Baba Mtakatifu Francisko amemteua Kardinali Kevin Joseph Farrell, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha kuwa “Camerlengo” mkuu wa Kanisa Katoliki. Huyu ni kiongozi mkuu wa shughuli za Kanisa wakati kunapotokea kwamba, kiti cha Khalifa wa Mtakatifu Petro kiko wazi kwa sababu mbali mbali. Kabla yake, dhamana hii ilikuwa inashikiliwa na Hayati Kardinali Jean-Louis Tauran, aliyekuwa Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini.
Kardinali Kevin Joseph Farrell, alizaliwa kunako tarehe 2 Septemba 1947 huko Dublin, nchini Ireland. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 24 Desemba 1978. Mtakatifu Yohane Paulo II, tarehe 28 Desemba 2001 akamteuwa kuwa Askofu msaidizi wa Jimbo kuu la Washington, DC., nchini Marekani na kuwekwa wakfu tarehe 11 Februari 2002. Tarehe 6 Machi 2007, akateuliwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Dallas nchini Marekani.
Tarehe 15 Agosti 2016 akateuliwa na Papa Francisko kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha, baada ya Baba Mtakatifu Francisko kufanya mabadiliko makubwa katika Sekretarieti kuu ya Vatican kwa kuunganisha kwa pamoja, Baraza la Kipapa la Walei pamoja na Baraza la Kipapa la Familia hapo tarehe 1 Septemba 2016. Ni kiongozi mwenye uzoefu mkubwa katika masuala ya uchumi, fedha na uinjilishaji sanjari na uhamasishaji wa miito mitakatifu ndani ya Kanisa yaani: wito wa ndoa, maisha ya wakfu pamoja na upadre.
Historia ya Kanisa Katoliki inaonesha kwamba, kuanzia karne ya kumi na moja, kulikuwepo na kiongozi aliyejulikana kama “Camera thesauraria” yaani “Mhazini wa Kanisa” aliyepewa dhamana ya kuratibu masuala ya fedha na mali ya Kanisa. Dhamana hii inatekelezwa hasa zaidi wakati ambapo kiti cha Ukulu wa Mtakatifu Petro kiko wazi, kama ilivyokuwa baada ya Baba Mtakatifu Benedikto XVI, kung’atuka kutoka madarakani hapo tarehe 28 Februari 2013. Kunako Karne ya 12, Mkuu wa Ofisi hii alijukana kama “Camerarius” au “Camerlengo”.
Kadiri ya miaka ilivyozidi kuyoyoma na Mama Kanisa kusoma alama za nyakati, Camerlengo ambaye kwa Kiswahili chepesi tungeweza kumwita “Mlinzi” au “Mratibu”akapewa dhamana kuwa Katibu mkuu wa shughuli za Kanisa pamoja na kuratibu masuala ya sheria na kesi mbali mbali ndani ya Kanisa. Ni kiongozi aliyekuwa juu ya Mahakama zote zilizokuwa chini ya Vatican. Tarehe 29 Juni 1908 Papa Pio wa tisa, katika Waraka wake wa kichungaji “Sapienti Consiglio” akamrudishia Camerlengo madaraka aliyokuwa nayo kwa miaka iliyopita, yaani kusimamia fedha na mali ya Kanisa wakati ambapo kiti cha Ukulu wa Mtakatifu Petro kiko wazi.
Kunako mwaka 1967 Mtakatifu Paulo VI, katika Waraka wake wa kichungaji “Regimi Ecclsiae Universe", alibainisha kwamba, ikiwa kama Camerlengo anazuiliwa kutekeleza wajibu wake kisheria, basi msaidizi wake afanye kazi kuanzia pale ambapo kiti cha Ukulu wa Mtakatifu Petro kiko wazi hadi uchaguzi wa Papa Mpya utakapofanyika. Mtakatifu Yohane Paulo II katika Waraka wake wa kichungaji “Pastor Bonus wa mwaka 1988 akathibitisha tena dhamana hii katika maisha na utume wa Kanisa. Kunako mwaka 1996, Papa Yohane Paulo wa Pili akatamka wazi katika Waraka wake wa kichungaji “Universi Dominici Gregis” kwamba, ni viongozi wakuu wawili tu ambao nyadhifa zao haziwezi kukoma wakati ambapo kiti cha Ukulu wa Mtakatifu Petro kiko wazi. Hawa ni Camerlengo na Mhudumu mkuu wa Idara ya Toba ya Kitume.
Maoni
Ingia utoe maoni