenda haki kwa waliokosewa; na kuondoa kashfa (Rej. CIC, c. 1341). Kati ya makosa ya uhalifu, yapo yale ambayo yanatambuliwa kuwa ni makosa makubwa ya uhalifu, Delicta graviora, na yametengwa ili kushughulikiwa, sio tena na Askofu Jimbo wala Wakuu wa Mashirika ya Kitawa na kazi za kitume, bali na Mahakama maalumu ya Baba Mtakatifu.

Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kunako mwezi Machi 2010 akaitisha mkutano wa Baraza la Maaskofu Katoliki Ireland kujadili kuhusu kipeo cha kashfa ya nyanyaso za kijinsia nchini humo na hatimaye, akachapisha “Barua ya Kichungaji kwa ajili ya Watu wa Mungu”. Tangu mwaka 2008, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akaanza kukutana na waathirika wa nyanyaso za kijinsia kutoka sehemu mbali mbali za dunia, dhamana na wajibu ulioendelezwa baadaye na Baba Mtakatifu Francisko. Mwongozo wa Kuwalinda Watoto Wadogo ukachapishwa. Mwaka 2012, kukafanyika Kongamano la Kimataifa lililowashirikisha wawakilishi kutoka sehemu mbali mbali za dunia na huo ukawa ni mwanzo wa Kituo cha Kulinda Watoto Wadogo, Chuo Kikuu cha Kipapa cha Gregorian chini ya uongozi wa Padre Hans Zollner, kama Rais wake ili kulisaidia Kanisa kuunda viongozi watakaosaidia mchakato wa kuwalinda watoto wadogo dhidi ya nyanyaso za kijinsia.

Maaskofu na viongozi wakuu wa Mashirika ya kitawa na kazi za kitume watakaoshindwa kuwalinda watoto dhidi ya nyanyaso za kijinsia wataondolewa kutoka katika nyadhifa zao. Hivi ndivyo Baba Mtakatifu Francisko anavyoandika kwenye Barua yake Binafsi ya kichungaji, “Kama Mama mpendelevu” iliyochapishwa Juni, 2016. Anasema haya ni kati ya makosa makubwa ambayo yamebainishwa barabara kwenye Sheria, Kanuni na Taratibu za Kanisa. Baba Mtakatifu anapenda kuwahimiza viongozi wa Kanisa kuwa macho dhidi ya nyanyaso za kijinsia wanazoweza kufanyiwa watoto wadogo; anaonesha hatua zitakazochukuliwa ili kutekeleza vifungu vya Sheria ambavyo viko tayari kwenye Sheria za Kanisa Namba 193§ 1 na Sheria za Kanisa la Mashariki Namba 975§1. Mkazo hapa ni wajibu wa viongozi wa Kanisa katika kutekeleza dhamana na utume wao!

Kunako mwezi Novemba 2014, Baba Mtakatifu Francisko akaanzisha Mahakama maalum ndani ya Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa kushughulikia kesi za makosa makubwa ya uhalifu, Delicta graviora, kesi ambazo kwa sasa zinashughulikiwa naAskofu mkuu Charles Jude Scicluna wa Jimbo kuu la Malta, ambaye pia ni Katibu Mwambata wa Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa. Kunako mwaka 2018, kashfa ya nyanyaso za kijinsia ikaligusa na kulitikisa Baraza la Maaskofu Katoliki Chile, baada ya mkutano wao na Baba Mtakatifu Francisko, Maaskofu wote nchini humo wakaandika barua ya kung’atuka kutoka madarakani kutokana na uzembe uliojitokeza. Baba Mtakatifu akachambua majina ya waliotuhumiwa zaidi na kuridhia uamuzi huu.

Mwezi Agosti 2018, Baba Mtakatifu akaandika Barua kwa Watu wa Mungu nchini Chile. Nyanyaso za kijinsia ni kielelezo madhubuti cha kumong’onyoka kwa maadili na utu wema, ni matumizi haramu ya madaraka na kwamba, hii ni kashfa kubwa dhidi ya utu na heshima ya binadamu; maisha na utume wa Kanisa. Kashfa hizi ni tendo la aibu sana. Baba Mtakatifu Mwezi Januari 2019 akaandika Barua kwa Watu wa Mungu nchini Marekani baada ya maisha na utume wa Kanisa nchini humo kutiwa dosari kutokana na kashfa za nyanyaso za kijinsia zilizowagusa hata viongozi wakuu wa Kanisa. Hii ni changamoto kubwa kwa Kanisa kujikita katika toba na wongofu wa ndani, kwa kubadili tabia na mwelekeo katika maisha na utume wake; ni wakati wa kupyaisha jinsi ya kusali na kumwilisha sala katika uhalisia wa maisha pamoja na kuratibu matumizi ya rasilimali fedha na mali ya Kanisa na kwamba, uongozi ndani ya Kanisa ni huduma kwa watu wa Mungu na wala si kichaka cha kujitafutia mali, utajiri na umaarufu usiokuwa na mvuto wala mashiko kwa ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa la Kristo!


Maoni


Ingia utoe maoni