Baraza Kuu la Mfuko wa Yohane Paulo II Ukanda wa Sahel, ulioanzishwa kunako mwaka 1984 ili kudhibiti kuenea kwa Jangwa na Sahara, limeanza mkutano wake wa mwaka tarehe 18 Februari 2019 na unatarajiwa kuhitimishwa tarehe 22 Februari 2019 huko Dakar, Senegal. Mfuko huu kwa sasa unasimamiwa na kuratibiwa na Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu na fungamani ya Binadamu. Katika mkutano huu Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu anashiriki.
Pia Maaskofu wanaoshiriki katika mkutano huu ni wale wanaotoka: Burkina Faso, Senegal, Mauritania, Niger, Cape Verde, Ciad, Gambia, Guinea Bissau na Mali, wanaongozwa na Askofu Sanou Lucas Kalfa kutoka Burkina Faso ambaye kwa sasa ndiye Mwenyekiti. Ujumbe kutoka Baraza la Maaskofu Katoliki Italia na Baraza la Maaskofu Katoliki Ujerumani unashiriki kwani, wao ndio wafadhili wakuu wa Mfuko wa Yohane Paulo II kwa Ukanda wa Sahel.
Baraza kuu la Mfuko wa Yohane Paulo II Ukanda wa Sahel linapitia miradi mbali mbali itakayogharimiwa na Mfuko huu kwa mwaka 2019. Kulikuwa na jumla ya miradi 125 iliyo gharimiwa kwa kipindi cha mwaka 2018. Ukanda wa Sahel ni kati ya maeneo maskini sana Barani Afrika na mara kwa mara limekuwa likiathirika sana na mabadiliko ya tabianchi. Kwa bahati mbaya sana, ni eneo pia ambalo limekuwa likihifadhi makundi ya kigaidi yanayohatarisha amani na usalama wa raia na mali zao.
Kanisa linapenda kuwekeza katika Ukanda wa Sahel kwa ajili ya kudhibiti kuenea kwa Jangwa la Sahara; kukuza na kudumisha kilimo bora na endelevu; ufugaji wa kisasa pamoja na kilimo cha uwagiliaji pamoja na kuhakikisha kwamba, wananchi wengi zaidi wanapata maji safi na salama. Kanisa kwa kushirikiana na wadau mbali mbali wa maendeleo, linapenda pia kuwekeza katika nishati rafiki kwa mazingira. Juhudi hizi zinakwenda sanjari na elimu, mafunzo na majiundo makini kwa rasilimali watu, ili kusaidia mchakato wa maboresho ya maisha ya watu.
Huduma ya maendeleo fungamani ya binadamu ni sehemu ya mkakati wa majadiliano ya kidini kati ya Wakristo na Waislam bila kusahau sera na mikakati inayopania kudhibiti wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji kutoka katika Ukanda wa Sahel. Waathirika wakuu ni vijana wanaotafuta fursa za maisha bora zaidi ughaibuni. Lakini kwa bahati mbaya, wanakumbana na mazingira hatarishi ugenini!
Maoni
Ingia utoe maoni